Bahati nasibu na michezo mingine ya kubahatisha imekuwa ni kimbilio la wengi katika zama hizi. Jinsi ambavyo michezo hii inatangazwa na kupambwa, inawafanya wengi waamini kwamba wanaweza kushinda pia kama na wao watacheza.

Tena kwa jinsi ambavyo zawadi zimewekwa kubwa, na uwekezaji wa mtu kuwa mdogo, inamfanya mtu aone kidogo anachotoa siyo kitu. Mfano kama mtu anaambiwa anacheza kwa shilingi mia tano, lakini anaweza kushinda shilingi milioni kumi, hiyo milioni kumi inamfanya mtu aone mia tano siyo kitu. Mtu atajiambia hata nikipoteza mia tano siyo kitu, ila naweza nikashinda milioni kumi.

Sasa tatizo kubwa sana la michezo ya kubahatisha siyo tu kupoteza fedha, japo nalo ni tatizo, ila tatizo kubwa zaidi ni namna inaharibu fikra za mtu linapokuja swala la mafanikio na kupata fedha. Inakufanya mtu uache kutegemea uimara ambao upo ndani yako, na uyaweke maisha yako kwenye bahati. Inakufanya mtu uache kujitegemea na kutumia uimara wako na kukufanya utegemee wengine na jinsi mambo yatakavyotokea.

Hakuna mtu anayefanikiwa kwenye maisha ambaye hajatumia uimara uliopo ndani yake, na hii ni kwa sababu mafanikio siyo tukio la mara moja, mafanikio ni mchakato mrefu. Watu wanapata na kukosa, wanapiga hatua kwenda mbele na baadaye kurudi nyuma. Kama mafanikio yangekuwa tukio, kila ambaye amewahi kukutana na bahati fulani na kupata vitu vingi kwa pamoja, angebaki kuwa na mafanikio. Lakini wengi hupoteza vitu hivyo.

Hata wale wanaoshinda bahati nasibu, baada ya muda maisha yako hurudi kawaida na wakati mwingine huwa chini ya kawaida. Yaani mtu anaweza kuwa na maisha mabovu sana baada ya kushinda bahati nasibu kuliko aliyokuwa nayo kabla ya kushinda.

Suluhisho la hali hii rafiki ni kutengeneza bahati nasibu yako mwenyewe. Jitengenezee maisha ya kujua, kuendeleza na kutumia uimara ambao upo ndani yako. Jitengenezee upendeleo wa kipekee kwako kiasi kwamba wale wenye uhitaji wa kile ambacho wewe uko imara nacho, wanakuja kwako moja kwa moja.

Kwa njia hii unajihakikishia ushindi kila siku, na hutegemei bahati au kile kinachotokea, badala yake unategemea kile unachoweza kufanya na matokeo unayoweza kuzalisha.

Jitengenezee bahati nasibu yako mwenyewe kwa kujiweka kwa namna ambayo sehemu ya mtiririko wa fedha kwenye uchumi unaingia na kwako pia. Kama ambavyo mtu anaweza kutoa mfereji kwenye mto mkubwa.

Ukishaweza kujijengea bahati nasibu ya aina hii, utaondokana na hali ya utegemezi kwenye bahati, haiwi tena bahati kwako, bali inakuwa ni mipango unayoweza kutegemewa. Japo watu wengi wa nje wataona una bahati, wengi hawataona yale maandalizi makubwa uliyoweka awali kabla matokeo hayajaanza kuonekana.

Jijengee bahati nasibu yako kwa kujua uimara uliopo ndani yako na kuutumia ipasavyo, tumia kile ulichonacho kutoa thamani zaidi, kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi na wao watakuwa tayari kukupa fedha zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha