Kwenye jamii zetu, imezoeleka kwamba kiongozi ni mtu ambaye anafanya maamuzi makubwa, maamuzi magumu na hatari sana. Kwa kufanya maamuzi hayo na matokeo yakawa mazuri, kiongozi hupata sifa kutoka kwa kila mtu. Pitia mifano ya viongozi wote, J. K Nyerere, Mandela, Gandhi, Mama Teresa na wengine wengi, ni watu ambao walifanya makubwa sana katika nafasi zao.



Lakini dhana hii juu ya viongozi ina makosa au mapungufu mawili makubwa;

Moja inawafanya wengi waamini kwamba kama hawawezi kufanya makubwa kama watu hao, basi wao siyo viongozi. Huwafanya watu wanaokazana kwenye maisha yao ya kila siku, kuhakikisha kazi zao na maisha yao yanakwenda vizuri wajione hawana mchango mkubwa kwenye mafanikio ya familia, taasisi, jamii, nchi na hata dunia kwa ujumla.

Mbili dhana hii inafanya watu waamini viongozi hao waliofanya hayo makubwa wao peke yao. Huonekana kama wao ndiyo walikuwa kila kitu, ni kweli wanakuwa wameweka mchango mkubwa, lakini kazi kubwa sana ilifanywa na wale waliokuwa chini yao. Wale ambao walikuwa wakifanya makubwa, lakini hawakuonekana, wala hawakuandikwa popote.

Mwandishi Joseph Badaracco, anatufafanulia aina muhimu sana ya uongozi ambayo ni KUONGOZA KIMYAKIMYA kama alivyokiita kitabu chake, LEADING QUIETLY. 

Katika aina hii ya uongozi, Joseph anatuonesha namna gani kila mmoja wetu ni kiongozi, na jinsi gani ya kuimarisha na kuboresha uongozi uliopo ndani yetu.

Kuna misingi ya kuongoza kimyakimya, kuna changamoto za kuongoza kimyakimya, yote haya anatufundisha kwa undani, ili tuweze kufanya maamuzi bora kwenye maisha yetu ya kila siku.

Karibu tujifunze kwa pamoja kupitia uchambuzi huu wa kitabu cha LEADING QUIETLY.

1. Kila fani ina mashujaa wake, watu ambao ni wanaheshimika kwa kazi kubwa walizofanya. Watu hawa huchukuliwa ni viongozi bora zaidi. Lakini ukweli ni kwamba, wapo viongozi ambao walikuwa bora sana lakini hatujawahi kusikia chochote kuhusu wao. Hii ina maana hata wewe unaweza kuwa kiongozi bora sana, hata kama hakuna atakayesikia kuhusu wewe.

2. Watu kwenye dunia ni kama wamegawanyika makundi mawili, kundi la kwanza ni wale wanaoitafuna dunia, hawa ni wale ambao wanatumia rasilimali za dunia kupita kiasi na kutengeneza vita. Na kundi la pili ni wale wanaoiokoa dunia, wale ambao wanatunza rasilimali za dunia, wanatengeneza amani. Viongozi wengi mashuhuri tunaowajua ni kwa sababu wapo kwenye kundi moja kati ya hilo, kwa mfano Adolf Hitler anakumbukwa kwa kutaka kuiangamiza dunia, na Mandela kwa kuwakomboa watu na ukandamizi. Lakini kwenye maisha yetu ya kila siku, watu hawapo kwenye makundi hayo mawili, bali wanakazana kuishi maisha yao, kufanya kazi zao na kuwa wema kwa wale wanaowazunguka, na huu ndiyo uongozi unaoleta mchango mkubwa kwenye dunia, japo hauongelewi sana.

3. Maisha yetu ya kila siku, changamoto tunazokutana nazo kwenye maisha, kazi na hata biashara, zinahitaji uongozi uliopo ndani yetu ili kuweza kutatua na kukabiliana nazo. 

Changamoto hizi huwa zinakuwa ndogo ndogo lakini kuzitatua kunahitaji umakini wa mtu anayekutana nazo. Hapa ndipo uongozi wa kimya kimya unapofanya kazi.

4. Changamoto tunazokutana nazo kila siku huwa zinakuwa ngumu zaidi pale ambapo tunakuwa hatuna uelewa wa kutosha kuhusiana na changamoto hiyo, au tunapojikuta inatubidi kupindisha sheria, au pale mtu aliyepo juu yako, anapokulazimisha ufanye kitu ambacho siyo sahihi kufanya. Hapo ndipo unahitaji kuwa na maarifa sahihi ya hatua gani uchukue.

5. Matatizo mengi huwa hayaji wazi, yakiwa na hatua tano za kuyatatua, au jambo moja la kufanya na mila kitu kikakaa sawa. Yanakuwa yana mchanganyiko na mahusiano na maeneo mengine ya maisha, kitu ambacho kinahitaji umakini mkubwa katika kuyashughulikia. Katika wakati kama huo, hakuna jambo la kishujaa unaloweza kufanya na likaleta mabadiliko makubwa, bali utahitajika kuchukua hatua ndogo ndogo ambazo zitapelekea utatuzi wa changamoto unayopitia.

6. Uongozi wa kimya kimya, ni njia ya kufikiria kuhusu watu, taasisi na hatua za kuchukua. Ni njia ya kujua namna gani mambo yanaenda na jinsi unavyoweza kuyafanya bora zaidi. Uongozi wa kimya kimya ni imani, kwa mambo madogo unayofanya yanayoweza kuleta matokeo makubwa.

7. Viongozi wakimya wanaishi kwenye uhalisia. Huwa wanaona dunia kama ilivyo na mambo namna yalivyo, hawajidanganyi kwamba mambo ni rahisi au ipo njia ya mkato ya kutatua. Wanajua kila tatizo au changamoto inahusisha mambo mengi, na hivyo hujipa uelewa wa kutosha kuchukua hatua. Hawategemei mambo yaende kama wanavyotaka wao, wanajua mara nyingi mambo yatakwenda vibaya zaidi ya wanavyotegemea, na wakati mwingine yatakwenda vizuri.

8. Viongozi wakimya wanathamini sana uaminifu. Wanajua ndiyo msingi pekee wanaoweza kuusimamia kwenye maamuzi yao. Pamoja na hayo huwa hawawaamini watu kabisa, wanajua kila mtu anafanya kitu kwa manufaa yake binafsi, na hata wao pia. Hivyo wanapofanyia changamoto kazi, wanategemea watu kufanya yale yanayowanufaisha.

9. Katika kufanya maamuzi ya changamoto au matatizo wanayopitia, viongozi wakimya hutumia misingi hii minne.

Moja; wanajua hawawezi kujua kila kitu, na hivyo hujipa muda wa kujua kiasi cha kuwatosha kufanya maamuzi.

Mbili; wanajua watashangazwa, pamoja na kujiandaa, wanategemea kukutana na mambo ambayo hawakuyategemea.

Tatu; wanaangalia wale wanaohusika kwa ndani. Kwenye kila jambo, kuna wahusika wa ndani na wahusika wa nje, wahusika wa ndani ni wa muhimu zaidi, kwa sababu wao ndiyo wanahusika kwenye maamuzi.

Nne; wanaamini lakini wanakuwa tayari kuchukua hatua sahihi, wanajua kuamini sana ni hatari kama kutokuamini kabisa.

10. Viongozi wakimya siyo watu wa kujitoa mhanga. Dunia inawatukuza watu wanaonekana kuitoa mhanga, kwa kuyatoa maisha yao kwa ajili ya wengine. Lakini huenda watu hao wangechukua hatua ndogo ndogo wangeleta mabadiliko makubwa. 

Hivyo unapojikuta kwenye hali ambayo inakuhitaji ujitoe mhanga, angalia kwanza kama hakuna njia nyingine za kupata ufumbuzi, hata kama zinachukua muda.

11. Viongozi wakimya hunaswa kwenye nia zinazojichanganya. Kwenye kuchukua hatua huwa na nia ya kutatua tatizo, lakini pia wakati huo huo hawataki kupoteza au kuumia wao. Kwa mfano kama mtu ameajiriwa, na bosi wake anamtaka achukue hatua ambazo siyo sahihi, hapo mtu anakuwa na nia zinazokinzana. Kumkatalia bosi lakini pia kulinda ajira yake. Hapo ndipo mtu anapaswa kuchukua hatua akizingatia hayo.

12. Kinachowafanya viongozi wakimya kufanikiwa, ni kuwa na nia zinazokinzana na kuweza kuzifanyia kazi. Yaani wanatatua tatizo, na wakati huo huo wanajilinda wao binafsi. Na wanafanya hivyo kwa kujipa muda, kuliua vizuri tatizo, na kutafuta njia mbadala za kufanya kitu.

13. Msingi muhimu wa viongozi wakimya ni kujali. Unapaswa kujali kuhusu lile unalofanya kabla haya hujaanza kulifanya. Kwa kujali ndiyo wanaweza kuweka juhudi zinazopaswa kuweka ili kubadili mambo namna yalivyo.

14. Dunia haitabiriki, dunia haieleweki, ni wale pekee wenye msukumo mkubwa kutoka ndani yao wanaoweza kufanya jambo kubwa kwenye maisha yao. Na hata hivyo jambo hilo hutokana na hatua ndogo ndogo wanazochukua, bila ya kukata tamaa. Usijaribu kutabiri chochote, usikazane kuielewa dunia, jua kipi unapaswa kufanya na kifanye.

15. Viongozi wakimya hawakimbilii kufanya maamuzi rahisi, badala yake wanajifunza kwa kina kuhusiana na hali wanayofanyia maamuzi, na kujua madhara ya maamuzi watakayochukua kabla hawajafanya maamuzi hayo. Ni kwa njia hii wanaepuka makosa na kufanya mamauzi bora.

16. Viongozi wakimya hununua muda pale ambapo wanakuwa hawajui hatua gani wachukue. Hujaribu kufanya mambo yatakayoongeza muda wa kufanya maamuzi, ili kujihakikishia wamejua vizuri kabla hawajafanya maamuzi. Usikimbilie kuamia jambo kama hujalijua kwa undani.

17. Viongozi wakimya huangalia uwekezaji ambao wameshafanya kabla ya kufanya maamuzi. Uwekezaji huu ni mtaji wa kisiasa, ambao unajengwa na sifa yake kwa wengine na mahusiano aliyojenga na wengine. Kila hatua unayochukua, jua inajenga au kubomoa sifa yako na mahusiano yako, hivyo angalia hilo kabla ya kuchukua hatua.

18. Viongozi wakimya huelewa kwamba dunia haileti mambo kwenye weusi na weupe, sahihi na siyo sahihi. Wanajua changamoto huwa zinakuja kwa namna ambayo kitu sahihi kufanya ni kile ambacho siyo sahihi. Lakini huwa makini wasifanye kwa manufaa yao binafsi.

19. Kila uwekezaji una hatari zake, na hatari ya viongozi kwenye maamuzi yao ni sifa na mahusiano yao. Hivyo kipimo cha uwekezaji wa viongozi ni mrejesho utakaotokana na kile wanachokiweka rehani. Iwapo matokeo yatakuwa makubwa na yenye manufaa, viongozi huchukua hatari ya kufanya jambo ambalo linaweza kubomoa sifa na mahusiano yao.

20. Viongozi wakimya husaidiwa na vitu hivi viwili; subira na ung’ang’anizi. Wanajua jambo lolote kubwa linahitaji subira, na hivyo hawakimbilii kufanya mambo ili kupata matokeo ya haraka. Pia wanajua changamoto zipo kila wakati, na hivyo huwa ving’ang’anizi kwenye yale wanayofanya.

Kila mmoja wetu ni kiongozi, tunachopaswa kufanya ni kuchukua hatua pale tulipo, kwa kuanza kutatua changamoto na matatizo yanayokukabili wewe na wale wanaokuzunguka. 

Kwa namna hii utayafanya maisha yako kuwa bora na hata ya wale wanaokuzunguka. 

Unaweza usiandikwe kwenye magazeti au vitabu, lakini utakuwa umefanya huduma kubwa hapa duniani. Chukua hatua sasa, kwa kuongoza kimya kimya.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita