Uaminifu ni jambo la muhimu sana na wengi wetu tumekuwa wepesi wa kuona wengine si waaminifu kwa kuwa wameenda kinyume na tulivyotegemea iwe. Mfano ni rahisi sasa kusikia wengi wetu tukilalamikia viongozi wanaokosa uaminifu kwa kufanya vitendo visivyofaa au hata kuingia mikataba isiyo na manufaa kwa wengi , ni kweli ni habari mbaya, haifurahishi na inaumiza sana tu katika hali ya kawaida.  Lakini tunasahau kuwa hata katika maisha yetu ya kawaida watu wengi wamekosa uaminifu sana, mfano mashuleni na hata vyuoni unakuta watu wengi wanafaulu mitihani yao lakini si kwa njia sahihi, si kwa kufanya kama ipasavyo kufanya ili wafaulu bali njia na mbinu zinazotumika si njema na si sahihi sana machoni pa watu na hata jamii kwa ujumla, lakini kwa kuwa wengi wanafanya hayo na wanaona yakiwafanikisha wanaona ni kitu sahihi tu.
Au tuna waalimu ambao hawasahihishi mitihani kwa haki bali wanapewa kitu fulani kidogo ili waweze pindisha matokeo ya mitihani na kwa kuwa labda mtu huyo amekuwa akifanya hivyo kwa muda mrefu anaona ni kitu sahihi au kwa kuwa haijulikani na wengi basi anaona yu sahihi tu.  Lakini kuna wanafunzi wenyewe ndio wanaowafuata walimu na kuomba wapewe majibu au namna ya kuweza kufaulu mitihani yao kwa urahisi kwa kuwapa kitu kidogo, na kwa kuwa pengine mtu anakuwa amefanya yeye kama yeye anajua yu salama na sahihi wala hasikii kuhukumiwa ndani mwake na ikitokea amesikia hivyo anapuuzia tu.
Maofisini wafanyakazi wengi wamekuwa si waaminifu pia, hasa kwenye swala la muda, wengi wanatumia muda wa kazi kufanya mambo ambayo hayana tija kwa waajiri wao, muda ambao mwajiri anawalipa wao wanafanya mambo ambayo hayamwingizii mwajiri faida, wengine wanachelewa sana kufika ofisini, au wanawahi kutoka kabla ya muda na kwa kuwa labda hakuna mtu anayemfuatilia basi anajiona yuko sahihi kufanya hivi, lakini kuna wengine akisikia tu bosi hayupo siku hiyo basi atachelewa kufika ofisini au atachelewa sana au anaweza wahi kutoka kwa kuwa hakuna mtu wa kumfuatilia au kumuulizwa kwa nini anafanya hivyo. Wengine pia wamekuwa wadanganya waajiri wao kwa kuwapa taarifa zisizo sahihi, mfano mtu ameagizwa akanunue kitu fulani dukani akifika huko ataongeza bei na hata kutengeneze risiti bandia ili tu aweze kuchukua kipato zaidi na kwa kuwa hana mtu wa kuweza kuligundua hilo basi anaona yu salama, wengi wananunua hata vitu visivyo na ubora ilimradi tu aweze kupata kitu  kidogo na kufikisha taarifa za uongo kwa mwajiri wake.
Imefikia hatua hadi majumbani mwetu uaminifu umekosekana yaani watu wamezoea tabia mbaya mpaka imeonekana ni sahihi, mfano unakuta hata mama pale nyumbani yupo tayari kumdanganya mumewe juu ya matumizi fulani ili mradi tu aweze kutimiza malengo yake , au mwingine anafikia hatua ya hata kuwatesa watu wa nyumbani mwake kwa kuwapa vitu vilivyo chini ya kiwango ili mradi tu aweze kufanya yake, watu wengi wamekosa uaminifu kabisa.
Kitu cha kushangaza watu niliowataja hapo juu ni watu wa kwanza kulaumu viongozi na serikali kwa ujumla kuwa imekosa uaminifu, wanasahau kwamba nao ni sehemu ya serikali, wanasahau kwamba nao popote pale walipo wana wajibu wa kuwa mawakili wa uaminifu, wanatakiwa kuwa waaminifu popote pale walipo haijalishi ni eneo gani, pale utakapokuwa mwaminifu kuna mwingine atajifunza kitu kwako, wapo utakaowafanya wajione kuwa nao wana wajibu katika hilo, watagundua kuwa hao watu waaminifu wanatengenezwa kuanzia huku majumbani mwetu, jiulize kama wewe si mwaminifu je wanao watakuwaje? Jiulize ni mbegu gani unapanda kwa jamii inayokuzunguka?  Unaweza kuamua kuanzia leo, kutimiza majukumu yako kwa uaminifu hata kama hakuna mtu anayekuomba ripoti, ni kwa faida yako ndugu, amua leo kuwahi kazini, ukifika fanya kazi kwa uaminifu, achana na mipango isiyo ya kiaminifu maana inakufanya uishi kwa wasiwasi na siyo salama kwa afya yako pia, ukiacha mbali hasara nyingine nyingi tu.
Anza wewe kuwa mwaminifu na wengine watajifunza kwako.
Imeandikwa na Beatrice Mwaijengo
Mobile number: +255 755 350 772
Email: bberrums@gmail.com