Habari mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? 

Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri kuishi maisha yeye maana hapa duniani. Maisha ya ubinafsi siyo maisha mazuri kuishi hapa duniani yaani unajifikiria wewe mwenyewe na siyo watu wengine. Leo ni siku ya kipekee sana kwetu tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai hivyo basi, tuitumie vizuri siku hii ya leo kwa kuzalisha mambo chanya na yenye tija kwenye maisha yetu.

Mpendwa msomaji, napenda kukualika tena katika makala yetu ya leo tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Leo tutakwenda kujifunza maneno mawili yasiyokuwa na msaada kwenye maisha yako. Je ungependa kuyafahamu ni maneno gani hayo? Basi karibu rafiki tuweze kujifunza wote kwa pamoja hivyo nakusihi sana uweze kusafiri na mimi mpaka mwisho wa makala hii na karibu tena tujifunze rafiki.

Inawezekana hapo ulipo umeshajilaumu sana kwenye maisha yako na kutumia haya maneno mawili hata kujilaani wewe mwenyewe na kujiona wewe siyo kitu kabisa hapa duniani. Wakati mwingine unaweza kujiona wewe ni mjinga wenzako wanaishi na wewe unachekesha tu hapa duniani kulingana na jinsi mambo yanavyokuendea.

Rafiki, maneno mawili ambayo hayawezi kuwa msaada kwenye maisha yako au yasiyoweza kubadilisha maisha yako kabisa ni LAITI NINGELIJUA. Laiti ningelijua yamekuwa ni maneno mawili yanayotumiwa na watu wengi sana katika maisha yao pale anapokuwa mambo yameenda tofauti na vile alivyotarajia.

Mpedwa msomaji, inawezekana mwingine anajilaumu na kujilaani laiti ningelijua bora ningeanza maisha yangu mapema kuliko kuendelea kula ujana ningeweza kuukomboa wakati hapa duniani na muda umeshaenda tena huwezi kupambana nao. Mwingine anajilaumu na kujilaani laiti ningelijua nisingelitegemea serikali na kuweka tumaini langu lote la maisha juu ya mikono ya serikali.

Aidha, utaendelea kujilaani na kujilaumu kwa kutumia maneno haya mawili laiti ningelijua na mwisho wake unakata tamaa kabisa ya maisha. Laiti ningelijua maana yake ni kwamba ulikuwa na tumaini la kitu Fulani halafu mambo yanakuja kwenda tofauti na ulivyotegemea. Ukichunguza kila idara ya maisha ya mtu lazima maneno haya mawili yamemgusa kwenye maisha yake.

Mpendwa msomaji, laiti ningelijua haiwezi kubadilisha maisha yako hata siku moja kwani huo ni wakati uliopita tena hauna nafasi tena kwenye maisha yako kwani wakati wenye nafasi katika maisha yako ni wakati wa sasa. Huwezi kubadilisha wakati wa jana kwani ulishapita bali unaweza kufanya kitu chochote sasa kwani ndio wakati wenye uhakika na wewe na wala siyo kesho wala baadaye.

Utaweza kujilaumu sana na kulalamika sana laiti ningelijua nisingefanya kitu Fulani, laiti ningelijua nisingelisoma masomo Fulani na mengine mengi yanayofanana na hayo. Kwanza kabisa laiti ningelijua ni dalili au ishara ya wazi kabisa inayodhihirisha kuwa mtu huyo anayesema hivyo ana dalili za ulalamikaji, kujilaani na kulaumu. Kwa mfano, Yuda Iskariyoti aliyekuwa mwanafunzi wa Yesu aliweza kujilaumu na kujilaani yeye mwenyewe kwani alimsaliti Yesu na kushindwa hata kujisamehe yeye mwenyewe na hatimaye kupelekea kujinyonga.

Mpendwa msomaji, kuna kina Yuda wangapi katika maisha yetu wanafanya makosa hatimaye wanakuja kujilaumu, kulalamika, kujilaani na kushindwa hata kujisamehe yeye mwenyewe? 

Kama mtu anafanya makosa katika maisha yake kwa sababu ya laiti ningelijua halafu anashindwa kujisamehe hata yeye mwenyewe na kujipelekea hata kujinyonga na kuona hata hakuna maana hata ya kuishi hapa duniani je mtu huyo anaweza kumsamehe hata mwenzake aliyemkosea?

Mpendwa rafiki, katika maisha yako siku zote mambo hayawezi kwenda kama ulivyotarajia. 

Huwezi kuilazimisha dunia iende kama vile unavyotaka wewe iende. Hupaswi kujilaumu, kujilaani na kushindwa hata kujisamehe wenyewe kama tulivyoona mfano kupitia Yuda. Unapaswa kujiandaa tayari kisaikolojia kupata matokeo tofauti na vile unavyotarajia wewe.

Pia, unapaswa kuwa na mpango wa ziada katika maisha yako yaani Plan B. Kuna wengine tumaini lao lilikuwa ni kusoma na kumaliza hatimaye kupata ajira ndani ya serikali au nje ya serikali lakini kwa sasa mambo yamebadilika. Kama ungekuwa umejiandaa kwa mpango wa pili huwezi kuja kujilaumu kwa kusema laiti ningelijua. Hata ukisema laiti ningelijua haiwezi kubadilisha maisha yako.

Hatua ya kuchukua leo, katika maisha yako chochote unachofanya jiandae kupata matokeo tofauti na unavyotarajia. Pili, ukiwa unaweka mipango yako hakikisha basi unakuwa na mpango wa ziada wa kuwa na plan B. na kama mambo yamekwenda ndivyo sivyo usilalamike chukua hatua bali chukua hatua chanya. Wengine wako mitaani wamekaa na kujilaumu bora hata wasingesoma kwa sababu wamesoma na kukosa ajira lakini kama ungejiandaa na bila kutegemea upande mmoja kwa sasa usingejilaumu.

Wewe bado ni bora kuliko mtu mwingine hapa duniani. Una kitu au hazina ndani yako ambacho bado hujaigundua. Una nafasi ya kuibadilisha duniani kama ukifikiria vya kutosha kwa kile ambacho unacho sasa.

Kwa kuhitimisha mpendwa msomaji, somo letu la leo limetualika kuwa katika maisha yetu maneno mawili laiti ningelijua hayawezi kabisa kubadilisha maisha yetu. Inatupasa kusahau yaliyopita na kuanza upya kabisa kwani katika maisha hakuna kufeli bali kuna kujifunza kutokana na makosa ya kila siku. Hupaswi kukata tamaa bali unapaswa kunyanyuka hapo ulipo uende ukaijaze dunia kwani bado ina njaa kubwa na mtu wa kuijaza ni mimi na wewe.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com