Kama Unafikiri Mafanikio Yako Hivi Tu, Tayari Umeshapotea.

Maisha ya binadamu hapa duniani yanaanzia pale anapozaliwa hadi anapokufa. Mara kwa mara utasikia watu wanasema, aliishi maisha marefu au aliishi maisha mafupi, wakimaanisha miaka aliyoishi hapa duniani tangu kuzaliwa kwake hadi kufa kwake. Kipindi chote hiki alichopitia huyu binadamu anakutana na mambo mengi sana, kadri ya muda atakaouchukua kwenye maisha.
Hebu tuangalie kidogo maisha ya binadamu huyu kuhusu upande wa mafanikio, kwa maana ya maendeleo atakayoyapata huyu binadamu katika maisha yake ya kila siku. Huu ni upande mmoja wa maana ya mafanikio kama wengi wanavyofikiri. Wanaona  kwamba mafanikio ni uwezo alionao binadamu wa kukusanya vitu. Wanatofautisha uwezo kutokana na vitu alivyokusanya binadamu.
Kwa mfano, kama mmoja amesoma sana mpaka akapata shahada moja au mbili, utasikia wakisema, amefanikiwa kusoma hadi akapata shahada. Kama umejenga au hata kununua gari, utasikia wakisema tena, amefanikiwa kwa kujenga nyumba au kununua gari.
Kwa hivyo basi, mafanikio kwa wengi wetu ni kiwango cha mali au vitu ambavyo amekusanya mhusika tu na si vinginevyo. Kwa ujumla, jamii inaangalia ulivyonavyo na vinavyoonekana au vinavyoweza kupimwa. Kwa mfano, elimu itapimwa kwa vyeti. Kama mtu atakuwa hana chochote kinachoonekana au kupimika, inaamuliwa kwamba, huyu hajafanikiwa. Watakuwa wanasema hana mafanikio yoyote.
Hebu tuangalie kwa makini na kujiuliza, je, haya ni mafanikio kweli? Vilevile tuangalie kama ni sahihi kuyaita haya kuwa ni mafanikio. Kabla ya kwenda mbali labda tungejiuliza swali hili. Je, maisha ni nini? Kwa sababu gani tunaishi au je, kuna shabaha au lengo lolote katika maisha?
Swali hili au maswali haya ni magumu sana kujiuliza binadamu. Yanataka kutumia busara ya hali ya juu kuyajibu na ni muhimu kupanua busara, ufahamu na utambuzi ili kupata majibu sahihi. Ni maswali ambayo yapo. Hata kama hujawahi kujiuliza, elewa tu kuwa kuna siku utajiuliza kwa njia moja au nyingine.
Kama hujawahi kujiuliza au huna majibu ya kweli, basi usiseme kuwa hakuna majibu. Kwa kuwa wewe hujui, usidhani kuwa wote hawajui. Tafuta kwa makini, tulia na kubali kujifunza ili upate maarifa. Jifunze kusikiliza ili upate faida ya kuelewa mambo.
Kila kitu hapa duniani kina sababu yake, hivyo hata maisha ni lazima yawe na sababu. Hata kama hatuijui, lakini sababu ipo tu. Wakati mtu anapozaliwa anakuwa makini na lengo lake, yaani sababu yake ya kuzaliwa. Lakini ufahamu huu huja kuchafuliwa na mazingira anayoyakutana baada tu ya kuzaliwa.
Anaanza kujenga malengo mengine mapya kadri anavyokua. Lile lengo kuu alilokuja nalo linaanza kuzibwa na malengo mengine yanayo badilika badilika kila wakati. Malengo haya yanatawaliwa na tamaa na akili au hisia. Haya yanakuwa mengi kwa kadri mtu huyu anavyokua.
Malengo haya yanakuwa yanabadilikabadilika kwa kuwa yanakuwepo kwa kutegemea hali ya wakatii huo, na mazingira mtu aliyomo. Yanategemea familia aliyokulia au anayokulia na jamii inayomzunguka. Kama amezaliwa katika familia yenye mali nyingi, basi na yeye atatamani kuwa na mali nyingi hapo baadaye. Atafurahia maisha ya kuhudumiwa kila kitu kuanzia kupikiwa na kufanyiwa kazi zote za nyumbani.
Ataweka malengo ya kuishi maisha kama uliyoyakuta hata kama hajajua kama uwezo huo atakuwa nao au la. Kama kwa mfano, atazaliwa familia ya kipato cha chini atakuwa na changamoto tofauti katika maisha.
Ninachotaka kusema hapa ni kuwa lile lengo letu la asili tunalozaliwa nalo tunaliacha, yaani ile sababu kubwa ya maisha, na kuanza kujipachika malengo mengine na kuyafanya ndiyo ya msingi. Mafanikio ya vitu tulivyokusanya hayawezi kutupatia furaha ya kweli kwenye maisha yetu.
Siku zote tunajiona tuna mapungufu na ndiyo maana kukusanya kwetu hakuna mwisho. Watu wanakwenda mbio huku na huko kwa malengo ya kukusanya vitu wakidhani kuwa wakivipata watakuwa na furaha ya kweli. Kwa mtazamo wangu, lengo la maisha ya binadamu ni kuwa binadamu wa kweli. Lengo ni kuonyesha ubinadamu, kuishi na kuonesha ubinadamu wako, yaani kuushusha ubinadamu au utu kwenye maumbile.
Pamoja na kuwa tunatafuta mafanikio ya kifedha na kuboresha maisha yetu kila siku, lakini hicho kinachoitwa binadamu na utu kinatakiwa kijionyeshe au kujibainisha katika maumbile kupitia kwa huyu binadamu au mtu. Maumbile ni mkusanyiko wa vitu vingi ikiwa ni pamoja na binadamu mwenyewe.
Mkusanyiko wa vitu ambavyo vinakwisha baada ya kutumika siyo lengo la maisha. Furaha ya kweli haipatikani kwenye vitu na ndiyo maana vinapokwisha au kuzoeleka, basi na furaha inapotea. Mhusika anakuwa ana huzuni kubwa sana anapopoteza vitu hivi na ndiyo maana kama unafikiri mafanikio yako hivi tu, yaani kukusanya tu vitu bila kuangalia upande wa pili, tayari umeshapotea.
Unakuwa umeshapotea kwa sababu mafanikio ya kweli hayategemei vitu vya nje peke yake. Mafanikio ya kweli ni yale ya ndani yako ambayo yatakufanya uwe na furaha muda mwingi bila kuyumbishwa na kitu chochote hayo ndiyo mafanikio. Lakini ukiwa unategemea mafanikio ya nje peke kukupatia furaha hiyo ni sawa na kuwa na mafanikio ya msimu, yakitoka na furaha imeondoka pia.
Ni muhimu kuwa makini sana tunapoangalia vitu kwenye hii dunia. Mafanikio ya leo tu, halafu kesho mafanikio yote yameondoka, basi hayo siyo mafanikio ya kweli. Ni vizuri tukawa na mafanikio ambayo hayaondoki na hayawezi kuondoka kamwe. Uwezo wa kukusanya vitu na mafanikio ni vitu viwili tofauti. Unaweza kukusanya vitu vingi lakini ukawa huna furaha ndani yako na hili ni tatizo kubwa na mafanikio yako yanakuwa hayajakamilika.
Ndiyo maana mimi nasita kuyaita ni mafanikio kwa kuwa kama ni mafanikio ya kweli, basi mhusika angekuwa na furaha kubwa sana katika maisha yake na bila shaka ingekuwa ni furaha ya kudumu.
Wale waliofanikiwa kwa mtazamo wangu, yaani kwa namna ninavyoyatazama mafanikio, wanaweza kuwa hawana vitu vingi kwenye maisha yao lakini wanafuraha kubwa sana kwenye maisha. Kumbuka, msisitizo hapa ni kuhakikisha unatafuta mafanikio huku ukijali utu ambao utakufanya uwe huru na furaha siku zote na siyo kuegemea upande mmoja tu.
Watu wenye mafanikio ya kweli hata nyuso zao na hali zao zinaonyesha neema tupu kuashiria furaha ya kweli waliyonayo na hayo ndiyo mafanikio katika maisha. Hali hii inaonyesha ukamilifu wa binadamu na yeyote aliyemiliki basi amepata mafanikio katika maisha. Anakuwa na uwezo mkubwa wa kujua nafasi yake katika maumbile na kuvipa vinginevyo nafasi yao katika maumbile.
Tunakutakia kila la kheri katika safari ya mafanikio, endelea kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kila siku kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.
Kwa makala nyingine nzuri karibu pia kwenye DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuboresha maisha.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 04 80 35,

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: