Kuwavutia wateja kwenye biashara yako siyo kitu kigumu sana, wengi wamekuwa wanadanganya na kutumia mbinu ambazo siyo sahihi ili tu kuwafanya wateja waje, na wengi wanakuja, ila wakishakuja mara moja hawarudi tena.
Kuwavutia wateja na kuwafanya wakuamini kiasi cha kuweza kurudi tena na hata kuwaambia wengine waje kwako, ni kitu chenye manufaa sana kwako na kwa biashara yako. Ni kitu ambacho kinahitaji kazi kiasi ili kuweza kukitekeleza lakini kina matokeo mazuri sana kwa biashara yako.
Njia ya kudanganya, kulaghai na hata kupunguza bei vinaweza kuwavutia wateja kuja kwenye biashara yako kwa mara moja, lakini wasirudi tena kwa mara nyingine. Hii ni kwa sababu yale unayokuwa umewaahidi hawayapati na uaminifu wao kwako haujengeki kabisa.
Kuna hatua mbili muhimu sana kwenye kuwavutia wateja na kuwafanya wakuamini,
Hatua ya kwanza ni kuweka ahadi zenye manufaa kwa wateja wako. Jua tatizo au hitaji kuu la mteja wako ni lipi, kisha weka ahadi ya kutatua tatizo au kutimiza hitaji hilo. Eleza kwa hakika nini mteja ategemee anaponunua na kutumia kile unachouza. Hapa unamfanya mteja awe na shauku ya kujaribu kile unachouza.
Hatua ya pili ni kutimiza kila ahadi unayoweka. Umewaambia watu watapata kitu fulani basi wakipate hasa, umewaahidi unachowauzia kitatatua matatizo yao basi kitatue kweli. Hakuna kitu kinachomuumiza mteja kama kuja kwenye biashara yako na matarajio fulani, mwishowe anaondoka kwa matarajio hayo kuwa yamevunjika.
Kitu kikubwa kinachowaumiza wateja na kupelekea biashara nyingi kukosa wateja ni ahadi zisizotekelezwa, matarajio yasiyotimizwa. Wateja wanakuja wakiwa na matarajio ya juu, lakini wanachopata ni tofauti kabisa na walichotegemea. Wanaondoka wakiwa wamevunjika moyo na kukata tamaa na hawawezi kurudi tena kwenye biashara hiyo.
Njia za mkato za kupata wateja wengi, kama kudanganya, kulaghai na kupunguza bei, huwa zinaishia kuwavunja moyo wateja kwa sababu njia hizo haziwezi kumpa mteja kile anachotaka.
Ndiyo maana wewe unapaswa kuepuka sana njia hizo, tumia hatua hizi mbili, ahidi kitu chenye manufaa kwa wateja wako na hakikisha unatimiza ahadi hiyo, kama ulivyoitoa. Pambana uwezavyo kuhakikisha kile ulichoahidi umekitekeleza. Kwa sababu mteja anakupa nafasi moja tu, kama utaitumia vibaya, hutamwona tena.
Maumivu ya ahadi zilizovunjwa na matarajio yasiyotimizwa yanadumu kwa muda mrefu, epuka sana kuyasababisha kwa wateja wako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kocha kwa haya mambo mawili ya kufanyia kazi kwa mstakabali wa ustawi wa biashara zetu.
LikeLike