Kitu pekee ninachojivunia kwa sasa ni afya njema niliyonayo ambayo ndiyo utajiri namba moja duniani, Naamini na wewe pia utaungana na mimi katika kuwafariji watanzania wengine ambao wanapitia changamoto mbalimbali ikiwemo ya afya, na kwa kuwa maendeleo ni watu na ukweli utabaki kuwa mtu ni afya. Makala hii ni maalumu kwa wale ambao daima huwaza mafanikio katika uwekezaji wa ardhi na majengo. Hapa ni uwanja wetu ambao tunaelimishana na kupeana uzoefu na ujuzi mbalimbali ili kila mmoja wetu aweze kufika pale anapotarajia kufika. Kwa sasa hali ya sera za nchi zinabadilika kwa kasi sana kuendana na kauli mbiu ya utawala wa sasa. Sera ya Tanzania ya viwanda na kuhamia makao makuu kwenye mji wa Dodoma ni sera ya kimaendeleo hasa katika mji wa Dodoma na mapinduzi ya viwanda nchini. Zaidi ya yote maendeleo ya matumizi ya ardhi na majengo yamekuwa ni kichocheo na alama ya maendeleo katika nchi na jamii kwa ujumla. Leo tuangalie fursa zinazoweza kujitokeza pamoja na changamoto zake ili kwa umoja wetu tuweze kutembea salama na kwa uhakika kuendana na mabadiliko yanayoendelea kujitokeza.

 

  1. MAHITAJI YA MAKAZI


Wananchi wengi wana mipango ya kujenga nyumba za kisasa kwa gharama nafuu na katika hali ya usalama na kujiamini zaidi. Nyumba ni moja kati ya mahitaji ya lazima ya mwanadamu ili aweze kuishi na kufanya shughuli zake za kimaendeleo katika hali ya usalama. Zaidi ya hapo nyumba zimekuwa ni mali katika mfumo wa maendeleo ya jamii na uchumi. Wakati ujao Dodoma itakuwa inapokea ongezeko la watu kadri muda utakavyoenenda. Katika hali na umuhimu wa makazi kila mwananchi anapaswa atimize hitaji la kuwa na makazi katika hali yeyote aliyokuwa nayo. Lengo langu katika safu hii ni kuona kila Mtanzania azione na azitambue fursa zitakazojitokeza, naamini kuwa uwezo tunao na sababu nyingi tunazo za kufanya yale ambayo yataleta tija na manufaa kwetu binafsi na kwa jamii zinazotuzunguka. Kutokana na huduma nyingi za serikali kuelekea Dodoma kutachochea ongezeko kubwa la mahitaji ya makazi. Makazi hayana mbadala, na sio wananchi wote watamudu mwendo kasi wa mabadiliko yanayoendelea kufanyika kwa sasa hivyo kulazimika miongoni kutafuta makazi ya muda.

SOMA; Huu Ndiyo Uwekezaji Bora Kabisa Unaokufanya Wewe Kuwa Tajiri Kwenye Maisha Yako.

  1. MAHITAJI YA BIASHARA NA UZALISHAJI MALI


Maendeleo hayana ukomo, lakini maendeleo yanahitaji miundo mbinu ya majengo tofauti kukidhi mahitaji husika. Kampuni, taasisi, watu binafsi na mashirika mbalimbali yanahitaji majengo ili kukidhi uzalishaji mali na utoaji huduma kwa jamii. Katika hili uwekezaji wa majengo hauepukiki, lakini kwa sasa tunahitaji kufanya mambo kwa namna ya tofauti sana, tujenge kwa weledi na tuache kufikiri kwa mazoea. Kwa sasa tunahitaji kuzingatia ufanisi na ubora katika kukidhi mabadiliko ya sayansi ya usanifu majengo na uhandisi majenzi unaoendelea kujitokeza kwa sasa. Zitazame fursa kwa namna tofauti na hakika utafanya kitu cha ziada. Mahitaji ya majengo ni jambo la lazima na hakika itamletea manufaa kwa atakayefanikiwa kuwekeza, tusisubiri wageni waje tuanze kulalamika, tuanze sisi na kuwakaribisha wao.

  1. MAHITAJI YA HUDUMA ZA JAMII

Mahitaji ya huduma za jamii ni muhimu sana kwa maendeleo ya jamii yoyote ile duniani. 

Katika hali yoyote mazingira yanayopokea ongezeko la watu lazima yawe tayari kukidhi ongezeko la huduma za jamii. Naamini watanzania wengi watajitokeza na kuzitumia vema fursa hizi za uwekezaji kwenye huduma za kijamii. Haya ni maeneo yenye mjumuiko wa watu wengi kwa wakati mmoja, ni vema yakapewa vipaumbele ikiwemo miundombinu yake. Nazungumzia majengo ya afya, elimu, michezo, kumbi za starehe na burudani. 

Changamoto kubwa ipo kwenye miji na majiji yetu yanayokuwa kwa kasi tofauti na uendelezaji wa miundombinu ya maendeleo ya jamii. Mifumo ya usalama, mawasiliano na sauti ni vema yakazingatiwa kwa sasa. Karne ya sasa tunahitaji kufanya mambo kwa njia tofauti sana. Tunahitaji kuifikiria Tanzania ya kesho, Tanzania ya leo ilijengwa jana na wazee wetu nasi tuna wajibu wa kuendeleza pale walipoishia na kuitunza kama lulu.

 SOMA; Guide To Investing(Muongozo Wa Uwekezaji).

  1.  UTAYARI WA MIUNDOMBINU


Miundombinu ya nchi ni mtambuka katika maendeleo ya uchumi na jamii yoyote duniani. 

Hapa nazungumzia njia kuu za mawasiliano, usafirishaji, nishati ya umeme, maji safi na maji taka. kwa sasa miundombinu iliyopo bado haikidhi mahitaji ya sasa kama inavyopaswa katika kumfikia na kutumika na kila mmoja pasipo shida ya aina yoyote. Miundombinu ya uhakika ni kichocheo kikubwa kwa maendeleo ya nchi, ingawa jitihada mbalimbali bado zinaendelea kufanyika katika kuboresha hali iliyopo ili kufikia viwango fulani ndani ya muda mfupi ujao. Hiyo ni njia pekee ya kuvutia uwekezaji wa aina yoyote kwa kuwa miundombinu hupunguza gharama za uwekezaji kwa kiasi kikubwa sana. Ni Imani yangu kubwa kuwa endapo tutafanikiwa kuimarisha na kuboresha miundombinu ya nchi, Tanzania itakuwa tofauti sana kwa muda mfupi ujao tofauti na wakati mwingine wowote. Namalizia kwa kusema kuwa maendeleo na ubora wa miundombinu ndiyo itakayoleta matokeo hasi au chanya katika mapinduzi ya kimaendeleo na uwekezaji nchini. Pia nimepata maswali mengi kuhusu utayari na ufanisi wa masta plani ya mji wa Dodoma ili kila mtu aweze kufanya upembuzi yakinifu ili aweze kutambua afanye nini na wapi ili kukidhi mahitaji ya kijamii, mazingira na uchumi pasipo na shaka ya aina yoyote. Naamini wahusika watakuwa wanalifanyia kazi jambo hili na tutapata msaada kadri itakavyowezekana. Hatutaki kuona vilio tena sababu zikiwa ni zilezile tu, ikiwemo upanuzi wa barabara ikiwa leo tuna uwezo wa kuwa na masta plani itakayokidhi mahitaji ya miaka mingi ijayo.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com