Sisi binadamu tunasukumwa na hisia kuu za aina mbili; hisia chanya na hisia hasi.

Hisia hasi ni hasira, wivu, aibu, kutojiamini, tamaa na hatia. Hizi ni hisia ambazo zinakubomoa na kuwa kikwazo kwako kuyafurahia maisha yako, bila ya kujali umepiga hatua kiasi gani.

Hisia chanya ni  kujiamini, unyenyekevu, ujasiri, shukrani na upendo. Hizi ni hisia ambazo zinakujenga na kukuwezesha kuyafurahia maisha yako, bila ya kujali uko katika hali gani.

Sasa, hisia hizi kuu za aina mbili zina mizizi yake, ambayo ukiielewa, hazitakusumbua tena.

Mzizi wa hisia hasi ni HOFU. Hofu ndiyo inakufanya uwe na hisia hasi, uone kwamba hustahili au wengine ni zaidi yako. Hofu ikikutawala, hisia hasi zinakuwa na nguvu kubwa kwako.

Mzizi wa hisia chanya ni IMANI. Imani inakufanya uwe na hisia chanya, uone kila unachokutana nacho ni sahihi kwako na ni wajibu wako kukitumia kupata matokeo mazuri zaidi.

Hivyo ukiangalia mizizi hii miwili, ni rahisi kuona jinsi inavyojengeka ndani yetu, na hivyo tunapotaka kubadili, tunajua wapi pa kuchukua hatua.

Hofu huwa inaanza na mashaka, baadaye yanapelekea kwenye wasiwasi na baada ya hapo mtu anajikuta hawezi kabisa kuchukua hatua, hofu inakuwa imetawala. Hivyo kama hutaki hofu ikuingie, hakikisha kila unapokuwa na mashaka na kitu, unapata ufumbuzi wake haraka kabla hujaenda kwenye wasiwasi na baadaye hofu.

Imani huwa inaanza na matumaini ambayo yanakua na kukupelekea kujiamini na kuamini kila kinachoendelea. Hivyo kama unataka kujijengea imani ili uwe na hisia chanya, anza na matumaini. Na uzuri ni kwamba, kwenye kila jambo, kuna kitu cha kukupa matumaini, ni wewe kukiona na kukitumia.

Chagua, hofu au imani, una nguvu ya kuchagua kipi unataka, itumie vizuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha