Mawasiliano ni moja ya mahitaji muhimu sana kwa maisha ya kila mwanadamu. Ni mawasiliano ndiyo yanatuwezesha kupata kile tunachotaka, na hata kutoa kile ambacho tunacho kwa wengine. Bila ya mawasiliano, hakuna mahusiano.Lakini mawasiliano yamekuwa changamoto kwa wavulana. Hii inatokana na saikolojia yao, utofauti wao na hata malezi yao. Vijana wengi wa kiume wamekuwa wakipata shida kubwa ya mawasiliano kwa kukosa mwongozo sahihi, hasa kutoka kwa wazazi wao.

Mwanasaikolojia Adam Cox ametuandikia kitabu hichi, kutokana na taaluma yake na uzoefu wake katika kufanya kazi na vijana wa kiume wenye changamoto za mawasiliano.

Katika makuzi ya watoto wa kiume, huwa wanapitia vipindi mbalimbali. Kuna kipindi mtoto anaweza kuwa mkimya sana, haongei na watu na akiulizwa chochote anatoa majibu mafupi pekee. Kuna kipindi anaweza kuwa na hasira, jambo dogo tu anakuwa na hasira sana. Kuna wakati mtoto anaweza kuwa mtundu sana, yaani hawezi kutulia sehemu moja bila ya kuharibu kitu. Haya yote yanachangia watoto wa kiume kuwa na mawasiliano mabovu katika makuzi yao na kuwa changamoto kwao wanapokuwa watu wazima.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hichi, tujifunze namna gani tunaweza kuwasaidia watoto wetu wa kiume kuwa na mawasiliano bora, ili waweze kuwa na mahusiano mazuri.

1. Wavulana wa maneno machache.

Jina la kitabu hichi, wavulana wa maneno machache, linatokana na dhana ya wanaume wa maneno machache. Hawa ni watu ambao wanatumia zaidi matendo kuliko maneno katika kuwasilisha kile wanachotaka kiwafikie wengine. Inaweza kuonekana ni hali ya kawaida, lakini kwa zama hizi tunazoishi, inamrudisha mtu nyuma katika kujenga mahusiano mazuri na wengine. Na kama wote tunavyojua, hizi ni zama za mahusiano, kuanzia kwenye kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla.

Hivyo iwapo mtoto wako wa kiume ana tabia ya kutumia maneno machache na matendo zaidi, basi unahitaji kufanya kazi kubwa kumsaidia aweze kuwa na mawasiliano bora.

2. Mafanikio yanategemea mawasiliano kuliko kitu kingine chochote.

Mafanikio kwenye elimu, kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla, yanategemea zaidi kwenye mawasiliano. Hii ina maana kwamba, wale watu ambao wana mawasiliano bora, ndiyo wanaonufaika zaidi. Na mawasiliano haimaanishi tu kuongea, bali kujua unaongea nini na kwa wakati gani.

Kama mtoto wako wa kiume ana changamoto ya mawasiliano, ni mkimya sana na anapendelea zaidi kufanya mambo yake kuliko kujichanganya na wengine, hilo linaweza kuwa changamoto kwake baadaye. Ni jukumu lako mzazi kumsaidia ili aweze kujenga mawasiliano mazuri.

3. Wavulana wanavyotofautiana na wasichana kwenye mawasiliano.

Wasichana huwa wanajihusisha moja kwa moja kwenye kila kitu kinachotokea pale walipo. Wanaongea sana na wanajichanganya na wengine. Lakini wavulana hujitenga, hutafuta vitu wanaweza kufanya wao wenyewe, kama kucheza ‘game’. Wavulana wamekuwa siyo waongeaji sana na hujitenga na shughuli nyingi zinazohusisha watu wengi. Hapa ndipo changamoto za mawasiliano zinapoanzia, kwa sababu hawajifunzi kupitia wengine.

Wasichana huchukulia mawasiliano kama sehemu ya kujieleza, kueleza hisia zao na kujichangana na wengine. Lakini wavulana wamekuwa wanachukulia mawasiliano kama njia ya kupata wanachotaka tu. Kwa njia hii wanakuwa na maneno makali yanayoenda moja kwa moja kwenye kile wanachotaka, hii ni changamoto kwenye mawasiliano.

4. Changamoto inaanzia kwenye hisia.

Japokuwa hitaji la mawasiliano linaweza kuwa moja, atakavyoeleza mvulana ni tofauti kabisa na atakavyoeleza msichana. Kwa mfano iwapo watoto wawili, wa umri sawa, msichana na mvulana, wote wanataka kitu kimoja, msichana atasema kwa lugha yenye hisia na inayoshawishi, mfano; mama naomba unilipie safari ya shuleni kwenda kutembelea mbuga za wanyama, ambapo tutajifunza mengi kuhusu wanyama. Lakini mvulana anaweza kusema; mama shule tumeambiwa tupeleke hela ya safari ya mbuga za wanyama. Unaweza kuona tofauti hiyo ni ndogo, lakini ina vikwazo vingi kwa wavulana kwenye mawasiliano yao.

5. Tabia za kujilinda kwenye udhaifu wa mawasiliano.

Wavulana wakishagundua hawapo vizuri kwenye mawasiliano, wanatafuta tabia za kulinda udhaifu wao huo. Hivyo wanakuwa na tabia ambazo hazieleweki, mfano inaweza kuwa hasira zisizoeleweka. Mara nyingi mtoto anakuwa na hisia fulani, lakini hajui anawezaje kuzieleza kwa wengine, na hii inampelekea kuwa na hasira. Kitu kidogo anakasirika sana.

Tabia nyingine ni kujitenga na wengine, kama wengi wanavyoita antisocial, siyo kwamba wanakuwa wanafurahia kuwa wenyewe, ila mara nyingi wanakosa namna ya kujichanganya na wengine.

6. Matatizo ya wavulana yanachangia zaidi kwenye changamoto ya mawasiliano.

Wavulana wana uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya kiakili ya watoto kuliko wasichana. Matatizo yao ni kama utundu uliopitiliza (Attention-Deficit/Hyperactivity Disorder), uzito kwenye kuelewa darasani na ukaidi. Hayo yote yanawazuia kujifunza mawasiliano, kwa sababu wanakuwa pekee zaidi kuliko kujichanganya na wengine. 

Matatizo hayo yanawapata watoto wa kiume kuliko wa kike, na hilo linaongeza changamoto kwenye mawasiliano ya wavulana.

7. Pande mbili za ubongo kwenye mawasiliano.

Ubongo wa binadamu umegawanyika kwenye sehemu mbili, ubongo wa kulia na ubongo wa kushoto. Ubongo wa kushoto ndiyo tunautumia kwenye kufikiri na kutatua matatizo, ubongo wa kulia ni kwa ajili ya ubunifu. Wavulana wanatumia ubongo wa kushoto pekee kwenye mawasiliano, na hii inawafanya kushindwa kuongeza ubunifu na hisia kwenye mawasiliano yao. Wasichana wanatumia pande zote mbili kwenye mawasiliano, na hii inawafanya kuwa vizuri kwenye mawasiliano.

8. Baba na mama nao wanahusika.

Kwenye jamii inajulikana kwamba wanawake wanaongea sana kuliko wanaume. Sasa kwa asili, watoto wa kiume wanajifunza sana kutoka kwa baba zao au wanaume wengine. 

Na wasichana wanajifunza zaidi kutoka kwa mama zao na wanawake wengine. Hii inawafanya watoto wa kike kujifunza mawasiliano mapema na kwa upana kuliko wavulana. Hii ni kwa sababu wanaume wengi wamekuwa siyo watu wa kuongea na kujieleza sana kama wanawake.

9. Tabia ya asili ya kutaka kushinda.

Wanaume na hata kwa wavulana, kwa asili wanapenda kushinda. Ndiyo maana wanaume wengi wanapenda kushiriki michezo mbalimbali, kwa sababu dhana ya kupambana na kushinda ni muhimu kwao. Sasa hili pia linakuja na madhara, pale mwanaume anapojua hana uwezekano wa kushinda kwenye kitu fulani, anakiepuka. Hii ndiyo inatokea kwenye mawasiliano, mvulana akishajua hayupo vizuri kwenye mawasiliano, basi anaepuka kabisa hali yoyote inayomtaka yeye kuwasiliana na wengine. Hilo linazidi kuharibu mawasiliano yake.

10. Mawasiliano yanapobadilika na mazingira.
Wapo wavulana ambao mawasiliano yao yanabadilika kulingana na mazingira waliyopo. 

Kwa mfano mtoto anaweza kuwa akiwa nyumbani ni mkimya kabisa, lakini akitoka na kuwa na wenzake anaongea sana. Au akiwa shuleni, darasani ni mkimya, ila ukija wakati wa michezo, anaongea sana. Hii inatokana na hofu ambayo watoto wanakuwa ameijenga kwenye maeneo na uhuru wanaokuwa nao kwenye maeneo mengine.

Amri kumi za mawasiliano ya wavulana.

Wewe kama mzazi, mawasiliano ya mtoto wako wa kiume, ni jukumu muhimu kwako. 

Unapaswa kumsaidia kuweza kuelewa mawasiliano, kuweza kujieleza, kuweza kuelewa hisia za wengine, kuweza kutoa hisia zao na hata kujua mazingira na muktadha wa mawasiliano.

Zifuatazo ni amri kumi za kuimarisha mawasiliano ya wavulana, zifanyie kazi kwa kuangalia mazingira yako na changamoto ya mtoto wako.

11. Tenga Muda.

Mawasiliano ya watoto wa kiume yanahitaji muda, lazima uweze kuwa na muda wa kukaa na mtoto wako, kujua changamoto zake na kumsaidia katika kuzitatua. Lazima uwe naye karibu, ujue kila analopitia ili kumsaidia, asijione yupo mwenyewe na kujenga tabia za kujilinda.

Muda ni changamoto kwenye dunia ya sasa ambayo mambo ya kufanya ni mengi kuliko uwezo wetu. Lakini jambo moja muhimu sana, weka vipaumbele, na kwa watoto wako, kiwe kipaumbele kikubwa.

12. Waelewe kihisia.

Kuna kumwelewa mtu, halafu kuna kumweleza kihisia, kuvaa viatu vya mtu. Ili kuweza kumsaidia mtoto wako kwenye mawasiliano, lazima umwelewe kihisia, lazima uweze kuona kile anachopitia, na kumhakikishia kwamba unaelewa changamoto zake. Hii itamfanya yeye kuwa wazi kwako na kuwa tayari kukushirikisha changamoto zake na pia kuwa tayari kupokea msaada unaompa.

13. Utayari wa kuchukua hatua.

Wazazi wengi huona changamoto kwenye mawasiliano ya watoto wao, lakini hawajui ni wakati gani sahihi kuchukua hatua. Wengi huona ni utoto tu, wakikua wataacha, lakini linakuwa ni tatizo kubwa ambalo linaleta madhara zaidi baadaye.

Wewe kama mzazi, unapoona tabia za mtoto wako hazieleweki, tangu anapokuwa mdogo, kaa naye karibu na anza kufuatilia. Hii itakupa nafasi nzuri ya kuweza kuchukua hatua mapema kabla muda haujaenda sana. Kwa sababu kama wanavyosema, samaki mkunje angali mbichi, ukiweza kumsaidia mtoto akiwa bado mdogo, unamjengea kujiamini mapema.

14. Kuwa chanya wakati wote.

Hata kama mtoto ana changamoto kubwa kiasi gani, usikate tamaa na kuona huyo hawezi tena kusaidiwa. Endelea kuwa chanya wakati wote, kwa kuendelea kumsaidia mtoto. Hata kama anarudia makosa yale yale, kuwa chanya kwamba atafika wakati na kuwa bora zaidi.

Pia mtoto anakuangalia, na unapoanza kuwa hasi na kufikiri hataweza, analiona hilo. 

Hivyo endelea kuwa chanya, na kuamini ataweza kuwa bora, na yeye atakuamini na kuweka juhudi katika kuboresha mawasiliano yake.

15. Jifunze zaidi.

Malezi ni moja ya vitu ambavyo watu wengi tumekuwa tunachukulia kirahisi sana, tunafanya kwa mazoea. Ni mara chache sana utakuta mtu anasoma vitabu vya malezi, au kuhudhuria semina za malezi.

Jifunze zaidi kuhusiana na tabia za watoto, namna ya kuboresha mawasiliano ya watoto na mengine muhimu.

Unaweza kujifunza kwa njia rasmi, kupitia vitabu, magazeti, semina. Au pia unaweza kujifunza kupitia njia zisizo rasmi, kwa uzoefu wa wengine.

16. Fundisha.

Pamoja na jukumu lako kama mzazi kuhakikisha mtoto anapata mahitaji yote muhimu kwake, kufundisha ni kitu muhimu unapaswa kukifanya. Unapokuwa na mtoto wako mfundishe, siyo tu namna ya kufanya, bali kwa nini unafanya.

Kwenye mawasiliano hili ni muhimu, kwa sababu linamjenga mtoto kuingiza hisia kwenye mawasiliano yake. Kwa mfano umuhimu wa kumwangalia mtu unayeongea naye usoni, badala ya kuangalia chini. Hii inamfanya mtu kuaminika na kuona mwingine anapokeaje kile anachoambiwa. Lazima watoto wa kiume wafundishwe hili, maana huwa hawaelewi.

17. Kuwa mfano wa kuigwa.

Hata kama utafundisha na kuongea kiasi gani, watoto wanafanya kile ambacho wewe unafanya. Hivyo hakikisha wewe unakuwa mfano wa kuigwa kwa watoto wako, hasa linapokuja swala la mawasiliano. Watoto wanakuangalia kwa kila jambo unalofanya, namna unavyojieleza, namna unavyopokea mawasiliano ya wengine na kadhalika. Tumia kila nafasi kuwa mfano wa kuigwa kwa watoto wako.

18. Ushirikiano.
Katika kujenga mawasiliano mazuri ya mtoto wako wa kiume, unahitaji kushirikiana na watu wengine wengi. Unahitaji kushirikiana na walimu wake shuleni ili kujua tabia zake shuleni na anasaidiwaje, unahitaji kushirikiana na watoto wengine ili kuona wanamchukuliaje. Hayo yote yanajenga mazingira bora kwa mtoto kujifunza.

19. Uvumilivu.

Kama ilivyo kwenye kila jambo tunalofanya kwenye maisha, kujenga mawasiliano ya mtoto wa kiume ni jambo linalohitaji muda. Siyo kitu cha haraka, hakuna njia ya mkato. 

Lazima uwe tayari kuweka muda ili kufikia lengo la mtoto kuwa na mawasiliano bora. 

Uvumilivu mara zote huwa unalipa.

20. Jenga maadili ya familia.

Kila familia inapaswa kuwa na maadili yake, na watoto wanapaswa kuyajua maadili ya familia yao. Maadili ya familia yanapaswa kujengwa kwenye mawasiliano ya watoto, kuanzia namna ya kuwasiliana na wengine, kujali, kuheshimiana. Haya yanaimarisha zaidi mahusiano na kuboresha mawasiliano.

Familia zinatofautiana na watoto pia wanatofautiana, lakini changamoto nyingi zinafanana kwa kila familia na kwa watoto wengi. Kwa haya tuliyojifunza, tumepata tu mwanga wa namna ya kuwasaidia watoto wetu kwenye mawasiliano. Jukumu letu kubwa ni kuendelea kujifunza na kuendelea kufanya kazi na watoto wetu kwa karibu ili tuweze kuwajengea mawasiliano bora yatakayowawezesha kufanikiwa kwenye dunia ya sasa.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita