#TANO ZA JUMA #18 2019; Wewe Siyo Biashara Yako, Nguzo Sita Za Biashara Yenye Mafanikio Makubwa, Hatua Nane Za Kujenga Biashara Yenye Maono Makubwa, Pesa Kama Damu Ya Biashara Na Muhtasari Wa Kufanikiwa Kwenye Biashara.

Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye TANO ZA JUMA la 18 la mwaka huu 2019. Naamini limekuwa juma la mafanikio makubwa kwako, juma ambalo umeweza kuchukua hatua kubwa na kupata matokeo bora kabisa.

Juma hili tunakwenda kujifunza kwa kina namna ya kujenga biashara yenye mafanikio makubwa. Tunakwenda kujifunza mwongozo wa kuendesha biashara kwa mfumo bora wa kijasiriamali, ambao unaweka msisitizo kwenye nguzo sita pekee za kuikuza biashara.

Mafunzo haya ya kina kuhusu ukuaji wa biashara tunakwenda kuyapata kutoka kitabu kinachoitwa TRACTION; Get A Grip On Your Business kilichoandikwa na Gino Wickman. Kwenye kitabu hiki, Gino anatuambia kama tutazingatia maeneo sita muhimu ya biashara ambayo ameyafundisha, biashara zetu zitakua na kuwa huru, kiasi kwamba hazitegemei uwepo wetu wa moja kwa moja ndiyo ziweze kwenda.

Traction_FrontCover

Kwa kuwa kila mmoja wetu anapaswa kuwa na biashara, basi haya ni mafunzo muhimu sana tunayopaswa kuyapata na kuyazingatia. Karibu kwenye TANO ZA JUMA hili ujifunze na kuweza kuboresha biashara yako.

#1 NENO LA JUMA; WEWE SIYO BIASHARA YAKO.

Hiki ni kitu ambacho kila mfanyabiashara anapaswa kuambiwa, tena kupigiwa kelele kila mara mpaka aelewe. Kwa sababu kama wafanyabiashara wakielewa hili, nusu ya matatizo ya biashara yatatoweka yenyewe.

Sehemu kubwa ya matatizo ya biashara yanasababishwa na mfanyabiashara kufikiri yeye ni biashara yake, kitu ambacho siyo kabisa.

Biashara nyingi hazikui kwa sababu hakuna mpaka baina ya biashara na mmiliki wa biashara. Mtu anaweza kutoa fedha kiholela kwenye biashara kwa sababu anaona biashara ni yake. Kitu ambacho kinakuwa na athari kubwa sana kwenye ukuaji wa biashara hiyo.

Rafiki, naomba nikusisitizie hili, na liandike mahali ambapo utaweza kulisoma kila siku; WEWE SIYO BIASHARA YAKO, wewe na biashara yako ni vitu viwili tofauti kabisa.

Wewe una maisha yako, ndoto zako na mahusiano yako, biashara ina maisha yake, ndoto zake na mahusiano yake. Kinachowaunganisha wewe na biashara yako ni mtaji ambao umeuweka kwenye biashara hiyo, mtaji huo umeikopesha biashara, na njia pekee ya kunufaika kupitia biashara hiyo ni pale inaopata faida baada ya kufanyika kwa biashara.

Ukiweza kuelewa hili, kwamba wewe siyo biashara yako, ukaiheshimu biashara yako na kuiacha ikue bila ya kuiingilia, ukaiendesha kwa misingi ya ukuaji wa biashara, utaiwezesha biashara hiyo kukua zaidi.

Na muhimu zaidi, biashara hiyo itakuweka huru. Watu wengi waliopo kwenye biashara hawapo huru, hii ni kwa sababu hawamiliki biashara kama ambavyo wanafikiri, badala yake biashara zinawamiliki wao.

Kama ukiondoka kwenye biashara kwa mwezi mzima biashara hiyo haiwezi kujiendesha basi humiliki biashara, bali biashara inakumiliki wewe.

Ili uimiliki biashara yako, unapaswa kuitengenezea mifumo ambayo inaweza kujiendesha yenyewe. Unahitaji kuwa na maono makubwa kwenye biashara hiyo na misingi sahihi inayosimamiwa. Unahitaji kuwajiri watu bora wa kukusaidia kuendesha biashara hiyo na kuwaamini katika majukumu unayowapa. Haya yote tunakwenda kujifunza kwenye kitabu cha juma hili.

Kitu kimoja muhimu kwako kukumbuka kila wakati ni wewe siyo biashara yako, unapaswa kuiendesha biashara na siyo biashara kukuendesha wewe.

#2 KITABU CHA JUMA; NGUZO SITA ZA BIASHARA YENYE MAFANIKIO MAKUBWA.

Kama unataka kufurahia biashara yako, basi unapaswa kufanya kazi nje ya biashara na siyo ndani ya biashara. Kufanya kazi ndani ya biashara ni pale ambapo unakuwa bize na shughuli za kila siku za biashara hiyo, kuuza, kuwahudumia wateja na kuzalisha au kuandaa bidhaa na huduma unazouza. Japokuwa unaweza kuona hilo ni muhimu na hata kupenda sana kulifanya, linakuzuia kuikuza zaidi biashara yako, maana unapofanya kazi ndani ya biashara, unachoka sana na hupati nafasi ya kuona mbali zaidi ya kile unachofanyia kazi kwenye biashara hiyo.

Kufanya kazi nje ya biashara yako ni pale ambapo unaiangalia biashara yako kama mtu baki, kuangalia kila kitu kinavyofanyika na kuona uimara na udhaifu wako. Ni sawa na kupanda juu angani kisha kuangalia biashara yako kwa chini, na kutathmini kila kinapofanyika. Unapofanya kazi nje ya biashara, hufikirii yale majukumu ya kila siku ya biashara, bali unaangalia kule ambako biashara inakwenda na uwezo wa kufika huko.

Kama unataka biashara yako ikue, lazima uweze kufanya kazi nje ya biashara yako, uweze kuiangalia biashara kama mtu wa pembeni na kupata picha ya pale ilipo sasa na inapoweza kufika.

Hiki ndiyo Gino Wickman anatushirikisha kwenye kitabu chake cha TRACTION; Get A Grip On Your Business. Gino anatupa mwongozo sahihi wa kuendesha biashara zetu, ambao unazingatia nguzo kuu sita, tukiweza kujenga vizuri nguzo hizo sita, tutaweza kuendesha biashara zetu kwa uhuru mkubwa na kuacha kuendeshwa na biashara.

Lakini kabla hatujaingia kwenye nguzo hizo sita, Gino anatupa changamoto tano kubwa ambazo zinaikabili kila aina ya biashara.

CHANGAMOTO TANO ZINAZOKABILI KILA AINA YA BIASHARA.

Zipo changamoto kubwa tano ambazo zinakabili kila aina ya biashara, changamoto hizi tano ndiyo zinapelekea biashara nyingi kufa na hata zinazopona kushindwa kukua zaidi.

Moja; kukosa udhibiti. Huna udhibiti wa kutosha kwenye muda wako, soko na hata biashara yako. Badala ya kuiendesha biashara, biashara inakuendesha wewe.

Mbili; watu. Unavurugwa na wafanyakazi, wateja, wabia na hata wanaokusambazia huduma mbalimbali. Watu hao hawaonekani kukuelewa na wala hawazingatii yale unayowataka wazingatie.

Tatu; faida. Faida unayopata haitoshi kuendesha biashara.

Nne; ukomo. Ukuaji wa biashara yako umefika ukomo, kila ukikazana kuweka juhudi zaidi hakuna ukuaji unaopatikana, unajikuta unachoka zaidi lakini hakuna cha tofauti unachopata.

Tano; hakuna kinachofanya kazi. Umeshajaribu mbinu mbalimbali za kuiwezesha biashara yako kukua na watu kukuelewa, lakini hakuna hata moja ambayo imeleta matokeo mazuri. Unaelekea kukata tamaa na kuona labda biashara siyo bahati yako.

Changamoto hizi tano zinaikabili kila aina ya biashara, lakini habari njema ni kwamba, changamoto hizi siyo mwisho wa biashara, unaweza kuzivuka na kuiwezesha biashara yako kukua zaidi kama utazingatia nguzo sita muhimu za ukuaji wa biashara yako.

Lakini kabla hatujaingia kwenye nguzo hizo sita za kuzingatia, kuna kitu kimoja muhimu unapaswa kukifanyia kazi, ambacho ni kuachilia kile ulichoshikilia sasa.

HATUA YA KWANZA YA KUFANIKIWA KWENYE BIASHARA; ACHILIA ULICHOSHIKILIA.

Gino anatupa mfano wa kufanikiwa kwenye biashara kama mtu ambaye amedondoka kwenye mti mrefu, lakini kwenye kushuka akajishika kwenye tawi, ambapo juu ni mbali na chini ni mbali. Anapiga kelele za msaada, akiuliza kama kuna mtu yeyote wa kumsaidia. Sauti inatoka chini na kumwambia jiachie nitakudaka, anaangalia chini kwa kuwa ni mbali haoni mtu, anaogopa kujiachilia na kuendelea kushikilia tawi.

Kila biashara ambayo haikui, kuna tawi ambalo mmiliki wa biashara hiyo amelishikilia na hathubutu kuliachilia. Tawi hilo ni kile ambacho amezoea kufanya, kile ambacho ana uhakika nacho, lakini siyo bora kwake.

Biashara yako haiwezi kukua kama huwezi kuchukua hatua ambazo zinaonekana ni hatari na zisizokuwa na uhakika. Kama utaendelea kufanya yale ambayo umezoea kufanya, utaendelea kupata matokeo ambayo umekuwa unapata.

Hivyo beba hili kwenye akili yako, ili kukuza zaidi biashara yako, kuna kitu ulichoshikilia sasa ambacho unapaswa kukiachia. Inawezekana ni maono na malengo ambayo hayakufai tena, inawezekana ni wafanyakazi ambao hawazalishi kwa ufanisi mkubwa, inawezekana ni aina ya biashara unayofanya, inawezekana ni wateja unaowahudumia au mfumo wako mzima wa kuendesha biashara.

Lazima uwe tayari kubadili yale ambayo unaendesha kwa mazoea kama unataka kukua zaidi kwenye biashara yako. Hilo tawi uliloshikilia sasa ndiyo linakuzuia usikue zaidi. Achilia tawi hilo, na amini utatua kwenye mikono salama, hasa kama utafuata nguzo sita za kukuza biashara yako ambazo tunakwenda kujifunza hapa.

NGUZO SITA ZA KUIKUZA BIASHARA YAKO; MFUMO WA KIJASIRIMALI WA KUENDESHA BIASHARA.

Gino anatuambia kwamba, kompyuta hauwezi kufanya kazi kama hakuna mfumo wa uendeshaji ndani yake. Kadhalika biashara zetu haziwezi kwenda vizuri kama hatuna mfumo wa kuziendesha.

Kwenye kitabu chake anatushirikisha mfumo anaouita ENTREPRENEURIAL OPERATING SYSYTEM (EOS). Huu ni mfumo wa kijasiriamali wa kuendesha biashara yako, ambao unazingatia nguzo sita muhimu, ambazo ukiweza kuzibobea hizo, utaweza kujenga biashara yenye mafanikio makubwa na inayokupa uhuru wa kutosha.

Zifuatazo ni nguzo sita za kuzingatia katika kutengeneza mfumo bora wa kuendesha biashara yako.

NGUZO YA KWANZA; MAONO.

Maono ndiyo nguzo ya kwanza na muhimu sana kwenye ukuaji wa biashara yako. Biashara nyingi ninakufa au kushindwa kukua kwa sababu hazina maono, au kama yapo basi hayajulikani na kila aliyepo kwenye biashara hiyo.

Maono ya biashara yanaieleza biashara inahusu nini, inaendeshwa kwa misingi gani, inategemea kuwa wapi miaka kumi ijayo na pia inaendeshwaje.

Hiki ni kitu ambacho kinapaswa kuwa kwenye maandishi na siyo kuwa kwenye mawazo ya mtu mmoja.

Lazima maono haya yaandikwe kwa mpangilio sahihi na rahisi, na kila anayefanya kazi kwenye biashara yako anapaswa kuyaelewa maono hayo na kujua kile anachofanya kinachangiaje kufikia maono makubwa ya biashara hiyo.

Kwenye makala ya juma, kipengele cha tatu hapo juu zipo hatua nane za kujenga biashara yenye maono makubwa. Isome makala hiyo na fanyia kazi hatua hizo nane ili kuweka maono yako kwenye maandishi na yaweze kueleweka na watu wote.

Kusudi lako kubwa kama kiongozi wa biashara yako ni kuiongoza biashara hiyo na watu wote waliopo kwenye uelekeo sahihi ambao ni ndoto kubwa za miaka kumi ijayo. Kusimamia misingi ya maadili inayoendesha biashara hiyo na kupata watu sahihi wa kuendelea kufanya nao kazi.

Pia kwa kuwa na maono utaepuka kukimbizana na kila fursa mpya zinazojitokeza, ambazo zimekuwa kifo cha biashara nyingi. Kwa kuchagua wapi unataka kufika na biashara yako miaka 10 ijayo, unaachana kabisa na fursa nyingine zinazoonekana nzuri na za kuvutia, lakini haziendani na lengo lako kuu.

Baada ya kuwa umeweka maono makubwa ya biashara yako, ishirikishe timu yako katika kuweka mipango ya kufikia maono hayo. Mipango hiyo inajumuisha malengo ya miaka mitatu, mipango ya mwaka mmoja, mikakati ya miezi mitatu na hatua za kuchukua kila wiki.

Kila kinachofanyika kwenye biashara yako lazima kiendane na ndoto yako kubwa kwenye biashara hiyo. Kila anayefanya kazi kwenye biashara yako lazima ajue majukumu yake yanachangiaje kufikia maono makubwa ya biashara hiyo. Bila ya kufikia hatua hii kwenye maono, biashara yako haiwezi kufanikiwa.

NGUZO YA PILI; WATU.

Ili biashara yako ifanikiwe, inahitaji sana watu wengine. Na watu muhimu sana kwenye biashara yako, ambao tunawaita wateja wa kwanza ni wale unaowaajiri kwenye biashara hiyo. Watu hawa ndiyo wenye nguvu ya kukuza au kuua biashara yako.

Unapaswa kuajiri watu sahihi na kuwapa majukumu sahihi kwenye biashara yako ili uweze kupiga hatua. Lakini wafanyabiashara wengi wamekuwa wanashindwa kunufaika na watu wanaowaajiri kwa sababu ya vyanzo viwili vikubwa vya matatizo katika kuajiri. Tutajadili vyanzo hivi hapo chini.

VYANZO VIKUU VIWILI VYA MATATIZO KWENYE KUAJIRI.

Kuna vyanzo vikuu viwili vya matatizo inapokuja kwenye kuajiri.

Vyanzo hivyo ni watu na nafasi. Watu hapa ni zile sifa na tabia za mtu unayemwajiri na nafasi ni ile kazi ambayo mtu anayeajiriwa kwenda kufanya.

Katika vyanzo hivi viwili, tunaweza kupata makundi manne katika kuajiri;

MOJA; WATU SAHIHI KWENYE NAFASI SAHIHI.

Hapa unakuwa na watu sahihi kwenye biashara yako, ambao wana sifa nzuri na tabia njema, wanaoendana na misingi yako ya maadili ya biashara yako na wanafurahia kazi wanayoifanya na hivyo kujituma zaidi. Watu hawa wanakuwa kwenye majukumu ambayo yanatumia vipaji na uwezo wa kipekee uliopo ndani yao, hivyo wanakuwana ufanisi mkubwa kwenye kazi zao.

Hii ndiyo ndoto ya kila mfanyabiashara, kupata watu sahihi na kuwaweka kwenye nafasi sahihi. Lakini kufikia hili lazima kwanza utengeneze nafasi hizo kwenye biashara yako, kisha kuweza kuwachuja watu kabla hujawaweka kwenye nafasi hizo, kitu ambacho tutajifunza hapa.

MBILI; WATU SAHIHI KWENYE NAFASI AMBAZO SIYO SAHIHI.

Hapa unakuwa na mfanyakazi ambaye ana sifa na tabia njema, na anaielewa na kuendana na biashara yako. Lakini nafasi uliyompangia kufanya kazi haiendani na vipaji au uwezo mkubwa uliopo ndani yake. Unakuta mtu ni mzuri sana kwenye mauzo au kuongea na watu, lakini anapewa kazi ya stoo au upangaji wa vitu. Mtu huyu licha ya kuwa sahihi, nafasi aliyopo haitumii kilichopo ndani yake na hivyo hawi na msukumo mkubwa kwenye kazi yake.

Hatua sahihi ya kuchukua hapa ni kumjua vizuri mtu, kulingana na vigezo vya kuchuja utakavyojifunza, kisha kumweka kwenye nafasi sahihi kama ipo kwenye biashara yako. Na kama nafsi hiyo haipo basi unaweza kuitengeneza na kama haiwezekani kutengeneza basi ni bora kumwondoa kwenye biashara yako kwa sababu kuendelea kuwepo kutakuwa mzingo kwako na kwake pia.

TATU; WATU WASIO SAHIHI KWENYE NAFASI SAHIHI.

Hapa unakuwa na mtu ambaye siyo sahihi, mtu ambaye hana tabia njema na haendani kabisa na biashara yako. Lakini mtu huyu anakuwa kwenye nafasi sahihi, yaani anafanya kazi vizuri na kuleta matokeo bora. mfano unakuwa na mtu wa masoko ambaye anakuletea wateja wengi sana, lakini kumbe anatumia mbinu za kudanganya kuleta wateja hao. Japokuwa analeta matokeo mazuri, lakini anakuwa siyo mtu sahihi, kwa sababu madhara makubwa yatatokea kwenye biashara.

Wafanyabiashara wengi wanapokuwa na mtu wa aina hii huona hakuna tatizo, kwa kuwa wanaleta matokeo basi tabia zao haziwahusu. Lakini wanasahau kwamba uwepo wa tabia hizo una madhara makubwa kwenye biashara zao, hasa kwa baadaye.

Unapokuwa na watu wasio sahihi kwenye nafasi sahihi za biashara yako maana yake hujatumia vizuri vigezo vya kuwachuja wafanyakazi kabla hujawaajiri. Hivyo unachoweza kufanya ni kuwapa misingi ya maadili ya biashara yako ambayo kila mtu anapaswa kuifuata. Kama watashindwa kufuata misingi hiyo basi itabidi uwaondoe kwenye biashara.

NNE; WATU WASIO SAHIHI KWENYE NAFASI ZISIZO SAHIHI.

Kwa kifupi hapa ni janga, unakuwa na watu ambao hawana tabia wala sifa njema, na pia kazi wanayoifanya siyo bora.

Kitu pekee cha kufanya kwa watu wa aina hii ni kuwaondoa kwenye biashara yako, huna namna ya kuwasaidia watu wa aina hiyo. Na maamuzi haya unapaswa kuyachukua haraka na mara moja, kwa sababu kadiri unavyowachelewesha ndivyo wanavyoleta madhara kwenye biashara yako.

Ili kunufaika na watu unaowaajiri kwenye biashara yako, kwanza tengeneza nafasi za watu kwenye biashara yako, hapa ni yale majukumu ambayo unayemwajiri anapaswa kuyatekeleza. Baada ya kuwa na nafasi sasa chuja wafanyakazi unaotaka kuwaajiri kuona kama wanafaa kwenye nafasi unazotaka kuwaajiri.

Kwenye #MAKINIKIA nitakushirikisha vigezo nane vya kuchuja watu unaowaajiri ili kuweza kupata wafanyakazi bora kwa biashara yako.

NGUZO YA TATU; NAMBA MUHIMU.

Mafanikio au kushindwa kwa biashara yako kupo kwenye namba chache muhimu sana zinazopima biashara hiyo. Kama hutazijua na kuzifuatilia namba hizi kwa karibu, biashara yako haiwezi kukua.

Ni jambo la kushangaza lakini wapo wafanyabiashara ambao wanaendesha biashara zao bila ya kujua namba zao. Wao wanachojua ni kununua na kuuza tu, hela zikiwa nyingi wanajua mambo mazuri, zikiwa chache wanaona kuna tatizo.

Zipo namba nyingi muhimu za kufuatilia kwenye biashara ukiacha mauzo na mapato pekee. Unapaswa kupima kila kinachofanyiwa kazi kwenye biashara yako, kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza kuboresha kile kinachofanyika kwenye biashara.

Baadhi ya namba muhimu za kufuatilia kwenye biashara yako ni hizi zifuatazo;

  1. Mtaji unaozunguka.
  2. Manunuzi yanayofanyika.
  3. Mauzo yanayofanyika.
  4. Gharama za kuendesha biashara.
  5. Idadi ya wateja wanaohudumiwa.
  6. Idadi ya wateja wapya waliofikiwa na njia mbalimbali za masoko.
  7. Kiasi cha wateja tarajiwa waliokuwa wateja kamili kwa kununua.
  8. Malalamiko ya wateja.
  9. Madeni ambayo biashara inadai.
  10. Mikopo ambayo biashara inadaiwa.

Hizo ni baadhi ya namba muhimu, lakini unaweza kuweka namba nyingine kulingana na aina ya biashara unayofanya. Mfano kama biashara inazalisha basi lazima namba za uzalishaji zifuatiliwe.

Namba hizo zinapaswa kufuatiliwa kila siku, kila wiki, kila mwezi, kila robo mwaka na kila mwaka. Wafanyabiashara wengi husubiri mpaka mwisho wa mwaka wanapofanya mahesabu ndiyo wapate namba zinaendaje, lakini mwaka kufika mwisho wa mwaka wanakuwa wameshachelewa, hakuna hatua wanaweza kuchukua. Lakini unapokuwa na namba unazofuatilia kila wiki, ni rahisi kuchukua hatua pale mambo yanapokwenda tofauti.

Zijue namba muhimu kwenye biashara yako na zifuatilie kwa ukaribu sana kila wiki na kufanya maamuzi kulingana na namba hizo zilivyo. Pia kila mtu uliyemwajiri kwenye biashara yako, hakikisha kuna namba anayofanyia kazi, ambayo utapima ufanisi wake kwa namba hizo. Kama mtu hana namba, huwezi kujua kama anapiga hatua au la.

NGUZO YA NNE; CHANGAMOTO.

Kila biashara ina changamoto mbalimbali zinazoikumba, na kadiri biashara inavyokua, ndivyo changamoto zinakuwa kubwa pia.

Wafanyabiashara wengi wamekuwa hawapendi kukutana na changamoto kwenye biashara zao na hivyo wamekuwa wanazikwepa changamoto wanapokutana nazo. Kitu wasichojua ni kwamba, kwa kuzikwepa changamoto siyo kwamba umeziepuka, bali umezipa nafasi ya kukua zaidi. Kadiri changamoto inavyochelewa kutatuliwa ndiyo inakuwa kubwa na kuleta madhara zaidi.

Kitu kinachowafanya wafanyabiashara wengi kukwepa changamoto ni kuogopa kufanya maamuzi magumu na sahihi. Changamoto nyingi zinahitaji kufanyiwa maamuzi ambayo ni magumu na yenye kuumiza kwa upande mmoja au mwingine. Mfano kuna mfanyakazi anaonekana hawezi kutimiza majukumu yake vizuri, lakini ni mfanyakazi ambaye amekuwepo kwenye biashara hiyo kwa muda mrefu, inakuwa vigumu sana kwa uongozi kufikia hatua ya kumwondoa, hivyo tatizo linaenda likifunikwa mpaka inafika hatua kwamba halifunikiki tena.

Zipo hatua tatu muhimu katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili biashara.

Moja ni kutambua changamoto husika. Hapa unaitambua changamoto husika na mzizi mkuu wa changamoto hiyo. Hii ni hatua muhimu kwa sababu changamoto nyingi zinazoonekana huwa ni dalili tu, kunakuwa na tatizo kubwa zaidi ndani.

Mbili ni kujadili. Hapa unapaswa kuwa na majadiliano ya kina kuhusiana na changamoto husika, ukiwahusisha watu wote wanaoguswa na changamoto hiyo. Hapa kila kitu kuhusu changamoto husika kinawekwa wazi na watu kujadiliana bila ya kuogopa au kuoneana aibu.

Tatu ni kutatua. Baada ya majadiliano ya changamoto husika, mnafanya maamuzi juu ya hatua za kuchukua ili kutatua changamoto hiyo. Maamuzi yanayofanywa hapo ndiyo yanayofanyiwa kazi na anapewa mtu mmoja jukumu la utekelezaji, ambaye atatoa taarifa baadaye mambo yanakwendaje. Mwisho kila mtu anaondoka akijua suluhisho ni nini na nani anayesimamia.

Kwa kufuata hatua hizi tatu, hakuna tatizo lolote ambalo litaisumbua biashara yako, na kadiri unavyoweza kuchukua hatua mapema, ndivyo biashara yako inavyokuwa imara.

Mwisho wa siku kwenye kutatua changamoto za biashara utakutana na hali tatu, moja changamoto isiyotatulika na hivyo kuishi nayo, kuichukulia kama ilivyo na kutoruhusu ikusumbue. Mbili changamoto inayofaa kubadili na kuna namna ya kuibadili ikaleta matokeo sahihi, hii unapaswa kuibadili. Na tatu ni changamoto ambayo inatatulika, lakini hata ukiitatua haina manufaa kwenye biashara, hii unapaswa kuifuta au kuiondoa kwenye biashara yako.

Zikabili changamoto kwenye biashara yako kabla hazijaota mizizi na biashara itakuwa imara mara zote.

NGUZO YA TANO; MCHAKATO.

Biashara yenye mafanikio ni ile ambayo mtu anaweza kuchukuliwa kutoka nje ya biashara, akawekwa kwenye biashara hiyo na akawawe kutekeleza majukumu anayopewa. Hii ni biashara ambayo inakuwa na mchakato wa utekelezaji wa majukumu yake, ambao umetengenezwa na unaeleweka.

Kutengeneza mchakato wa utekelezaji wa majukumu ya biashara yako ni hitaji muhimu kama unataka kuwa huru na biashara hiyo. Wafanyabiashara wengi hawana uhuru kwenye biashara zao kwa sababu wao ndiyo kila kitu, hakuna mtu mwingine anayeweza kutekeleza majukumu kama wao hawapo. Hata wanapoajiri watu, wao ndiyo wanawapangia majukumu ya kufanya na jinsi ya kufanya.

Ondokana na hali hiyo kwa kuweka chini mikakati na mchakato wa utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya biashara. Na hii inakuja baada ya kuwa umeshatengeneza nafasi kwenye biashara yako, kisha kuandaa mchakato wa kila nafasi.

Kwa mfano umetengeneza nafasi ya masoko, hapa unaandaa mchakato mzima wa masoko, ambapo mtu anayeajiriwa kwenye kitengo hicho ataufuata. Kuanzia kuwafikia wateja walipo, kupata mawasiliano yao, kuendelea kuwafuatilia kwa mawasiliano na mengine mpaka wanapokuwa wateja kamili. Mchakato huu unapaswa kuwa kwenye maandishi kitu ambacho kinakuwa rahisi kwa yeyote unayempa jukumu hilo kufuata.

Ukishaweka mchakato wa kila kitengo cha biashara yako, watu wote wanaofanya kazi kwenye vitengo hivyo wanapaswa kuufuata kama ulivyo. Hii inakuwa rahisi kwako kuifuatilia biashara hata kama upo mbali, kwa sababu unajua kila mtu anapaswa kufanya nini na namba gani ambazo anapimwa nazo.

Mchakato wa kuendesha biashara yako ni muhimu sana kwa sababu ndiyo utakaokupa uhuru wa biashara yako. Pale kila eneo la biashara yako linaendeshwa kwa mchakato sahihi, biashara yako inageuka kuwa mashine ya kuzalisha fedha, maana mashine yoyote huwa inajiendesha kwa michakato inayoeleweka.

Ukishaiweka biashara yako katika uendeshwaji wa mifumo sahihi, inakupa uhuru ufuatao;

  1. Unaweza kuikuza zaidi bila ya wewe kuwa na majukumu zaidi.
  2. Unaweza kuiacha ijiendeshe yenyewe na wewe kufanya vitu vingine.
  3. Unaweza kuiuza kwa watu wengine.
  4. Unaweza kuwapa watu kibali cha kufungua biashara kama hiyo eneo jingine.
  5. Au unaweza kufungua matawi zaidi kwenye maeneo mengine.

Ukishaweza kuiendesha biashara yako kwa mifumo sahihi, unakuwa umefikia uhuru kamili kwenye biashara na maisha pia.

NGUZO YA SITA; UWAJIBIKAJI.

Nguzo tano tulizojifunza mpaka sasa ni muhimu sana kwa ukuaji wa biashara yako na kuweza kusimama imara. Lakini nguzo zote hizo haziwezi kufanya kazi kama hakuna uwajibikaji.

Uwajibikaji ni kuchukua hatua kwenye yale yote uliyojifunza na kuyatengeneza kwenye biashara, ambapo kila mtu anapimwa kwa kile anachozalisha kwenye biashara yako.

Hili ni eneo ambalo wafanyabiashara wengi huwa linawashinda, kwa sababu hawana mfumo sahihi wa uwajibikaji. Wanaweza kuwa na wafanyakazi wengi, lakini hakuna matokeo ya tofauti wanayofanya. Na hiyo ni kwa sababu watu wanafanya mambo kwa mazoea na hawapimwi kulingana na ufanisi wao.

Ili kuondokana na hali hiyo, ili kila aliyepo kwenye biashara yako aweze kuwa na manufaa kwenye biashara hiyo, lazima uweke mfumo wa uwajibikaji kwa kila mtu.

Uwajibikaji kwenye biashara unaweza kuhimizwa kwa vitu viwili;

Kitu cha kwanza ni kila mtu kuwa na majukumu anayofanyia kazi, ambayo yeye ndiye mhusika mkuu na anayehusika kuhakikisha yametekelezwa kwa kiwango kinachohitajika. Ukishaweka watu wawili kwenye jukumu moja na wote wakawa wahusika wakuu, basi jua jukumu hilo halitafanyiwa kazi. Kila jukumu liwe na mtu mmoja anayeshikiliwa kwa uwajibikaji wake, hata kama kuna wengine wanahusika nalo basi wanakuwa chini yake. Mtu mmoja anapokuwa anahusika na jukumu fulani, atajituma na hali ya kutegeana haitakuwepo. Weka mtu mmoja anayewajibika kwenye kila idara na jukumu la biashara yako.

Kitu cha pili ni mikutano ya kupima hatua ambazo kila mtu anapiga. Mikutano ni kitu ambacho kimekuwa inapigwa vita na wengi kwa sababu inachukua muda mwingi na mingi haina tija. Lakini huwezi kuendesha biashara yako vizuri kama hakuna mikutano. Hivyo unapaswa kuwa na mikutano yenye tija na uzalishaji mkubwa.

Mikutano hii inapaswa kuwa ya aina tatu, mikutano ya kila wiki, mikutano ya kila robo mwaka (kila baada ya miezi mitatu) na mikutano ya kila mwaka. Kila wiki mnakutana kupitia mipango ambayo watu wanafanyia kazi, utekelezaji wake na kuweka mipango mipya kwa wiki inayofuata. Kila robo mwaka pia mnafanya hivyo. Na kila mwaka mnakuwa na mkutano mkubwa ambao unapitia mwaka unaoisha, unaangalia malengo ya miaka 10 ijayo, miaka 3 ijayo na kisha kuweka malengo ya mwaka unaofuata.

Ili kuhakikisha mikutano mnayofanya inakuwa na tija, hasa mikutano ya kila wiki, basi mnapaswa kuzingatia mambo yafuatayo;

  1. Mkutano ufanyike siku ile ile kila wiki, kama ni jumatatu basi kila jumatatu ya kila wiki. Kwa mikutano ya robo mwaka mnaweka kabisa tarehe za mikutano hiyo.
  2. Mikutano ifanyike kwa muda ule ule kila wiki, kama ni saa mbili asubuhi basi kila wiki, jumatatu saa mbili asubuhi ni mkutano, hakuna kitu kingine cha kuingilia hilo.
  3. Ajenda ziwe zile zile ambazo zimechapwa kabisa. Kupitia mipango iliyopita na utekelezaji wake, kujadili changamoto ambazo watu wamekutana nazo na kuzitatua kisha kuweka mipango ya kwenda kufanyia kazi kwa kipindi kinachofuata.
  4. Mikutano yote ianze kwa muda, na kila mtu awahi kama muda unavyofahamika.
  5. Mikutano yote iishi kwa muda uliopangwa.

Kufanya mikutano kwa siku ile ile ya wiki kunafanya mkutano kuwa sehemu ya utaratibu wa biashara. Kuwa na ajenda zile zile kwenye kila mkutano inaepusha kuingia kwenye malumbano yasiyo na tija. Kuanza kwa muda na kumaliza kwa muda kunaongeza nidhamu na mkutano unakwenda haraka na hauchoshi watu ukilinganisha na mikutano inayochelewa kuanza na kuchelewa kuisha pia.

Hizo ndiyo nguzo sita za kuzingatia ili uweze kuikuza zaidi biashara yako na uwe na uhuru mkubwa na maisha yako. Yaweke haya kwenye biashara yako ili uweze kuikuza biashara yako, utoke pale ulipokwama sasa ambapo biashara inakumiliki na uweze kufika hatua ya juu kabisa ambapo unaimiliki biashara.

#3 MAKALA YA JUMA; HATUA NANE ZA KUJENGA BIASHARA YENYE MAONO MAKUBWA.

Kuingia kwenye biashara siyo kitu kigumu kwa zama hizi. Njia za ufanyaji wa biashara zimerahisishwa sana, mtu anaweza kuanza biashara bila hata ya kuwa na eneo la biashara, mtaji au hata bidhaa au huduma. Kwa kutumia mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii, watu wengi wanaweza kuanza biashara kwa urahisi sana.

Lakini biashara nyingi zinazoanzishwa zimekuwa zinakufa muda mfupi baada ya kuanzishwa, hazidumu kwa muda mrefu. Na hata zile biashara ambazo zinadumu kwa muda mrefu, zimekuwa hazikui, zinadumaa, zinabaki kuwa ndogo wakati wote.

Watu wana vitu vingi wanavyoweza kusingizia kwa nini biashara zinakufa au hazikui. Uchumi, serikali, mazingira, watu na hata hali ya hewa ni vitu ambavyo vimekuwa vinabebeshwa sana lawama pale biashara zinapokufa au kutokukua.

Lakini ukweli ni mmoja, biashara zinakufa au kutokukua kwa sababu ya kukosa maono makubwa. Na hata kama biashara ina maono makubwa, basi siyo kila mtu aliyepo kwenye biashara hiyo anayaelewa na kuyaishi maono hayo.

Kama unataka biashara yako isife, iweze kukua zaidi ya pale ilipo sasa, basi unapaswa kuwa na maono makubwa, ambayo kila anayehusika kwenye biashara hiyo anayaelewa na anajua kile anachofanya kinachangiaje kufikia maono hayo. Lazima watu wote kwenye biashara wawe na uelekeo mmoja na hapo ndipo mnaweza kupiga hatua.

Makala ya juma hili, nimekushirikisha hatua nane za kujenga biashara yenye maono makubwa na ambayo itafikia mafanikio makubwa. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo, unaweza kuisoma sasa hapa; Hatua Nane Za Kujenga Biashara Yenye Maono Makubwa Na Itakayokufikisha Kwenye Mafanikio Makubwa.

Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku, kuna makala nzuri za kukuwezesha kupiga hatua zaidi zinazowekwa kila siku.

#4 TUONGEE PESA; PESA KAMA DAMU YA BIASHARA.

Biashara ni kiumbe hai, ambacho kina maisha yake kama sisi viumbe wengine tulivyo na maisha yetu. Biashara inazaliwa, kukua, kuzeeka na hata kufa kama ambavyo sisi viumbe wengine tunaenda kwenye maisha yetu.

Kwa sisi binadamu, hakuna kitu kinaweza kumuua mtu haraka kama kupoteza damu. Kwa kuwa damu ndiyo inabeba uhai wetu, kwa kubeba pumzi na virutubisho na kuvisambaza sehemu mbalimbali za mwili, unapopoteza damu nyingi, sehemu za mwili zinakosa hewa ya oksijeni na virutubisho na hivyo zinakufa.

Biashara kama kiumbe hai nacho kina damu yake, ambayo ikipotea kwa wingi basi biashara inakufa. Na ukiangalia biashara zote ambazo zinakufa, chanzo kikuu ni kupotea kwa damu hiyo ya biashara.

Damu ya biashara ni fedha, mzunguko wa fedha kwenye biashara ni sawa na mzunguko wa damu kwenye miili yetu. Kama mzunguko wa fedha haupo vizuri kwenye biashara, hakuna namna biashara hiyo itapona.

Kama biashara inapoteza fedha, basi biashara hiyo inaelekea kwenye kifo, kama hatua hazitachukuliwa haraka.

Swali ni je unajuaje kama biashara yako inapoteza fedha?

Jibu ni lazima uzijue namba muhimu za biashara yako na kuzifuatilia vizuri kila siku, kila wiki, kila mwezi, kila robo mwaka na kila mwaka.

Namba muhimu sana inapokuja kwenye fedha ni hizi;

  1. Mtaji unaozunguka kwenye biashara kwa kipindi husika.
  2. Manunuzi yaliyofanywa kwenye biashara kwa kipindi husika.
  3. Mauzo yaliyofanyika kwenye biashara kwa kipindi husika.
  4. Gharama za kuendesha biashara hiyo kwa kipindi unachopigia hesabu.
  5. Mali iliyopo kwenye biashara katika kipindi unachopiga hesabu.

Biashara yenye afya na inayokua, mapato ni makubwa kuliko matumizi yote. hapa mapato yanajumuisha mauzo yote na matumizi yanahusisha manunuzi, gharama za mauzo na gharama za kuendesha biashara.

Biashara yenye matatizo na inayoelekea kufa matumizi ni makubwa kuliko mapato. Hii ndiyo biashara ambayo inapoteza damu na haitachukua muda kabla haijafungwa.

Wajibu wako kama mfanyabiashara ni kufuatilia uhai wa biashara yako kwa kuangalia kwa karibu mzunguko wa fedha kwenye biashara yako. Kila unaoona kuna fedha zinapotea chukua hatua haraka kabla mambo hayajawa makubwa na magumu.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; MUHTASARI WA KUFANIKIWA KWENYE BIASHARA.

“In summary, successful businesses operate with a crystal clear vision that is shared by everyone. They have the right people in the right seats. They have a pulse on their operations by watching and managing a handful of numbers on a weekly basis. They identify and solve issues promptly in an open and honest environment. They document their processes and ensure that they are followed by everyone. They establish priorities for each employee and ensure that a high level of trust, communication, and accountability exists on each team.” ― Gino Wickman

Kwa maneno machache tunaweza kujumuisha mafunzo yote ya kitabu hiki kama ifuatavyo; biashara zenye mafanikio zinaendeshwa kwa kuwa na maono makubwa ambayo yanaeleweka na kila mtu, zina watu sahihi katika nafasi sahihi, zinafuatilia kwa karibu namba muhimu za biashara hizo, zinatambua changamoto na kuzitatua mapema, zinatambua mchakato wake na kuuweka kwenye mfumo rahisi kufuatwa na kila mtu, zinaweka kipaumbele cha kila mfanyakazi na kutengeneza mazingira ya uaminifu, uwajibikaji na mawasiliano baina ya timu nzima.

Hivi ndivyo unavyoweza kuijenga biashara yako ikawa na mafanikio makubwa na kukupa wewe uhuru wako, kwa kuwa na MAONO, kuwa na WATU sahihi, kutaua CHANGAMOTO, kuwa na NAMBA muhimu unazofanyia kazi, kuweka vizuri MCHAKATO wa kuendesha biashara hiyo na kuweka UWAJIBIKAJI kwa kila anayehusika na biashara hiyo.

Simamia nguzo hizo sita ulizojifunza kwenye kitabu hiki cha TRACTION na biashara yako itaweza kukua na kukupa uhuru wa maisha yako.

Kwenye #MAKINIKIA ya kitabu hiki tutakwenda kujifunza vigezo nane vya kutumia katika kuwachuja wafanyakazi wa biashara yako ili kupata wafanyakazi bora, tutajifunza hatua za kuchukua ili uweze kunufaika na mfumo huu wa nguzo sita kwenye biashara yako, na mwisho nitakupa vifaa vitano vya msingi unavyopaswa kuwa navyo kwenye biashara yako ili kutumia vizuri mfumo huu kwenye biashara yako.

Karibu sana ujiunge na CHANNEL YA TANO ZA JUMA ili uweze kupata #MAKINIKIA hayo. Kama bado hujajiunga fuata maelekezo hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu