KITABU; Meditations / Marcus Aurelius.
UKURASA; 19 – 28.

Kwenye maisha yetu, tumekutana na watu mbalimbali, kuanzia tunazaliwa mpaka tunakuwa watu wazima.
Kila mtu ambaye tumewahi kukutana naye kwenye maisha yetu, ana mchango fulani kwa pale tulipo sasa.
Ukianza na wazazi, ndugu wa karibu, walimu, marafiki na hata viongozi mbalimbali, kuna vitu wamechangia kwenye maisha yetu.

Wengi huwa hatutambui hili na badala yake tunakuwa rahisi kuona makosa na mapungufu ya wengine.
Kwenye kitabu cha kwanza cha Meditations, Marcus Aurelius anachukua nafasi ya kumshukuru kila mtu ambaye amekuwa na mchango fulani kwenye maisha yake.

Anaanza kwa babu yake ambapo alijifunza kuwa mnyenyekevu na msikivu, kuepuka hasira na mapenzi ya vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wake.

Kwa mama yake alijifunza kuwa mtu wa imani, kuridhika na kidogo anachopata na kuepuka kuwa mtu wa tamaa kwa vitu vingi.

Kutoka kwa Giognetus alijifunza kutokupoteza muda wake kwa kufanya yasiyo sahihi. Pia kutokuamini kiurahisi chochote kinachosemwa na kila mtu.

Kutoka kwa Apollonius alijifunza uhuru wa kweli kwenye maisha ni kuridhika na vichache na siyo kuwa na vingi. Pia kuendelea kuwa mtu yule yule iwe unapitia mazuri au mabaya.

Kutoka kwa Sextus alijifunza kuishi kulingana na sheria za asili. Kutokukasirishwa na matendo ya wengine na kutokulazimisha mambo yaende kama anavyotaka yeye.

Kutoka kwa Alexender alijifunza kutokuwasema wengine vibaya wala kumsingizia mtu yeyote kitu chochote.

Katika kitabu hichi cha kwanza ameendelea kuwataja watu wengi zaidi ambao wote wamemfundisha jinsi ya kuwa na maisha bora, kuridhika na kile alichopata na kuishi kuendana na sheria za asili.

Je wewe ni watu gani unawashukuru kwenye maisha yako kwa hapo ulipo sasa? Ni watu gani ambao umejifunza kwao na leo unajivunia kwa hatua ulizopiga? Kuchukua hatua ya kuwashukuru watu hao japo kwa ndani yako ni muhimu kwa maisha yako.

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa