Kama kuna kazi ngumu hapa duniani basi ni kuishi. Ndio maisha ni
mazuri na ndio maisha ni matamu ila ni kazi kubwa sana kuweza kuyaishi.
Ni kazi kubwa kuyaishi kwa sababu huwezi kuishi maisha ya peke
yako. Umezungukwa na watu wengi na watu hawa wana tabia tofauti tofauti. Watu
wote hawafanani tabia.
Kuna wakati unafikiri kama watu wote wangekuwa kama fulani basi
mambo yangekuwa mazuri sana. Saa nyingine unafikiria kama wateja wote wangekuwa
kama mteja fulani basi biashara ingekuwa nzuri sana. Au wakati mwingine
unafikiria kama bosi wako angekuwa na roho ya tofauti na aliyonayo sasa basi
maisha yako ya kazi yangekuwa mazuri sana.
Lakini ukweli ndio huo kwamba watu hatufanani na pamoja na
tofauti zote hizo bado unahitaji kushirikiana na watu wote hao.
SOMA; Tabia Saba Za Watu Wasiokuwa Na Mafanikio.
Matatizo yote ya kwenye mahusiano, yawe ya kindugu, ya
kibiashara, ya kikazi au hata ya kimapenzi yanaanzia pale mtu mmoja anapotaka
kumbadilisha mwingine. Yaani ikishafikia hatua hii kwamba mtu mmoja anataka
mwingine abadilike, ndio matatizo makubwa sana yanaibuka.
Unajua ni kwa nini? Kwa sababu mwanadamu atafanya kitu chochote
kile kinachowezekana ili mradi tu asibadilike. Watu hawapendi kubadilishwa na
wanapenda kuendelea kuwa vile walivyo. Tena kama ndio mtu mzima, ndio basi
kabisa, atahakikisha anakataa kubadilika hata kama kufanya hivyo kunagharimu
maisha yake.
Wakubali watu vile walivyo, au kama huwezi kuwakubali walivyo
achana nao. Kama wataona wewe ni wa muhimu sana na hawawezi kukupoteza basi
watabadilika wao wenyewe. Na mtu anapoamua yeye mwenyewe kubadilika inakuwa
rahisi kwake kubadilika hata kwa kiasi kidogo. Ila kama wewe ndio unamlazimisha
mtu abadilike, okoa nguvu zako.
TAMKO LA LEO;
Najua matatizo makubwa kwenye mahusiano ya watu huwa yana anza
pale watu wanapojaribu kuwabadilisha wengine. Najua ya kwamba binadamu hawapendi
kubadilishwa. Sitapoteza nguvu zangu kutaka kumbadilisha mtu. Nitamkubali mtu
kama alivyo na kama siwezi nitaachana naye iwe ni mteja, bosi, ndugu au mwingine
wa karibu. Muda wangu ni wa thamani sana siwezi kuupoteza kwa kufanya kazi
ambayo haileti matunda.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita
Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi
yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365
bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo
maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya
facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya
email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na
KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata
utaratibu.
TUPO PAMOJA.