Kanuni ya masoko na matangazo ni hii, watu wanahitaji kuambiwa kitu mara saba kabla hawajakisikia kwa mara ya kwanza.

Ndiyo maana unaona makampuni na biashara nyingi huwa zinakuwa na matangazo yanayojirudia rudia mara kwa mara.

Ni asili ya binadamu kwamba mtu anapoambiwa kitu kwa mara ya kwanza hakipi uzito wowote, anakipuuza kabisa, anapokisikia kwa mara ya pili anakipotezea pia, mara ya tatu anakumbuka alishasikia kitu hicho mahali, mara ya nne anaamua kusikiliza, mara ya tano anataka kupata maelezo zaidi, mara ya sita anafanya maamuzi na mara ya saba anachukua hatua.

Hivi ndivyo saikolojia yetu binadamu ilivyo, hakuna mtu anayesikia kitu mara moja na kuchukua hatua, hata kama ana uhitaji kiasi gani. Tunahitaji kusikia tena na tena na tena ndiyo akili yetu ishawishike kufuatilia na kisha kuchukua hatua.

Sasa rafiki yangu nimekushirikisha hili ili uweze kulitumia kwenye kila eneo la maisha yako, yaani kwenye kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla.

Kwenye kazi kama kuna kitu unachotaka watu wafanye au tabia unataka wabadili, usiwaambie mara moja na kuona wameshaelewa, unapaswa kurudia kuwaambia tena na tena, kadiri wanavyoendelea kusikia ndiyo watafika hatua ya kuchukua hatua.

Kwenye biashara, usichoke kuwaambia wateja wako kuhusu bidhaa na huduma unazotoa, usijiambie umeshawaambia na tayari wanajua. Kuna watu wengi hawajui hata kama upo kwenye biashara unayofanya. Na hata wale ambao ulishawaambia, wengi wameshasahau, maana wanasumbuka na mambo mengi kwenye maisha yao. Hivyo rudia kuwaambia tena na tena na tena. Kwa kuwa na mawasiliano yao endelea kuwasiliana nao mara kwa mara. Inaweza kuchukua hata miaka, lakini siku moja mteja huyo akaja kununua.

Kwenye maisha yetu ya kawaida, kwenye mahusiano na maeneo mengine ya maisha hayo, kile tunachotaka wengine wafanye lazima tukipe msisitizo mkubwa. Kusema kitu mara moja na kuachana nacho, ukiamini mtu ameelewa ni kujiandaa kuangushwa. Hata kama mtu ameelewa kabisa, endelea kukumbushia mara kwa mara. Watu wanapoona unakumbushia sana wanajua ni muhimu, wanalipa jambo kipaumbele na kulikamilisha ili kuondokana na hali ya kukumbushwa kila mara na wewe.

Kumbuka, watu wanahitaji kusukia kitu mara saba kabla hawajaamua kuchukua hatua, je wewe umeshawaambia watu kitu mara ngapi mpaka ujiambie hawasikii? Kama ni chini ya mara saba, siyo kwamba hawasikii, bali wewe ndiyo hujawaambia bado.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha