Katika maisha zipo nyakati, ambazo naweza sema ni nyakati ngumu sana na zina misukosuko mingi, kiasi cha kwamba usipokuwa makini unaweza ukaachana na kila kitu kutokana na nyakati hizi kuwepo kwako.

Nyakati hizi ngumu katika maisha ya mwanadamu huwa zinatokea sana na inawezekana pia hata hivi sasa unapitia nyakati hizo na umekuwa ukijikuta huelewi ni nini cha kufanya hasa unapokutana na hali kama hii.
Kikawaida, nyakati hizi ngumu katika maisha huwa haziletwi na kitu kingine chochote zaidi ya changamoto za kimaisha. Changamoto za kimaisha, hasa ndizo ambazo hupelekea maisha kuanza kuonekana kuwa magumu na hata mtu kukosa tumaini.
Kuna wakati inafika hadi unaweza ukajiuliza umekosa ni nini kwenye hii dunia hadi ukakutana na changamoto nzito kama hizo, hapo hujikuta unaweza ukaumia au ukilia sana, lakini yote hiyo inakuwa bado haisaidii kitu.
Pambana kwa kila hali, mpaka utoke kwenye chanagamoto za kimaisha.
Ninasema inakuwa haisaidii kwa sababu, unakuwa bado upo pale pale kwenye changamoto zako, na dawa pekee ambayo unatakiwa kuwa nayo ni kutoka kwenye changamoto hiyo kwa namna yoyote ile.
Haijalishi unapita kwenye kipindi gani, lakini lilokubwa kwako ambalo kila wakati unapaswa kulielewa na kuliangalia zaidi ni kwa jinsi gani wewe utaweza kumudu hali hiyo ya kutokata tamaa na kuendelea na maisha yako unapokuwa kwenye kipindi hichi.
Ni lengo la makala haya, kukupa mwanga na kukuonyesha njia ya kupita, ili ikusaidie kutokukata tamaa, wakati unakutana na changamoto kubwa za kimaisha.  Hapa inabidi uwe shujaa upigane mwanzo mwisho.
Unawezaje  kutokukata tamaa katika kipindi kigumu unachopitia nyakati mgumu za maisha? Yafuatayo ni mambo ya msingi kuzingatia ili usikate tamaa katika kipindi ambacho unakutana na changamoto ngumu katika maisha yako.
1. Kipindi cha nyakati ngumu, siyo chako peke yako.
Nyakati ngumu unazopitia au changamoto unazopitia, kitu cha kwaza ambacho unatakiwa uelewe, wewe sio mtu wa kwanza kukutana nazo, bali wapo watu ambao wameshakutana nazo sana na wakaishinda pia.
Kama hiyo ilitokea kwao hivyo, basi hata wewe unayo nafasi ya kuishinda changamoto hiyo na kuwa mshindi kwenye maisha yako. Huna haja ya kujuta au kuendelea kulia sana, jipe moyo na utashinda majaribu hayo.
2. Nyakati ngumu katika maisha, zinakujengea ukomavu.
Maisha yanajengwa kwa namna tofauti. Kipo kipindi yanaweza kujengwa katika njia ya kawaida na kuna wakati yanajengwa kwenye njia ngumu na hatari kama hiyo ya changamoto na nyakati ngumu.
Ukilijua hilo, basi elewa unakomazwa na maisha. Siku ukija kutoka hapo utakuwa kama dhahabu ambayo tayari imeshapitia kwenye moto. Utakuwa umekamilika kila eneo na hakuna kitakachokubabaisha.
3. Nyakati ngumu katika maisha, zinakusaidia kukujengea hali ya uvumilivu mkubwa sana.
Sio siri tena, unapopitia katika nyakati ngumu katika maisha yako, ni kipindi ambacho unapitia kwenye uvumilivu mkubwa sana. ukilielewa hili, itakusaidia sana kupita kwenye nyakati zozote ngumu zinazojitokeza kwenye maisha yako hata kwa baadae.
Kwa kuzingatia mambo hayo, bila shaka utakuwa umepata mwanga ni kwa jinsi gani unaweza ukapita kati kati ya nyakati ngumu zinazoweza kujitokeza katika maisha yako wakati wowote na ukawa mshindi mkubwa.
Chukua hatua katika kufikia mafanikio makubwa na pia endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kwa kuweza kujifunza kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Blog, dirayamafanikio.blogspot.com
Mawasiliano; +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com