Kama hukubaliani na kile ambacho unaambiwa au kushauriwa ufanye, basi tuambie au tuoneshe unafanya nini.

Tatizo la wengi wanaopinga au kukosoa ni kwamba wakishafanya hivyo wanarudi kuendelea na maisha yao yale yale, hawafanyi jitihada zozote za kubadili maisha yako.

Labda umesoma hapa kwamba unahitaji kuweka juhudi zaidi kwenye kazi yako, maana hiyo ndiyo itakayokutoa hapo ulipo sasa. Kwa sababu wewe ni mpingaji unasema hujui kazi yangu, hata niweke juhudi kiasi gani hakuna atakayejali. Halafu unaendelea kufanya kazi hiyo kwa njia ile ile. Hili ni jambo la kushangaza sana kwa sababu unakuwa umegoma wewe mwenyewe kuwa bora. Kama hukubaliani na wazo la kuweka juhudi zaidi, basi angalau fanya kitu kingine tofauti, labda acha kabisa kazi hiyo.

Ninachotaka kukuambia wewe rafiki yangu leo ni kwamba, kama kuna kitu ambacho hakipo sawa kwenye maisha yako, na ukapewa ushauri ambao wewe hukubaliani nao, angalau fanya kitu kingine mbadala. Usiendelee kufanya kile ambacho unafanya sasa kwa njia zile unazotumia kufanya sasa. Kama umeona ushauri unaopewa hauwezekani, angalau unajua ni kipi kinachowezekana, basi fanya hiko. Usiwe tu mtu wa kupinga na kukosoa wakati maisha yako yanaendelea kuwa magumu.

Kama hukubaliani na kile unachoambiwa, basi fanya mbadala wake. Lengo ni wewe ufanye kitu ili kuboresha maisha yako.

SOMA; Hivi Ndivyo Waajiriwa Wanavyopoteza Uhuru Wao Wenyewe, Na Jinsi Ya Kuudai Tena.

TAMKO LANGU;

Nimejikumbusha ya kwamba ni muhimu sana kuchukua hatua kama nataka maisha yangu yabadilike na kuwa bora. Na nimejua kama sikubaliani na kile ninachoambiwa, nitafute kitu mbadala ya kufanya. Nisiishie tu kupinga, bali niangalie ni nini naweza kufanya na kukifanya.

NENO LA LEO.

“If you do what you’ve always done, you’ll get what you’ve always gotten.” –Tony Robbins

Kama utafanya kile ambacho umekuwa unafanya kila siku, utapata matokeo yale ambayo umekuwa unapata kila siku.

Kubadili maisha yako unahitaji kuanza kufanya vitu vya tofauti. Anza sasa kufanya kwa utofauti.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.