Naamini umewahi kusikia ushauri huu, unaweza kupata chochote kile unachotaka kwenye maisha yako, au kuwa yeyote yule unayetaka kuwa. Ukaambiwa kwa hamasa kubwa na kuamini kwamba hilo linawezekana.
Ni kweli kabisa kwamba linawezekana, ila halitawezekana kama utaendelea kuishi kama unavyoishi sasa.
Ili kupata unachotaka, unahitaji kuishi tofauti kabisa na unavyoishi sasa, na baadhi ya mambo unayopaswa kuyafanya tofauti ni haya;
Moja; jua kwa hakika ni nini unachotaka, usilete siasa, nenda moja kwa moja kwenye nini unataka.
Mbili; acha kufanya vitu ambavyo havichangii wewe kufika kule unakotaka kufika. Kama kitu hakikupeleki unakotaka kufika huo ni usumbufu kwako, achana nao.
Tatu; lenga lengo lako, macho yako yote yawe kwenye kile unachotaka na vingine vyote achana navyo. Kwa sababu kuna vingi vizuri vitapita mbele yako, lakini havikufikishi unakotaka, achana navyo.
Nne; weka kazi, kazana kuwa bora kila wakati. Hakuna mtu anayeanza akiwa anajua kila kitu, akiwa tayari kwa kila kitu. Kila mtu anaanzia chini na kukua kadiri anavyokwenda, kuwa tayari kuanzia chini na kukua kadiri unavyokwenda.
Ukifuata mambo hayo manne, utakuwa na maisha ya tofauti kabisa, na hutabaki hapo ulipo sasa, hata kama hutafika kule ulikotaka kufika, lakini utafika juu zaidi ya pale ulipo sasa.
Hakuna chochote katika hayo manne kinahitaji uwe na elimu kubwa, fedha nyingi au koneksheni na watu fulani, yote yanaanza na wewe mwenyewe, hivyo anza kuyafanyia kazi sasa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kweli kocha kuna meng lazima nibadilike ili kufika kule napotakiwa kufika kuna mambo s ya kukumbatia yanarudisha nyuma sana
LikeLike
Vizuri Hendry,
Chukua hatua.
LikeLike