Mpendwa msomaji, nipende kutumia nafasi hii kukualika tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale muhimu niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo.
Hivyo nakusihi sana tuweze kusafiri pamoja kimawazo hadi pale tamati ya kipindi chetu cha leo. Kupitia makala yetu ya leo ninakwenda kukushirikisha falsafa muhimu ya kuwafikiria na kuwajali wengine hapa duniani.
Dunia ya leo imetawaliwa na ubinafsi na madhara ya ubinafsi ni makubwa ukilinganisha na faida zake. Ubinafsi ni hasara kwa sababu ubinafsi huwa ni falsafa ya kujifikiria wewe mwenyewe bila kujali wengine au kuwafikiria wengine. kila mtu yuko hapa dunia kwa ajili ya faida kwa mwingine lakini cha ajabu watu wanabakia kubaki na ule umimi wa kutotaka wengine wasipate na kuona kwamba wao ndiyo wanastahili zaidi kupata kuliko wengine.
Mpendwa msomaji, nilipokuwa nasoma elimu ya kidato cha tano na cha sita nilikuwa kiongozi mkuu wa serikali ya wanafunzi yaani head prefect, sasa pale shule tulikuwa tunaishi kwa kuongozwa na falsafa moja ambayo ilikuwa inasimamia haki na kuwajali wengine. Na hii ilitokana na baadhi ya wanafunzi wasiojali wengine na kujiangalia tu wao walikuwa wanaweza kuwahi eneo la chakula na kuchukua chakula kingi hadi kupelekea wengine wanakosa chakula. Kwa hiyo, baada ya kuona watu wengi wanamiss yaani kukosa tukaamua kuanzisha kauli mbiu iitwayo mind a gap.
SOMA; Hii Ndiyo Kansa Kubwa Inayosambaa Kwenye Jamii Zetu Na Jinsi Ya Kuiepuka.
Katika kauli hii ilikuwa na misingi kuwa popote unapokuwa iwe ni kwenye chakula au mazingira ya shule yaliyokuwa yanahitaji kuwafikiria wengine. kwa mfano, wewe ukiwa unaenda kupakua chakula kumbuka kuwafikiria wengine bado au kuwajali wengine. Hivyo, usije kufanya jambo kwa kujiangalia tu wewe na kusababisha wengine wanaumia, hata katika mazingira yetu ya kawaida iwe ni nyumbani au sehemu yoyote kumbuka kumfikiria na mtu mwingine bado siyo kujiangalia tu wewe mwenyewe.
Tunatakiwa kuwajali wengine na kuwafikria pia na siyo kujiangalia sisi kama sisi. Kwa mfano, unaweza kwenda sehemu labda benki unakuta wenzako wamepanga foleni badala ya wewe kufuata utaratibu unataka uchepuke na kwenda mbele uanze kuhudumiwa wewe na kuona kama wengine hawana maana vile waliokaa katika foleni wakisubiria huduma. Kila mtu ana haraka na anapenda kuwahi sehemu kwa wakati husika kwa hiyo ni vizuri kuwaangalia wengine na siyo kujiangalia wewe tu yaani unatakiwa ‘’kumind e gep’’.
Rafiki, unapokwenda sehemu kuonana na mtu fulani kwa ajili ya kupata huduma fulani kumbuka kuwafikiria na wengine pia siyo ukienda unatumia muda mrefu kuongea na huku ukitambua kuwa kuna watu wengine nyuma wanahitaji kuhudumiwa au kusikilizwa kama wewe. Kila mtu anahitaji kusikilizwa na kuhudumiwa hivyo usipende kutumia muda mrefu kwa kurefusha maongezi badala yake nenda moja kwa moja kwenye lengo au kwenye pointi ili kuokoa muda na kuachia nafasi watu wengine waweze kuhudumiwa.
SOMA; JAMII INAYOKUZUNGUKA NI MUHIMU SANA KWAKO, USIIACHE NYUMA.
Muda mwingine unaweza kugeuka kero kwa watu wengine na hata kupelekea kuwakwaza watu kwa sababu tu ya kushindwa kuishi misingi au falsafa ya kuwafikiria wengine pia wanahitaji kuhudumiwa au kusikilizwa kama wewe. Unapofanya jambo lolote kumbuka kuwafikiria wengine nao wanahitaji kufanikiwa katika jambo fulani kama wewe unavyopenda kufanikiwa. Kama wewe leo kuna kitu kimekusaidia katika maisha yako unaweza pia ukawasaidia wengine kwa kuwashirikisha namna kitu hicho kilivyokusaidia na hatimaye unakuwa msaada kwa wengine.
Hatuwezi kuijaza dunia na kuifanya kuwa sehemu salama kwa kila mmoja wetu kama kila mtu akijiangalia na kujifikiria mwenyewe tu. Leo hii tunanufaika na matunda ya watu wengine wanaoamua kujitoa kwa ajili ya watu wengine na huenda vitu vyao viko vinakusaidia kila siku katika maisha yako. Pengine waliogundua vitu hivi wameweza kuwa msaada kwetu leo na hawapo hata duniani lakini waliamua kuwafikiria na wengine, basi nasi tunaalikwa kuweza kuwafikiria wengine na tuwawezeshe ili waweze kufanikiwa.
Hatua ya kuchukua leo, ubinafsi ni hasara katika maisha ya mwanadamu. Hivyo unaalikwa kuacha tabia ya ubinafsi na kuanza leo kuwafikiria wengine na kuwajali kama vile unavyopenda kujijali wewe mwenyewe. Tupo duniani kwa ajili ya kusaidiana hakikisha kila siku unamsaidia mtu kubadilisha sehemu yoyote ya maisha yake, mguse kwa aina yoyote ili mradi tu usimwache kama alivyo.
Kwahiyo, ili tuweze kufanikiwa na kuiendelezea hii dunia tunatakiwa kwanza tuache kujifikiria sisi mwenyewe na badala yake tuanze kuwafikiria wengine zaidi. Tufikirie kutatua matatizo ya watu wengine ili kuweza kuifanya dunia kuwa sehemu bora ya kuishi kwa kila mmoja wetu.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kujifunza kila siku. Asante sana.