Habari rafiki?

Tangu nimeanzisha kipengele hichi cha USHAURI WA CHANGAMOTO INAYOKUZUIA KUFIKIA MAFANIKIO, mwaka 2014, hakuna kitu ambacho kimekuwa kinaombwa ushauri kama biashara, hasa wapi pa kuanzia.Makala tu ambazo nimeshaandika za kushauri hilo ni nyingi mno, kuanzia wazo la biashara, upateje mtaji, usimamizi na hata kushirikiana na wengine. Lakini bado kila siku yupo mtu ataomba ushauri wa jinsi gani aanze biashara.

Kwa kuwa ninyi ni marafiki zangu, na jukumu nililojipa ni kuhakikisha nawashirikisha maarifa sahihi ya kuweza kufanya maamuzi sahihi, nitaendelea kuliandikia hili mara kwa mara.

Lakini kabla sijaendelea kuliandikia hili, napenda leo nitoe angalizo, kulingana na uzoefu wangu kwa wale ambao wanataka kufanya biashara na wanaofanya biashara kweli.

Kabla sijakueleza angalizo hilo kwa kina, tusome maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hili;

Nina malengo ya kuwa mfanya biashara, lakini napata changamoto kwenye maswala ya kupata mtaji utakaoweza kuniruhusu kuanza biashara yangu. je nifanyeje? Naomba msaada wako. Asante. – Steven P. Y.

Kama alivyoandika rafiki yetu Steven hapo juu, ana malengo ya kuwa mfanyabiashara, lakini hana mtaji wa kuanza. Na anataka kujua aanzeje.

Hivyo ninachokwenda kumwambia ndugu Steven ni kile anachopaswa kufanya, siyo anachofikiria kuja kufanya.

Kwa uzoefu wangu, kupitia watu ninaowajua, na wale ambao ninawashauri, kuna makundi mawili ya watu linapokuja swala la biashara.

Kundi la kwanza ni wale ambao wanapanga kuingia kwenye biashara. Hawa wanasema wana mpango wa kuingia kwenye biashara, ila kila wakati wana sababu inayowachelewesha, wengi husema mtaji, wengine wazo, wengine muda na sababu nyingine zinazowafaa.

Kundi la pili ni wale ambao wanafanya biashara. Hawa hawana maneno mengi, wao wanafanya biashara, na siyo kwamba hawana vikwazo, wanavyo sana, ila hawaruhusu vikwazo hivyo kuwazuia, bali wanavitumia kama kichocheo cha kuweka juhudi.

Hivyo ninachotaka ndugu yetu Steven aelewe ni kwamba, kuwa na mpango wa kuwa mfanyabiashara ni mzuri, ila haukufikishi kwenye biashara mpaka pale ambapo unaingia kwenye biashara kweli.

Kama unataka kuwa mfanyabiashara, hakuna chochote kinachokuzuia kwenye zama hizi, ambazo unaweza kumiliki biashara bila hata ya kuwa na eneo la kufanyia biashara. 

Unaweza kufanya biashara ukiwa nyumbani kwako na huduma au bidhaa, ukatafuta soko kupitia mtandao, na kisha kuwasambazia biashara. Kitu pekee kinachoweza kumzuia mtu kuingia kwenye biashara, ni yeye mwenyewe.

Baada ya kusema hayo machache, naomba niwashirikishe njia za kuanza biashara kama huna mtaji.

1. Anza na biashara ya huduma.

Biashara nyingi za huduma hazihitaji wewe uwe na mtaji wowote. Hapa unatoa huduma ambayo inategemea ujuzi ulionao, au nguvu zako, na hata muda wako. Inaweza kuwa kuwasaidia watu kupitia kile unachojua, au kuwafundisha kile ambacho unajua. Pia inaweza kuwa kuwasaidia wale ambao wana uhitaji wa vitu fulani ila wao hawana muda wa kuvifanyia kazi.

Kulingana na mazingira yako, angalia ni huduma gani unaweza kutoa kwa wanaokuzunguka, kulingana na uhitaji wao au changamoto zao. watu wanahangaika na kitu gani ambacho unaweza kuwasaidia? Chukua hatua na wasaidie.

2. Anza kwa kuajiriwa au vibarua kukusanya mtaji.

Mtaji bora kabisa wa kuanza biashara, ni fedha zako mwenyewe. Siyo mkopo kwa sababu utakuumiza, na wala siyo fedha za ndugu kwa sababu zinakuja na masharti. Hivyo ni vyema kujishughulisha, kwa lengo la kukusanya mtaji.

Kama una ujuzi au sifa, omba ajira na fanya kwa kipindi pekee, lengo likiwa kukusanya mtaji. Kama huna sifa za kuajiriwa, au unazo lakini ajira ni shida, fanya vibarua, angalia ni kipi unaweza kufanya na omba mtu umsaidie kufanya. Wala usitake fedha mwanzoni, wewe sema utamsaidia nini, mwombe akupe nafasi ya kusaidia, fanya vizuri halafu yeye aone anakulipaje. Hapo lengo wewe ni kukusanya mtaji.

3. Anza kidogo, anzia chini kabisa.

Kitu kimoja ninachoamini ni hichi, unapoamua kweli kufanya kitu, hakuna anayeweza kukurudisha nyuma. Kila unapoangalia, utaona fursa za kuanzia. Hivyo panga kuanza, anzia chini kabisa, anza kidogo. Anza na biashara unayoweza kuanzia chini, kwa pale ulipo. Labda kuna kitu ambacho hukitumii, kiuze, kisha hiyo fedha, itumie kununua kitu kingine unachoweza kuuza, na kuendelea hivyo. Ukienda kwa nidhamu, baada ya muda utajikuta mbali sana.

4. Fanya biashara ya mtandao (network marketing).

Hii ni biashara unayoweza kuanza kwa mtaji kidogo au hata bila ya mtaji kabisa. 

Unaweza kuchagua kampuni unayoweza kuanzia nayo chini, ukapambana na kuweza kujifunza biashara na kutengeneza mtaji pia. Yapo makampuni ya biashara hii ambayo yanatoa mafunzo mazuri kibiashara, kwa kuwa kwenye makampuni hayo, utajifunza mengi kuhusu biashara na hata kujua unaweza kuanzaje biashara yako nyingine. Kama ungependa kujua zaidi kuhusu biashara ya mtandao, soma kitabu nilichoandika, kinaitwa IJUE BIASHARA YA MTANDAO, kukipata tuwasiliane kwa namba 0717 396 253.

5. Anzisha blog yako na iendeshe kibiashara.

Mtandao wa intaneti kwa sasa umekuwa fursa kubwa ya kibiashara kwa mtu yeyote anayeweza kuutumia vizuri. Hivyo mtu yeyote, anaweza kutumia mtandao wa intaneti kibiashara, kwa kuwa na blogu ambayo ataitumia kuuza huduma na bidhaa zake, au hata kutangaza biashara za wengine. Ni biashara unayoweza kuanzia chini kabisa na kuweza kuikuza kadiri uwezavyo. Kama ungependa kujua zaidi jinsi ya kutumia blogu kibiashara, nimeandika kitabu kinaitwa JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG. Kitabu hichi kitakupa mwanga, kipate na ukisome. Kukipata tuwasiliane kwa namba 0717396253.

Rafiki yangu, kama unaendelea kujiambia unapanga kuingia kwenye biashara, basi utapanga milele. Ila kama kweli unataka kuingia kwenye biashara, unachopaswa kufanya ni kuamka na kuingia kwenye biashara, kwa kuanzia hapo ulipo sasa. Na uzuri ni kwamba, ukishaamua kweli, hakuna wa kukuzuia.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog