Habari ndugu msomaji wetu wa makala za kilimo. Ni matumaini yetu unaendelea vizuri na majukumu ya kila siku katika kutafuta mafanikio. Tunashukuru kwa ufuatiliaji wa makala za kilimo, siku zinavyozidi kwenda  tunaendelea kupata watu wengi wenye kiu ya kupata maarifa ya kilimo kupitia makala tunazoweka hapa kwenye AMKA MTANZANIA. Kutokana na somo ambalo tumekua tukijifunza la kilimo cha nyanya, tumekua tukipata maswali, na mengine yamekua yakijirudia mara kwa mara. Hivyo tunapendelea kujibu baadhi ya maswali hayo kwa faida ya wasomaji wote. 
Karibu tujifunze kupitia maswali hayo:
Mkuu asante sana kwa elimu hii nzuri. Naomba unijuze gharama za mtaji na kufunga greenhouse katika shamba la matikiti maji. Pia specifications za size.
Hamis Msigwa
Habari Bwana Hamisi
Natumai unaendelea vizuri, tunashukuru sana kwa kutuandikia email kwa ajili ya kupata ushauri kuhusu green house.
Kwanza tunakupongeza kwa wazo la greenhouse, maana ni tecknolojia nzuri na ndiko kilimo chetu kinakoelekea.
Ila tunapenda pia kukushauri mambo mawili au matatu hivi:
1. Greenhouse inafaa sana kwa mazao yanayoota kwenda juu na sio kwa yanayo tambaa kama tikiti. Kwa sababu mazao yanayotambaa yanachukua nafasi kubwa maana itabidi upande mbalimbali. Na lengo la greenhouse ni kuongeza uzalishaji wenye ubora, hivyo lazima tuangalie swala la uchumi, matumizi mazuri ya nafasi ni muhimu.
2. Mazao yanayofanya vizuri kwenye greenhouse ni nyanya, pilipili hoho na kidogo matango, mabiringanya, bamia na ngogwe. Ila hasa hayo mawili ya mwanzo ndio mazuri zaidi.
3. Greenhouse bei zake zinatofautiana kutokana na sababu mbalimbali. Kwanza supporting materials za hiyo green house. Kama material yake ni chuma (metals) bei yake ni ya juu zaidi kulinganisha greenhouse ya materials ya miti. Lakini pili bei inatofautiana kutokana na size ya green house unayotaka kutengeneza. mfano kuna ya 8m X 15m (upana mita 8 urefu mita 15),  15m X 20m, 15m X 30m, greenhouse ya robo eka na hata ya nusu ekari
Greenhouse unaweza kupata kutokea hapa nchini au pia unaweza kuagiza toka nje ya nchi. Mfano unaweza kuagiza to China, na wanakupa machaguo (options) mbalimbali za bei na ubora wa greenhouse yenyewe, inakua kazi kwako tu kukachagua.
Kwa vyovyote vile unavyotaka tunaweza kukupatia usaidizi huo wa kupata greenhouse unayoihitaji, iwe ni kutoka nje au ndani ya nchi.
Natumaini ukipitia ushauri wako hapo juu, utaelewa zaidi na ukituandikia tena tutaweza kukusaidia zaidi maana sasa utakua na specifications za greenhouse lakini pia utakua unajua unataka kulima nini kwenye hiyo greenhouse. Lakini tutaongelea kwa undani kilimo cha greenhouse kwenye makala za mbele.
Natamani sana kufanya shughuli za kilmo, tatizo kubwa nililonalo ni
ukosefu wa pembejeo bora za kilimo, unaweza kunisaidia kuyafahamu
makampuni au mashirika ya kilimo ili waweze kunisaidia?
Hongera ndugu kwa kuonyesha nia ya kufanya kilimo, pembejeo ni suala ambalo limekua ni changamoto kwa wakulima na wawekezaji wengi wa kilimo, ni ukweli usiopingika kwamba ili kupata mavuno mengi ni sharti uanze na pembejeo zilizo bora. Tunapozungumzia pembejeo tunajumuisha, mbegu, madawa, mbolea pamoja na zana za kilimo kama mashine mbalimbali. Kuhusu kuyafahamu makampuni ya pembejeo inategemea na eneo ulilopo pia na zao unalotaka kulima, maana kuna sehemu kampuni zina matawi kuna sehemu hakuna ,kutokana na soko la pembejeo zao. Pia makampuni yanatofautiana katika pembejeo wanaozalisha na kusambaza, kuna kampuni zinajihusisha na madawa tu (mfano Twiga Chemical), nyingine mbegu tu (mfano East west, East Africa Seed, Seed Co.), nyingine mbolea tu (mfano Yara, au Minjingu), ila kampuni nyingi zinajihusisha na pembejeo zaidi ya moja. Mfano Kibo seed, Suba Agro, Balton Tz, Meru Agro,n.k. Pia kama upo maeneo ya ndanindani, makampuni mengi hayafiki huko moja kwa moja, hutumia mawakala wa pembejeo. Ila kama nilivyosema awali pembejeo zitategemea unataka kuzalisha zao gani. Tutashukuru kama utatuandikia na kutueleza mahali ulipo na zao unalotaka kulima ili uweze kupatiwa ushauri wa aina ya mbegu, utunzaji n.k

Ndng. Daudi,

Binafsi nakushukuru kwa Elimu ya zao la nyanya, imefumbua macho yangu kwa kiwango kikubwa sana. Je tunaweza kupata Elimu kama hiyo kwa zao la matikiti maji?

Natanguliza Shukrani

Tunashukuru kwa kua mwanafunzi mzuri. Kifupi ni kwamba mazao mengine kama matikiti, pilipili hoho, vitunguu n.k, makala zake zitakua zinatujia hapa kwenye AMKA MTANZANIA.
Asante kwa somo zuri kuhusu kilimo cha nyanya.
Mimi nimeanzisha bustani yenye miche 800 hivi. Nimeotesha na kupandikiza mbegu aina ya ‘MWANGA’ lakini siijui vema.
Ningependa kama unayo maelezo yake; ni mbegu fupi au ndefu? Ni hybrid au ya kawaida? Uzaaji wake ni mzuri kibiashara au laa! nk.
Nakutakia heri ktk utoaji elimu hii adhimu kwa wajasiriamali.
Ndimi,
D.M.Milambo
Asante sana Bwana Milambo kwa maswali mazuri. Kwa ufupi Nyanya aina ya Mwanga ni mbegu ya kawaida na kwa ukuaji aina hii ni fupi. Hii ni aina mpya ya Nyanya inayosambazwa na Kibo seed company. Katika tafiti za Karibuni aina hii imeonekana kuweza kuvumilia magonjwa kama ukungu, japo pia inategemea na maeneo na maeneo. Mazao ya aina hii yanakadiriwa kua tani 30 hadi 40 kwa ekari moja. Sifa nyingine za aina hii ya nyanya ni kua na ganda gumu hivyo kuweza kukaa muda zaidi kuliko aina nyingine, lakini pia matunda yake ni makubwa na ni moja ya nyanya zinazopendwa. Mbegu nyingi za hybrid za nyanya ni ndefu japo pia zipo chache ambazo ni fupi.
 Asante sana. Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Kwa ushauri au maswali, Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.comau dd.mwakalinga@gmail.com