Habari ya wakati huu Mpendwa Rafiki na Msomaji wa Amka Mtanzania? Karibu tena katika siku hii nyingine mpya ambayo ni fursa kubwa kwetu na ya kipekee kabisa ya kwenda kuboresha maisha yetu bila kusahau kukua katika mafiga matatu ambayo ni muhimu kwa kila mwanadamu. Kama tunavyojua huwezi kuweka sufuria au chungu jikoni ambapo kuna mafiga mawili au moja. Mafiga matatu yana ushirikiano wa hali ya juu sana kama figa moja halipo basi mafiga mengine hayawezi kufanya kazi. Huenda ukawa unajiuliza mafiga matatu hayo ni yapi? Basi, ndugu msomaji, ninaposema unatakiwa kukua katika mafiga matatu namaanisha kwamba kukua katika sehemu kuu tatu nazo ni; kukua kiroho, kimwili na kiakili.

Ndugu msomaji, katika harakati zako zote hakikisha unakua katika sehemu hizo kuu tatu. Unatakiwa uwe sawa usikue tu kimwili, bali kua kiroho na kimwili. Na uwe na ushirikiano katika maisha yako kama mafiga matatu. Karibu katika makala yetu ya leo ambapo leo tutajifunza kwa pamoja falsafa ya asili kabisa ambayo inagusa maisha ya watu wengine katika safari ya mafanikio. Huwezi kuikwepa falsafa hii katika maisha yako kama wewe uko hapa duniani. Je unajiua falsafa hii muhimu sana katika safari yako ya mafanikio ambayo unaitumia kila siku? Karibu twende sanjari mpaka mwisho wa safari hii.

SOMA; Mbinu Saba(7) Za Kuongeza Ushawishi Wako Kwa Wengine Na Kupata Chochote Unachotaka.

Kuna bahari inaitwa Bahari Mfu (Dead Sea) hii bahari iko pale mashariki na kati katika nchi ya Israel. Sifa kuu ya bahari hii ina mazoea ya kupokea maji tu pale mashariki na kati. Hii bahari yenyewe ni kupokea tu na haitoi hata tone ili kumegea wengine bali imeshikilia tu maji yote. Matokeo yake maji yananuka na hayafai kwa matumizi ya mwanadamu.

Kwa mfano huo, wa bahari mfu tunaweza kuuona katika maisha yetu ya kawaida. Watu wamekuwa kama bahari mfu wenyewe ni kupokea tu bila kutoa hata tone kwa wengine. 
Falsafa ninayoizungumzia hapa ni falsafa ya KUTOA NA KUPOKEA. Leo siyo mara yako ya kwanza kusikia hii dhana katika maisha yako kwamba unapopokea unatakiwa kutoa na unapotoa tarajia kupokea. Katika dunia ya leo kama unataka kufanikiwa unatakiwa usiwe kama bahari mfu. Ni wangapi wanapenda kupokea tu katika maisha yao bila kutoa? Umejaliwa kila kitu na Mungu je unatoa kuwasaidia wengine? Au umekuwa bahari mfu? Unapenda kupokea bure tu siku ukiambiwa kulipia gharama unakimbia hujui hata vya bure vina gharama?

Katika maisha ya mafanikio usitegemee kupokea kama hujatoa. Unapotoa ndio unapokea, je unayatumiaje maarifa uliyonayo kuwasaidia wengine nao waboreshe maisha yao? Kama una kitu katika akili yako na unaona kama kitakuwa ni msaada kwa wengine wasaidie na wengine ili nao wanufaike pia. Hujui jinsi unavyowasaidia wengine ndivyo na wewe unavyopokea kwa sababu unakuwa siyo bahari mfu tena bali una faida kwa wengine.

SOMA;  UCHAMBUZI WA KITABU; START WITH WHY, Jinsi Viongozi Wakubwa Wanavyohamasisha Watu Kuchukua Hatua.

Lazima utoe huduma ndio uweze kupokea malipo. Huwezi kupokea malipo bila kutoa huduma. Hivi karibuni bilionea Mohamed Dewji ambaye ndio bilionea kijana Afrika aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa instagramu hivi ‘’Mungu anapokubariki kwa utajiri usiboreshe kiwango cha maisha yako, boresha kiwango chako cha KUTOA’’ hakuna tajiri au mtu aliyefanikiwa aliwahi kufilisika kwa ajili ya kusaidia wengine. Hivyo basi, unapopata toa, na unapotoa ndio utapokea.

Unapopata mafanikio na wengine wanufaike pia na siyo kuwa kama bahari mfu unapokea tu hata hutoi kwa wengine. Tena katika utoaji unatakiwa kutoa kwa moyo na ukarimu. Kama una kipaji fulani katika maisha yako au taaluma fulani saidia kuwapa huduma watu kwa kile ambacho unacho. Ubinafsi na umimi hautakusaidia kitu. Huwezi kurefusha wasifu wako hapa duniani kwa kuangalia tu familia yako. Pale wasifu wako unaposomwa wakati upo kwenye jeneza tayari kwenda kuzikwa usiwe hivi, marehemu aliacha mke na watoto watano, kumi, magari ya kifahari kumi na nyumba ya kifahari tayari wasifu umeisha. Sasa huu ni wasifu wa umimi au ubinafsi ambao unaonesha kujitoa kwa familia yako zaidi kuliko kwa watu wengine. Bora hata yule aliyekuwa na kibanda cha chipsi na kuajiri hata watu wawili atakua amegusa maisha ya watu wengine na atakumbukwa na watu kulingana na huduma yake ya chipsi aliyokuwa anatoa na kuajiri watu.

Usikalie maarifa ambayo unayo, ulienda shule kuyapata bali yatoe duniani ili yatengeneze dunia. Usiwe astashahada, stashahada, shahada, uzamili na uzamivu jina tu bali kuwa na vitendo kulingana na elimu yako uliyoipata. Wasaidie wengine waonje matunda yako uliyoyapata shule siyo kuwa msomi cheti wa maneno bila vitendo.

Kabla hujalalamika na kusema serikali haijanifanyia kitu fulani jiulize je na wewe umeifanyia nini serikali yako?, mwajiri wako hajakufanyia kitu fulani je na wewe umeongeza thamani gani kwa mwajiri wako?, wateja wako wamepungua katika biashara yako na n.k jiule je na wewe umewafanyia nini wateja wako? Kwenye kila kitu usitegemee kupokea kama na wewe hujatoa chochote. Hata ng’ombe hawezi kukupa maziwa kama na wewe hujamhudumia chakula chake ili akuzalishie maziwa. Ukiyahudumia mazingira vizuri nayo yatakuhudumia vizuri.

SOMA; Kama Una Wasiwasi Sana Katika Maisha Yako, Hakikisha Unasoma Hapa.

Kwa hiyo, ndugu msomaji, tunatakiwa kuishi katika falsafa hii unapopokea unatakiwa kutoa. Ukipokea bila kutoa unakuwa una deni hivyo unatakiwa kulilipa kabla hujaondoka hapa duniani. Tafadhali usiwe kama bahari mfu katika maisha yako kwani utakuwa unanuka mbele za watu maisha yako yamekuwa hayana msaada kwa wengine kama vile bahari mfu. Kama umepokea toa kwa moyo na ukarimu. Mali isikufanye udhulumu, udharau, utumikishe na kudhalilisha utu wa watu wengine. Na usiendelee kuishi kwa mazoea kwani mazoea yataendelea kuacha watu wakose Baraka za Mungu kwa miaka mingi. Hivyo amka na badilika.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com