Karibu rafiki yangu mpendwa kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali tunazopitia kwenye maisha na zinazotukwamisha kufanikiwa. Kila mmoja wetu, bila ya kujali ni hatua gani amefikia kwenye maisha, kuna changamoto mbalimbali ambazo anapitia.

Kwa kila changamoto, kuna hatua ambazo mtu unaweza kuchukua na mambo yakawa bora zaidi ya yalivyo sasa. Lakini wewe peke yako ni vigumu kuziona hatua hizi, na hapo ndipo ushauri unaposaidia sana kwenye changamoto, kwa sababu unakupa mtazamo wa tofauti juu ya changamoto yoyote unayopitia.

Leo tunakwenda kupata ushauri kuhusu kusudi la maisha, tunakwenda kuona hatua za kuchukua pale ambapo hujajua kusudi la maisha yako.

jua kusudi.jpg

Kabla hatujaingia kwenye hatua hizo za kuchukua, tupate maoni kutoka kwa msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili;

Changamoto, bado sijapata wazo au kusudi ambalo ni zawadi aliyonipa Mungu, ili niweze kufanyia kazi na nifanikiwe. – Nelson K. M.

Kama ambavyo ametuandikia Nelson hapo juu, kuna wengi ambao wamekwama kwenye kazi au biashara fulani, wanakuwa hawapendi kile wanachofanya, bali wanafanya kwa sababu hawajui wafanye nini.

Hii ni hali mbaya sana kwenye maisha kwa sababu mtu unakuwa na maisha ambayo huyafurahii, na kwa njia hiyo huwezi kuwa na mafanikio kwenye maisha yako.

Hapa nakwenda kukushirikisha hatua tatu unazoweza kuchukua kama mpaka sasa hujalijua kusudi la maisha yako. Kwa kuchukua hatua hizi tatu, utaweza kuwa na maisha bora, utaweza kufanya makubwa, hata kama bado hujajua kusudi la maisha yako.

Moja; fanya kile ambacho unaweza kukifanya vizuri.

Kila mtu kuna kitu ambacho anaweza kukifanya vizuri kuliko wengine. Kuna kitu ambacho wengine wakiwa na uhitaji fulani wanakuja kwako kwa sababu wanajua unakifanya vizuri. Kuna kitu ambacho wewe unaweza kukifanya kawaida, lakini wengine wakashangaa sana umewezaje kukifanya. Kuna kitu ambacho unapokifanya wengine wanakusifia sana.

Hapo ndipo unapopaswa kuanzia sasa, anza kwa kukifanya kitu hicho.

Angalia kile ambacho uko vizuri kwenye kukifanya, na kifanye hicho kwa wingi uwezavyo. Na siyo lazima kiwe kitu ambacho unapenda kukifanya, muhimu ni kiwe kitu ambacho unaweza kukifanya vizuri na kukifanya kweli.

Mbili; toa thamani kubwa kwa wengine.

Kupitia kile ambacho unaweza kukifanya vizuri, angalia ni kwa namna gani unaweza kutoa thamani kubwa kwa wengine. Angalia wengine wana uhitaji gani mkubwa kwenye maisha yao, wana changamoto zipi ambazo unaweza kuwasaidia kuzitatua kupitia kile unachoweza kufanya.

Lengo lako la kwanza kwenye kufanya chochote, linapaswa kuwa kuwasaidia wengine, kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi ya yalivyo sasa.

Kila wakati jiulize ni kwa namna gani kile unachofanya kinaweza kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi, kisha fanya hivyo. Nenda hatua ya ziada katika kuhakikisha maisha ya wengine yanakuwa bora kupitia kile unachofanya.

Unapozalisha matokeo bora kwa wengine, na wao wanakuwa tayari kukulipa wewe. Na haiishii hapo kwenye kulipwa, bali utajisikia vizuri pia na kuyafurahia maisha yako.

Tatu; chukua hatua kulijua kusudi la maisha yako.

Hatua ya tatu ni wewe kuchukua hatua ya kulijua kusudi la maisha yako. Hakuna siku kusudi la maisha yako litakutokea ndotoni au ukapata ufunuo kwamba wewe umekuja hapa duniani kufanya kitu fulani.

Hakuna mtu yeyote anayeweza kukuambia kusudi lako ni lipi, hata wazazi na wale wa karibu, hawawezi kujua kusudi lako. Wao wanaweza kukuambia uko vizuri kwenye vitu gani.

Lakini kile hasa ambacho ndiyo kusudi lako, utaweza kukijua mwenyewe na utakijua kwa kupata muda wa kujitafakari na kuyatafakari maisha yako.

Kuna makala nzuri ya kukusaidia kulijua kusudi la maisha yako, isome sasa hapa; UCHAMBUZI WA KITABU; NOBLE PURPOSE (Furaha Ya Kuishi Maisha Yenye Maana.)

Rafiki, usikubali kutokulijua kusudi la maisha yako kuwe kikwazo kwako kuchukua hatua. Popote ulipo sasa, una mengi ya kuanza kufanya, ukawanufaisha wengine na ukajinufaisha na wewe pia. Hebu anza kuchukua hatua leo, kupitia kile unachoweza kufanya huku ukiangalia ni jinsi gani unaongeza thamani zaidi kwa wengine.

Kama hujasoma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, unajichelewesha kufika kwenye uhuru wa kifedha na utajiri. Kipate leo na uweze kushika hatamu ya maisha yako. Piga simu au tuma ujumbe kwenye namba 0678 977 007 na utatumiwa au kuletewa kitabu popote ulipo Tanzania.

elimu fedha 2

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog