Rafiki yangu mpendwa,

Jukumu la kuu la biashara yoyote ile ni kutengeneza wateja wanaoiamini na kuitegemea biashara hiyo. Kisha wateja hawa wataleta faida kwenye biashara hiyo na hatimaye lengo la biashara linakuwa limefikiwa.

Wengi wanapoingia kwenye biashara huwa wanakazana kuangalia faida pekee, ambayo hawaipati na biashara inakuwa ngumu.

Kama wewe utabadili kile unachoangalia, ukaacha kuangalia faida pekee na kuanza kuangalia wateja ambao unawatengeneza kwenye biashara yako, utaiwezesha biashara yako kukua zaidi.

Kwenye biashara yoyote unayofanya sasa, kuna wateja muhimu sana ambao hupaswi kuwapoteza. Hawa ni wateja ambao wapo tayari kununua kile unachouza na wapo tayari kuwafikia wengine na kuwashawishi waje kununua.

Wateja ninaotaka kukushirikisha leo, ni wale wateja ambao tayari unao, wale wateja ambao tayari wameshanunua kwako.

Kama biashara itakuwa ni mgodi, basi wale wateja ambao walishanunua kwako ni shimo la dhahabu, ambapo muda wowote unaweza kuchimba na kuondoka na dhahabu ya kutosha.

NETWORK MARKETING

Kuwa na mteja ambaye ameshanunua kwako ni nafasi bora sana kwako kuwatumia vizuri ili kukuza zaidi biashara yako.

Mteja ambaye tayari ameshanunua kwako, na kama ulimhudumia vizuri ni mteja ambaye tayari ameshajenga imani na biashara yako, tofauti na wateja ambao hawajawahi kununua kwako.

Mteja ambaye ameshawahi kununua kwako, anajua kile unachouza na anajua kinamsaidiaje, hivyo hahitaji ushawishi mkubwa ili kununua tena, kama ule unaopaswa kuutoa kwa wateja wapya.

Hivyo jukumu lako kuu la kwanza kwa upande wa wateja wa biashara yako ni kuhakikisha wale wateja ambao walishanunua kwako, wanaendelea kuwa na imani kubwa kwenye biashara yako na wanaendelea kununua zaidi na zaidi.

Usikubali kamwe kumpoteza mteja ambaye tayari alishanunua kwako, kwa sababu utapoteza kitu kikubwa sana kwenye biashara yako.

Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanafanya kosa moja kubwa sana, wamekuwa wanakazana kupata wateja wapya na kusahau wale wateja ambao tayari wakishanunua kwao. Wanaweka nguvu nyingi kuwapata wateja wapya, na kuwasahau wale wateja ambao tayari wanao.

Kumpata mteja mmoja mpya mpaka anunue, inakuhitaji nguvu nyingi kuliko kuwakumbusha wateja kumi ambao walishanunua kwako kununua tena.

SOMA; Hii Ndiyo Njia Moja Ya Uhakika Ya Kuwashawishi Wateja Kununua Chochote Unachouza.

Na kila biashara, huwa ina wateja ambao walishawahi kununua lakini kwa sasa hawanunui tena. Na siyo kwamba hawana uhitaji wa kununua, bali wanakuwa wameachwa nyuma na biashara. Wateja wa aina hii kama wakikumbushwa basi wanarudi na kuendelea kununua.

Ni lazima wewe kama mfanyabiashara uelewe kwamba wateja wako wanakutana na kelele nyingi na wao binafsi wana mambo mengi kwenye maisha yao, hivyo inaweza kuwa rahisi kwao kusahau kurudi tena kwako na kwenda kwa wengine.

Hivyo moja ya majukumu yako ni kuhakikisha unakuwa na mawasiliano ya kila mteja ambaye ameshawahi kununua kwako na mara kwa mara wakumbushe kuhusu biashara yako na wakaribishe kuja kununua tena.

Ukiweka nguvu kubwa kwenye wateja ambao tayari walishanunua kwako, utaweza kuongeza mauzo kwa kiasi kikubwa na faida pia. Pia utaweza kuwatumia wateja hao kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi wa biashara yako.

Usisahau wateja ambao walishanunua kwako, ni wateja ambao bado wanahitaji muda wako na kukumbushwa ili kuendelea kuja kununua, lifanye hili kuwa jukumu lako kwenye biashara.

Leo anza kwa kuwakumbuka wateja wote ambao wamewahi kununua kwako siku za nyuma lakini hujawaona tena, tafuta mawasiliano yao na wakaribishe tena kwenye biashara yako.

Pia kila unapopata nafasi ya kumhudumia mteja, mhudumie kwa ubora wa hali ya juu sana kitu kitakachomfanya arudi tena na tena na tena. Kwa sababu mteja akishanunua kwako mara moja, na ukawa umemhudumia vizuri kwa kumpatia kile chenye msaada kwake, hatakuwa na sababu ya kutokurudi tena kwenye biashara yako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL