Tukiishi katika maisha ya visasi hatutafika bali tutazaa mauti. Ni vema kusamehe kwa faida yako na kisasi mwachie Mungu apambane na watesi wako. Mtesi wako mwekee kaa la moto kichwani, atembee nalo mwishowe litamchoma. Katika maisha kuna watu ambao wamekuwa miiba katika miili ya watu, wamekuwa vikwazo kwako,wamekusababishia majeraha ya moyo, wamejeruhi nafsi yako kwa namna moja au nyingine. Hivyo basi, kila mtu atakua amepitia mateso fulani katika maisha yake na kuumizwa sana nafsi yake.

Ili upate furaha ya moyo yakupasa kuondoa uchungu ulioumbika ndani ya moyo wako. Unaondoa uchungu ulioumbika katika moyo wako kwa kusamehe na kuanza maisha mapya. Samehe ili uweze kusamehewa na wala usilipe kisasi kwa mtu aliyekufanyia ubaya bali njia pekee ni kumwachia Mungu apambane na watesi wako. Samehe kwa faida yako wewe mwenyewe.

hour to live

Hakuna adhabu kubwa kama kumwekea mtu kaa la moto kichwani au kumtesa kisaikolojia,kiakili. Kwa mfano, ndugu x anakufanyia ubaya halafu wala wewe ukagundua kuwa amekufanyia ubaya badala ya wewe kumrudishia ubaya unaendelea kumtendea wema ule ule wa mwanzo. Yule ndugu x utakuwa unamtesa sana kwanza atakuwa anajiuliza iweje mtu huyu nime mfanyia ubaya wote lakini yeye haniambii neno lolote zaidi zaidi ananitendea tu wema. Hali kama hiyo huwa inawatesa sana watu wengine wanaamua hata kujimaliza kwa kujinyonga kwa kuona aibu  kwa mtu aliyemtendea ubaya hajamfanyia chochote na huku akitegemea kufanyiwa kisasi.

SOMA; Kitu Pekee Ambacho Mtu Mwenye Wivu Hana

Usitake kupambana na mtesi wako wewe tumia mbinu hii ya kumwekea kaa la moto kichwani tu. Kumwekea mtu kaa la moto kichwani ni kama vile kumwachia hatia ndani yake yaani guilt juu ya kile alichokufanyia, hata mtu akikutukana, akikuongelesha kwa ukali na hasira, ukikaa kimya bila kumjibu ni sawa na kumwekea kaa la moto kichwani kwa sababu baadaye anapokuja kukaa mwenyewe ataanza kujirudi na kujitambua kuwa hakika mtu yule sijamtendea sawa.

Ndugu mmoja aliwahi kumfumania mwenza wake baada ya kurudi nyumbani yule mke wake alitegemea mume wake atampiga au kumfanyia kitu kibaya. Mambo yakawa tofauti yule ndugu hakumuuliza wala kumfanyia chochote akajifanya kama vile hajui chochote na aliendelea kuwa na uhusiano kama ule wa awali. Yule mwanamke akawa anaumia sana moyoni, anajiuliza mbona nimemfanyia ubaya lakini yeye ananitendea tu wema? Basi ile hali ya kumwacha kama alivyo tunaweza kuita kumwekea mtu kaa la moto kichwani au kumtesa kisaikolojia. Basi, yule mwanamke ilibidi tu afungashe aondoke pale kwa mume wake kwani hali ile ilimtesa sana na akawa na maswali mengi kweli badala ya mkosewa ndiyo apate shida lakini mkosa ndiyo anapata shida.

Hatua ya kuchukua leo, kama kuna mtu amekukosea amua leo kumfutia deni, unapoamua kumfutia  mtu deni maana yake umeamua kumsamehe lile deni ambalo alipaswa kulilipa kama mdaiwa unalifuta. Ni uamuzi wa makusudi kabisa. Usijisumbue kutaka kulipa visasi na watesi wako, bali wewe wawekee kaa la moto kichwani na mwachie Mungu apambane na watesi wake.

SOMA; Huu Ndiyo Wakati Sahihi Wa Kutua Mizigo Tuliyobeba Kwenye Mioyo Yetu.

Kwahiyo, tunapoamua kuwasamehe wenzetu tunakuwa tumechukua hatua za kurudisha yale mahusiano ya awali. Muda mwingine mpaka tunakwepana hata kwa kubadilisha njia kama  umemuona mtesi wako anakuja mbele yako, hivyo njia pekee ya kuishi maisha huru ni kuamua kusamehe.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu, kwa kutembelea tovuti  hii  hapa  www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana na karibu sana !