Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri katika maisha yako. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani leo ni siku nyingine mpya na bora kwetu kwenda kutimiza malengo tuliyojiwekea.

 

Ndugu msomaji, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena katika kipindi chetu cha leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja kile nilichokuandalia siku hii ya leo. Karibu tusafiri pamoja hadi pale tamati ya kipindi chetu cha leo ambapo leo nitakwenda kukushirikisha kauli maarufu inayotumiwa na watu wengi katika malezi ya watoto.

Watoto huwa ni zawadi kutoka kwa Mungu na tunaalikwa tuwapokee watoto kama walivyo bila kujali udhaifu wao. Tunapaswa kutambua kuwa watoto siku zote hawawezi kufanana hata siku moja na changamoto kubwa kwa wazazi wengi wa leo iko katika malezi ndiyo maana waswahili wanasema kuwa kuzaa siyo kazi ni kulea mwana.

SOMA; Huyu Ndiye Adui Namba Moja Kwenye Malezi Ya Watoto.

Rafiki, malezi ya watoto siyo kitu rahisi kama vitu vingine pale unapopata mtoto hakuna mwongozo unaopewa uufute katika malezi ya mtoto. Ndiyo maana malezi yanakuwa shida kila mtu anamlea mtoto kwa jinsi anavyojua yeye kama ni kwa kufuata misingi ya kimazoea au la hilo linakuwa chini ya wazazi wenyewe.

Ni ngumu sana mtoto kuwa wa tofauti katika jamii kama wazazi siyo wa tofauti, hii ni kwa sababu mtoto huwa anapenda sana kuiga kutoka kwa watu wake wa karibu kama vile wazazi. 

Mtoto asipofundishwa na wazazi kuwa hili ni jambo jema na hili ni baya hawezi kujua hivyo kama mzazi anachukua nafasi ya kuwa mwalimu wa kwanza katika malezi ya mtoto.

Mpendwa msomaji, wapo wazazi wengine wanategemea watoto wao wakuwe katika njia sahihi bila yao wao kua katika njia sahihi. Hii inakuwa ni changamoto kubwa sana katika malezi pale wazazi wanapotaka watoto wao wapitie katika njia Fulani halafu wao hawataki kubadilika. 

Mtoto hawezi kubadilika kama mzazi hawezi kubadilika vivyo hivyo hata katika kukua. 

Unatakiwa kama mzazi kuishi katika yale unayowafundisha watoto wako kama ukisema kitu fulani basi wewe ndiyo inabidi uwe mfano kwa watoto wako juu ya kitu hicho.

Huwezi kumhubiria mtoto jambo ambalo wewe unalifanya halafu wao wasifanye, unatakiwa kuwa mtu sahihi kwanza wewe mwenyewe na watoto watakufuata. Kuna kauli maarufu inayotumiwa na watu wengi katika malezi ya watoto nayo ni watoto wa siku hizi bwana, watoto wanafanya mambo ndivyo sivyo lakini wazazi wanafurahia kwa kauli ya watoto wa siku hizi bwana bila kuwachukulia hatua stahiki. Sasa kama wazazi wanawashangaa watoto wa siku kwa maadili yao je watoto wa siku wanazaliwa na wazazi wa kipindi gani? Jawabu ni kwamba watoto wa siku hizi wanazaliwa na wazazi wa siku hizi. Kama tunawashangaa watoto wa siku hizi basi wazazi wanapaswa kujishangaa wao kwanza kwani wao ndiyo chanzo cha yote haya.

SOMA; Mambo Matano(5) Muhimu Ya Kuzingatia Kwenye Malezi Ya Watoto Ili Kuwaandaa Kufikia Mafanikio.

Mpendwa msomaji, kama wazazi wanapaswa kuliangalia swala la maadili kwa watoto kwa jicho la tatu, chanzo cha watoto kubadilika mhusika mkuu ni mzazi wewe ndiyo unapaswa kuwajibika na wala huna wa kumlaumu. Kwa mfano, unakuta mzazi analalamika mtoto wake anashindwa kujisomea kwa masomo yake ya ziada akiwa nyumbani kwa sababu ya kuangalia tv na kucheza gemu. Vitu kama tv na nk nyumbani viko ndani ya uwezo wa mzazi anaweza kuvidhibiti hata kuifungia chumbani kupiga marufuku lakini wazazi wengine wanalalamika eti watoto wa siku hizi bwana hawapendi kusoma wakati chanzo ni wewe mwenyewe mzazi.

Hatua ya kuchukua leo, kumbuka hakuna mtoto wa siku hizi bila mzazi wa siku hizi, watoto wa siku hizi wanazaliwa na wazazi wa siku hizi hivyo wazazi wanapaswa kuwajibika ipasavyo katika malezi ya watoto. Tenga muda wa kuwasiliana na watoto wako na kujua maendeleo yao kuwapa mahitaji yao tu pekee yake haitoshi bali unabidi uwajibike kama mzazi kuchukua nafasi yako na siyo kukwepa majukumu.

Kwa kuhitimisha, ili tuweze kupata watoto bora katika jamii tunaalikwa kuwa na watoto bora katika familia. Familia ndiyo msingi wa mambo yote hivyo wazazi wanawajibika kuwapa watoto malezi bora na kuwafundisha maadili na jinsi ya kukabiliana na changamoto za ulimwengu huu wa zama za taarifa.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kujifunza kila siku. Asante sana.