Mpendwa rafiki yangu,
Zipo sifa nyingi sana za uongozi lakini kama kiongozi umekosa sifa ambayo tunakwenda kuijua siku hii ya leo utakua siyo kiongozi sahihi.
Kila mmoja anatakiwa kuishi kama kiongozi, fanya maamuzi kama kiongozi kwa kutumia akili na wala siyo hisia.
Ukiwa ni mtu wa kutumia hisia, utaweza kufanya mabaya amabyo hata hukuyatarajia kutokea katika maisha yako. Lakini ukitumia hekima, mambo mengi yataenda vizuri sana.
Hakuna sehemu ambayo mambo yataweza kwenda vizuri kila siku. Katika uongozi kuna nyakati tofauti, hivyo ukiwa kama kiongozi unapaswa kujua hilo kuwa mambo huwa yanaenda ndivyo sivyo wakati mwingine.
Leo tunakwenda kujifunza sifa ya ziada anayopaswa kuwa nayo kiongozi. Na sifa ya ziada anayopaswa kuwa nayo kiongozi ni tabia ya kufanya kazi zaidi ya wengine.
Shida nyingi zinatokea katika maeneo ya kazi kama kiongozi ameshindwa kufanya kazi yake kwa umakini. Mtu anafikiria kuwa akishakuwa kiongozi basi anatakiwa asifanye kazi sana na wale anao waongoza ndiyo wafanye kazi sana.
Ukiwa kiongozi halafu huna sifa ya kazi unapoteza ladha. Kiongozi usiwe mvivu na unatakiwa kufanya kazi zaidia ya wengine. Unatakiwa kwenda hatua ya ziada, usifike kwa kazi na siyo kutumia muda mwingi kupiga hadithi.
Kiongozi ukiwa mtu wa kazi hata wale wanaokusimamia nao watakua watu wa kazi. Huwa tunapenda kufanya kwa vitendo, tukiona kiongozi wetu anafanya na sisi huwa tuna hamasika kufanya pia.
Ondoa falsafa hii katika uongozi, ambayo ni kutumikiwa badala ya kutumika. Uko katika uongozi kwa ajili ya kutumika na siyo kutumikiwa. Viongozi wengi wanaingia na gia ya kutumikiwa ndiyo maana wanashindwa kutekeleza wajibu wao vizuri.
Kila mmoja wetu ni kiongozi wa maisha yake, hivyo basi kila mtu anatakiwa kwenda hatua ya ziada katika nafasi aliyopo ili aweze kwenda na kasi ya uongozi bora.
Hatua ya kuchukua leo; Sifa ya kiongozi ni kufanya kazi zaidi ya mtu mwingine.
Kwa kuwa wewe ni kiongozi nakusihi sana leo nenda kafanye kazi zaidi ya mtu mwingine.
Kwahiyo, ingia na gia ya kutumika na siyo kutumikiwa na utakuwa kiongozi bora sana.
Kiongozi ni kazi hivyo nenda kafanye kazi kama asili ya mwanadamu. Nenda kawe sehemu salama na watu wakikuona waseme kweli fulani ni kiongozi na siyo kusemwa kwa sifa mbaya.
Kila la heri rafiki yangu.
Makala hii imeandikwa na;
Mwl. Deogratius Kessy ambaye ni mwalimu, mwandishi na mjasiriamali.
Unaweza kuwasiliana naye au kutembelea tovuti yake kwa kutumia anuani zifuatazo.
Mwl. Deogratius Kessy
0717101505//0767101504
deokessy.dk@gmail.com
kessy@ustoa.or.tz na tovuti yake
http://kessydeo.home.blog
Karibu sana na
Asante sana.