Peter Drucker, aliyekuwa mtaalamu wa usimamizi kwenye biashara, aliwahi kusema kwamba kwa kuwa lengo la biashara ni kutengeneza wateja, biashara yoyote ina majukumu mawili tu ya msingi; masoko na ubunifu. Vitu hivi viwili ndio vinaleta faida kwenye biashara, vingine vyote vinaleta gharama.
Leo katika makala hii ya kona ya mjasiriamali tutajadili vitu hivi viwili muhimu sana na jinsi unavyoweza kuvitumia kukuza biashara yako. Wewe kama mfanyabiashara una jukumu kubwa la kufanya ili kuweza kunufaika vizuri kupitia biashara unayofanya.
1. Masoko.
Masoko ni eneo muhimu sana kwenye ukuaji wa biashara yako. Unahitaji kuwajua wateja wa biashara yako ni watu gani na ni jinsi gani unavyoweza kuwafikia. Biashara yako haiwezi kumudu ushindani na kukuletea faida kama haina wateja. Na njia bora kabisa ya kutengeneza wateja kwenye biashara yako ni kutatua tatizo. Angalia ni tatizo gani ambalo watu wanalipitia na wapo tayari kulipia suluhisho la tatizo hilo kama likiwepo. Kwa kuja na suluhisho utapata watu ambao wanataka kuondokana na tatizo walilonalo.
Kama ukiweza kupata tatizo kubwa na linalowasumbua watu wengi na ukaliletea suluhisho basi utaweza kupata wateja wengi na wao wakakuletea faida kubwa. Kama utatatua tatizo linalosumbua watu wachache utapata wateja wachache pia.
Katika masoko kuna kitu muhimu sana cha kuzingatia ambacho ni mteja kujua kwamba wewe upo na unaweza kutatua tatizo lake. Hivyo unahitaji njia ya kuweza kumfikia mteja wako. Hapa kuna kutangaza biashara yako kupitia njia mbalimbali ambazo zitamfikia mteja wako. Unahitaji kujua mteja wako yuko wapi na ni njia gani itakuwa rahisi kumfikia. Kwa mfano kama unafanya biashara ambayo wateja wake ni wanafunzi, unajua sehemu rahisi ya kuwapata wanafunzi ni maeneo ya shuleni au vyuoni. Kutumia gharama yoyote na kutangaza biashara yako sehemu ambayo wanafunzi wengi hawawezi kupata matangazo hayo ni kupoteza fedha zako.
Kitu kingine kikubwa cha kuzingatia kwenye kujiweka kwenye soko ni kujua kitu cha tofauti ulichonacho wewe. Kama mteja anaweza kununua kutoka kwa mtu mwingine kwa nini aje anunue kwako. Unahitaji kuwa na kitu cha tofauti ambacho kitawavutia wateja kuja kwenye biashara yako. Usifanye biashara kama watu wengine wanafanya, hata kama ni biashara inayofanana, unahitaji kuwa na kitu cha kukutofautisha na kitakachowafanya wateja wafurahie kuja kwako.
2. Ubunifu.
Kitu kingine kikubwa cha kuzingatia ili kukuza biashara yako na kupata mafanikio ni ubunifu. Kama biashara haina ubunifu haina safari ndefu kwenye ulimwengu wa sasa ambao una changamoto nyingi sana za kibiashara. Kwa kuwa biashara unayofanya kila mtu anaweza kuifanya na kwa kuwa mahitaji ya watu yanabadilika, unahitaji ubunifu ili kuweza kuendelea kuwepo kwenye biashara na kuikuza zaidi.
Unahitaji ubunifu ili kuweza kujitofautisha na wafanyabiashara wengine wanaofanya biashara kama unayofanya wewe. Ukianza biashara ambayo inaonesha mafanikio, kuna watu wengi wataiga biashara hiyo, hivyo kama hutakuwa na ubunifu, watu watakuja kukuondoa kwenye biashara uliyoanzisha mwenyewe.
Ubunifu ni muhimu pia kwenye kuendelea kutatua matatizo ya wateja wako. Tumeona kwamba unahitaji kujua ni matatizo gani watu wanayo na kisha biashara yako iyatatue. Sio kwamba ukishajua matatizo haya basi ndio umeshafanikiwa, kadiri siku zinakwenda matatizo ya watu nayo yanabadilika. Hivyo kuendelea kutoa suluhisho la zamani kwa tatizo jipya utapoteza wateja wengi. Unahitaji kuwa mbunifu na kuona ni nini kinaendelea kwenye maisha ya wateja wako na jinsi unavyoweza kuiboresha biashara yako iweze kuenda na mabadiliko hayo.
Tuna changamoto kubwa sana ya ubunifu kwenye biashara hapa Tanzania, watu wanapenda kujua biashara inayolipa ili waweze kuingia bila hata ya kusumbua akili zao. Hii inapelekea watu wengi kujikuta wakifanya biashara moja na hivyo kujikuta kwenye ushindani mkubwa. Usitake na wewe kuwa sehemu ya matatizo haya ambayo yataizuia biashara yako kukua.
Fanyia kazi maeneo haya makubwa kwenye biashara yako, masoko na ubunifu na utaweza kuendesha biashara yako inayokua na kukuletea mafanikio.
TUPO PAMOJA.
Asante
LikeLike