Zipo changamoto nyingi ambazo wengi wamekuwa wanakutana nazo wakati wa kufanya maamuzi na hizo kuwa kikwazo kwao kupiga hatua kwenye maisha yao.
Kuna changamoto ya kuwahi kufanya maamuzi, hasa pale mtu anapokuwa anaendeshwa na hisia kali za furaha au hasira. Aina hii ya maamuzi huwa siyo sahihi na baadaye huwa na madhara.
Kuna changamoto ya kuchelewa kufanya maamuzi, kwa kuwa hali haieleweki vizuri, mtu anachukua muda mrefu kufikia maamuzi. Anapokuja kufikia maamuzi anakuwa ameshachelewa na hivyo hayamnufaishi tena.
Kuna changamoto ya kuachana na maamuzi haraka pale ambapo hayaleti matokeo ambayo mtu alikuwa anategemea. Hata kama juhudi hazijakomaa, mtu anaacha na kuona haiwezekani.
Kuna changamoto ya mtu kuchelewa kuachana na maamuzi licha ya muda na gharama kuwa kubwa huku matokeo yakiwa hayawezekani. Kadiri mtu anavyokuwa ameweka muda na gharama kubwa, ndivyo anaendelea kukomaa na maamuzi yake kwa sababu hataki kupoteza kile ambacho amewekeza.
Kutokana na changamoto hizi, ufanyaji wa maamuzi umekuwa ni kitendawili kwa sababu inabidi usiwahi wala kuchelewa sana kuyafanya na usiwahi au kuchelewa kuyavunja. Hivyo unapaswa kujua ni mlinganyo upi sahihi. Na mlinganyo sahihi unatofautiana kulingana na uzito wa maamuzi.
Msingi mzuri wa kufuata ni huu;
Kwenye kufanya maamuzi, jipe muda wa kupata taarifa za kutosha, ukiangalia upande chanya na upande hasi kabla hujafanya maamuzi. Lakini jiwekee ukomo ili usitumie muda mrefu zaidi.
Kwenye kuvunja maamuzi, panga muda na gharama ambazo unategemea kuwekeza kwenye maamuzi unayofikia, kisha weka kiwango cha juu ambacho hutavuka zaidi ya hapo kama matokeo yatakuwa hayajaanza kuonekana. Kisha fanya na ukishafikia ukomo, vunja maamuzi hayo, kama hujafikia, endelea kuweka juhudi.
Lakini kabla hujavunja maamuzi, hakikisha umefanya kila kinachopaswa kufanyika, umeweka juhudi kubwa na umegusa kila eneo. Kama imeshindikana iwe ni kwa sababu ambazo ziko kabisa nje ya uwezo wa kibinadamu (siyo nje ya uwezo wako tu) na hivyo huna la kufanya.
Kufanya maamuzi haijawahi kuwa rahisi, hasa kwa mambo magumu na mazito, mwongozo huu utakusaidia kufanya maamuzi kwa usahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante kocha makala hii nzuri kwangu, na imekuja kwa wakati has a ukizingatia naendelea kufanyia kazi maamuzi yangu ya kubadili biashara.
LikeLike
Vizuri Tumaini.
LikeLike
Hakika Kocha Dr. Amani, Ili swala sikuwai kupata shule mahali popote pale ninaweza kusema hivi sababu kwa wiki tatu mbili hapo nilikutana na swala la kuniitaji nifanye maamuzi sahihi na usiyo nifanya baadaye nijutie, japo kweli kwa hatua nilizoweza kuchukua ni sawa kabisa na hatua yako ya pili la Kwenye kufanya maamuzi, la kujipa muda wa kupata taarifa za kutosha, ukiangalia upande chanya na upande hasi kabla hujafanya maamuzi. Lakini pia kujiwekea ukomo ili usitumie muda mrefu zaidi. Na hapa ndipo naweza kutoa ushuhuda nilifikiri vyema na sahihi kama ulivyoweza kusema pia na wewe. Ahsante kwa Maarifa zaidi.🤝💪
LikeLike
Vizuri, umeshayapata maarifa, yatumie kufanya maamuzi sahihi.
Kila la kheri.
LikeLike