Ni ukweli usiopingika kwamba msingi wa kwanza na muhimu sana wa wewe kuweza kufikia mafanikio makubwa ni mtazamo chanya. Unaweza kufanya kazi kwa juhudi kubwa na maarifa, ila kama mtizamo wako haupo sahihi, huwezi kufikia mafanikio makubwa.
Mafanikio yoyote makubwa yanaanzia kwenye mtizamo wako kwanza na kisha ndio yanajitokeza kwenye maisha yako. watu wawili wanaweza kufanya kazi moja na wote wakaifanya kwa viwango sawa, ila mmoja akafanikiwa sana na mwingine akaishia kuwa kawaida. Kwa nje unaweza kuona huyu aliyefanikiwa ana bahati. Ila kama utapata nafasi ya kumchunguza kwa ndani utagundua ya kwamba kuna vitu vya tofauti ambavyo anavyo kwenye mtizamo wake vinavyomweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufanikiwa.
Leo katika makala hii tutaangalia tabia saba muhimu za watu ambao wana mtizamo chanya na zinazopelekea watu hawa kuweza kufikia mafanikio makubwa. Angalia ni ipi kati ya hizi unazo na kama huna basi uanze kubadili mtazamo wako ili mafanikio yawe uhakika kwako.
1. Kujiamini mwenyewe.
Kujiamini wewe mwenyewe ni msingi muhimu sana wa mafanikio makubwa kwenye maisha yako. katika safari yako ya mafanikio, utahitaji kufanya mambo ambayo ni mageni, wengi hawajawahi kuona yakifanywa. Na watu watakapoona unafanya, watakukatisha tamaa na kukuambia huwezi au utashindwa. Kama wewe mwenyewe unajiamini ni rahisi kuachana nao na kusonga mbele. Kama hujiamini ni rahisi kukubaliana nao na kuacha kufanya mipango yako mikubwa.
Kama tayari unajiamini wewe mwenyewe hongera sana. Kama bado hujiamini anza kujitengenezea mtazamo huu. Anza kujiona kwamba unaweza kufanya makubwa kwa ajili ya kufikia mafanikio makubwa.
2. Kuwa tayari kuona mambo bora kwa wengine.
Watu wanaofikia mafanikio makubwa sio wabinafsi kama watu wengi wanavyofikiri. Sio watu ambao wanajiangalia wao tu wanapata nini. Bali watu ambao wanafikia mafanikio makubwa ni wale ambao wanapenda kuona wengine wakiwa bora zaidi. Ni wale wanaopenda kuona maisha ya wengine yakiwa mazuri, na kama inawezekana uwe mchango wao kwenye kuboresha maisha haya.
Ni katika hali hii watu hawa wanakuwa tayari kutoa huduma bora sana kwenye kile wanachofanya, iwe ni kazi au biashara wakilenga wale wanapokea huduma zao wawe bora zaidi. Na katika kutoa huduma hizi bora, wanajitengenezea njia bora ya kufikia mafanikio makubwa. Kama bado hujaanza kuwafikiria wengine kuwa na maisha bora, anza sasa, hiki ni kitu kimoja ambacho kitaleta mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako.
3. Uwezo wa kuoa fursa kila mahali.
Hivi unajua kila mahali, ndio kila mahali kuna fursa. Kila hatua ya maisha yako unayopitia, iwe ya furaha au huzuni, iwe mafanikio au kushindwa, hapo kuna fursa nzuri sana ya wewe kufikia mafanikio makubwa zaidi.
Kuweza kuona fursa kila mahali ni kitu ambacho kinawatofautisha waliofanikiwa na wale wanaosukuma tu siku. Wanaosukuma siku hutafuta sababu ya kulalamika au kulaumu pale mambo yanapokuwa hayajaenda kama wao walivyokuwa wanategemea. Wenye mtizamo mzuri na wanaofanikiwa sana , huangalia hali ambayo wapo na kisha kujiuliza ni fursa gani ambazo naweza kuzipata kwenye hali hii.
Anza kufungua macho yako na uone fursa kila mahali ambapo unapita au unakuwepo. Huhitaji kutafuta fursa zaidi, unahitaji kuziona maana nyingi zimekuzunguka. Kwenye kila hali unayopitia, jiulize ninawezaje kutumia hali hii na ikawa fursa nzuri zaidi kwangu? Ukijiuliza swali hili na kwa mtizamo chanya utakaokuwa nao, utaona majibu mengi sana na mazuri.
4. Kufikiria zaidi suluhisho na sio tatizo.
Kila mtu kwenye maisha yake nakutana na matatizo mbalimbali, iwe amefanikiwa au hajafanikiwa. Sasa kinachowatofautisha waliofanikiwa na walioshindwa sio idadi au aina ya matatizo wanayopata, bali uwekezaji wa mawazo yao. Linapotokea tatizo watu ambao wanafikia mafanikio makubwa huwekeza mawazo yao kwenye kufikiria suluhisho la tatizo hilo. Hufikiria zaidi ni njia gani ambazo wakizitumia zinaweza kutatua tatizo hilo. Watu walioshindwa wao huwekeza mawazo yao kufikiria zaidi tatizo lililotokea. Watu hawa wanatumia muda mwingi kulichambua tatizo, na huenda kulalamika kwamba kwa nini wao ndio wapate tatizo hilo. Sasa njia hii haiwezi kusaidia kutatua tatizo hilo.
Anza sasa kupeleka mawazo yako kwenye suluhisho na sio tatizo. Fikiria zaidi jinsi ya kutatua kila hali ambayo unapitia, na utashangaa kuona majibu mengi sana yanakujia. Ukifanyia kazi hayo majibu utazidi kuelekea kwenye kilele cha mafanikio.
5. Kuwa tayari kutoa.
Kitu kimoja ambacho kinawafanya wenye mafanikio kuendelea kuwa na mafanikio zaidi ni utayari wao wa kutoa. Watu wenye mafanikio na wanaoendelea kupata mafanikio makubwa ni watoaji wazuri sana. Watu hawa wanaijua sheria ya dunia inayosema kwamba unapokea kile ambacho unakitoa. Hivyo wao wanaenda vyema na sheria hii kwa kuanza kutoa halafu wanajikuta wanapokea zaidi hata kama hawatarajii hivyo.
Watu ambao hawajafanikiwa hawapo vizuri kwenye kutoa. Watu hawa hawaielewi sheria ya dunia ya kwamba unapokea kile unachotoa. Wao huhangaika kufikiria kupata tu, huangalia ni jinsi gani ya kupata zaidi na hivyo kutumia nguvu nyingi na kupata matokeo madogo. Kubadili hili kuwa mtu wa kutoa. Tumia muda wako na nguvu zako kufikiria na kutekeleza njia ambazo unaweza kuwasaidia wengine au kutoa kwa wengine badala ya kufikiria ni jinsi gani unaweza kunufaika kutokana na wengine. Kwa kubadili hili tu, utaona fursa nyingi za kutoa kilicho bora kwa wengine na kadiri unavyotoa na wewe pia unapokea.
6. Ung’ang’anizi.
Watu waliofanikiwa sana na wanaoendelea kufanikiwa ni watu ambao ni ving’ang’anizi hasa. Ukiwaangalia watu hawa wanakuwa wameng’ang’ana kwenye kitu ambacho kimewafikisha kwenye mafanikio. Kila unapoangalia maisha yao unaona sio kwamba walianzia hapo walipo sasa, ila walianzia chini sana. Na hata walipoanzia chini sio kwamba safari yao ilikuwa mwororo sana, bali walikutana na changamoto nyingi sana ambazo ziliwarudisha nyuma. Lakini wao walikataa kitu kimoja, kukata tamaa.
Kama kila unapoanza kitu kipya, ukikutana na changamoto unafikiria kuachana nacho na kutafuta kingine, jua ya kwamba haupo kwenye kundi la wanaofanikiwa. Hii ni kwa sababu kwenye kila kitu ambacho utakwenda kufanya, utakutana na changamoto. Na kitakachokuletea mafanikio sio kutokukutana na changamoto, bali kukutana nazo na kuzivuka kwa kuwa king’ang’anizi.
Usikubali kabisa kuishia njiani kabla hujafikia kile ambacho ulikuwa unataka kukipata. Piga marufuku kukata tamaa. Na naweza kumalizia kwa kusema KOMAA NA LAZIMA UTAFANIKIWA.
7. Kushika hatamu ya maisha yao.
Nioneshe mtu aliyefanikiwa sana ambaye yeye huwa anamlaumu na kumlalamikia kila mtu. Nioneshe mtu huyo ambaye kila jambo linalotokea anatafuta wa kumnyooshea kidole. Na pale ambapo mambo hayaendi vizuri anatafuta ni nani kaharibu maisha yako. huwezi kuniletea mtu mwenye mafanikio makubwa mwenye sifa hizo, hii ni kwa sababu mtu mwenye hizo sifa hawezi kufikia mafanikio makubwa kamwe.
Hatua ya kwanza kabisa ya kufikia mafanikio makubwa ni kushika hatamu ya maisha yako. watu wote wenye mafanikio makubwa wanajua kwamba maisha yao ni jukumu lao binafsi. kama kuna kitu ambacho hawakipendi kwenye maisha yao basi wanaweza kukibadili, na kama hawawezi kukibadili basi wanaachana nacho na kuendelea na mambo mengine.
Anza leo kushika hatamu ya maisha yako kama ulikuwa bado hujafanya hivyo. Amua kutokumlaumu mtu wala kulalamika, amua kwamba chochote ambacho kinatokea kwenye maisha yako ni jukumu lako. Na kubali kwamba wewe ndio dereva mkuu wa maisha yako, chochote unachotaka una uwezo wa kukipata kama utajitoa vya kutosha.
Karibu Tushirikishane.
Katika tabia hizi saba ni zipi ambazo unazo?
Na je tabia hizo ulizonazo umeonaje mchango wake kwenye maisha yako?
Na kwa zile ambazo huna, umejipangaje ili kujijengea tabia hizi?
Tushirikishane kwa kuweka maoni hapo chini, kwa kufanya hivi kwa pamoja tutajifunza zaidi.
Karibuni sana.
Habari Amani, Asante pia kwa kuendelea kutuhamasisha siku hadi siku kwa makala zako nzuri. Sehemu kubwa ya tabia hizi tayari ninazo,na ukweli ni kwamba nilianza kujijengea nilipojiunga kuwa mwanachama wa kisima cha maarifa tangu mwaka 2014. Mwanzoni kabla ya kujiunga sikuwa hata na mmoja ya tabia hizi. Leo hii najiamini kwa kiasi kikubwa,na naamini katika kile ninachofa nya na sina hofu ya kushindwa kama ilivyokuwa mwanzo. TABIA MBILI AMBAZO SINA. 1)Unga’ng’anizi 2)Kufikiria zaidi suluhisho na sio tatiz Katika tabia hiyo ya Ung’ang’anizi nitatole a mfano moja: Katika malengo yangu ya kifedha, kila mwezi huwa nawek a lengo la kutengeneza faida kiasi fulani mfano:1,000,000. Nikitathimini katikati ya mwezi hakuna uwezekano wa kulifikia lengo na nakukubaliana na matokeo.
LikeLike
Habari Ngutiti,
Asante kw akutushirikisha maoni yako hapa.
Hongera sana kw akuweza kujijengea tabia tano kati ya hizi saba, ni hatua kubwa sana ambayo umeipiga kwenye maisha yako ambayo wengi hawataweza kuipiga kabisa kwenye maisha yao.
Kwa hizo mbili ambazo bado, endele akuzifanyia kazi na tuendelee kushirikiana ili uweze kufikia kile ambacho umepanga kufikia.
Karibu sana,
TUPO PAMOJA.
LikeLike
Naendelea kujifunza vitu vizuri kutoka kisima cha maarifa
Nitahakikisha najijengea tabia hizo zaba za mafanikio
LikeLike