Wakati bora kabisa wa kupanda mti ulikuwa miaka 20 iliyopita, wakati mwingine bora ni sasa. Hii ni kauli maarufu ya Wachina wa kale ambayo wengi siyo tu wamekuwa hawaielewi, ila pia hawaiweki kwenye matendo.

Tarehe 10/10/2014 kwenye mtandao wa AMKA MTANZANIA, niliandika makala iliyoitwa Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja. Kwenye makala hiyo nilieleza jinsi mtu unavyoweza kuanza kujenga utajiri wako kwa kuanza na kiasi kidogo sana cha shilingi elfu moja tu kwa siku.

Kwenye makala hiyo pia nilishirikisha kuhusu mfumo mzuri wa uwekezaji, ambao ni rahisi kufanya, kwa kuanza na kiasi kidogo cha fedha na kuwekeza mara kwa mara na baadaye uwekezaji wako kukua na kukupa faida zaidi. Mfumo huo ni kupitia mfuko wa uwekezaji wa pamoja unaojulikana kama UTT.

Sasa turudi kwenye kauli ya wakati mzuri wa kupanda mti. Kama ulielewa na kufuata ushauri niliotoa kuhusu uwekezaji huo, tarehe 12/10/2014 kipande kimoja cha mfuko wa umoja kilikuwa kinauzwa tsh 464. Tarehe 01/10/2020 kipande kimoja cha mfuko huo huo wa umoja kinauzwa kwa tsh 646. Hili ni ongezeko la tsh 182 kwa kila kipande au asilimia 40 kwa miaka 6. Hili ni ongezeko la juu kabisa ambalo huwezi kulipata kwenye uwekezaji mwingine wowote.

Lakini kwa kuangalia ongezeko la kipande kimoja au asilimia huwezi kuona picha nzuri, wacha nikupe mfano halisi.

Tarehe 12/10/2020 mimi binafsi nilinunua vipande vya tsh 700,000 (picha nimeambatanisha) ambapo kwa bei ya siku hiyo nilipata vipande 1508. Kwa vipande hivyo hivyo, tarehe 01/10/2020 thamani yake inakuwa tsh 974,168 ambayo inakupa ongezeko la tsh 274,168.

Fikiria hiyo ni karibu laki 3 ambayo mtu unaipata kwa kuwekeza laki 7 halafu kusahau na kuendelea na mambo yako. Kwa kuwekeza kwenye mfumo huo huhitaji kufuatilia chochote, husumbuki na chochote, wewe unaendelea tu na mambo yako mengine huku uwekezaji wako ukiongezeka thamani. Ni raha iliyoje?

Nikirudi kwenye sehemu ya pili ya usemi, kwamba wakati mwingine mzuri ni sasa.

Kama hukupata makala ya mwaka 2014 au uliipata na kupuuza, basi leo una nafasi nyingine ya kujifunza na kuchukua hatua.

Klabu ya KISIMA CHA MAARIFA ya mkoa wa Arusha, kwa kushirikiana na UTT wameandaa mafunzo ya uwekezaji yatakayofanyika siku ya jumapili, tarehe 04/10/2020 jijini Arusha.

Mafunzo haya ni maalumu kwa wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, ila kwa kuwa nakupenda sana wewe rafiki yangu, nimemuomba mwenyekiti wa Klabu ya Arusha aruhusu wasio wanachama nao kuhudhuria na kujifunza, kwa sababu sitaki ukose vitu hivi vizuri.

Mwenyekiti amekubali na hivyo una nafasi ya kwenda kujifunza. Kama upo Arusha au eneo la karibu na utaweza kuhudhuria mafunzo hayo ya uwekezaji yatakayokusaidia sana, basi wasiliana na mwenyekiti wa Klabu Ya KISIMA CHA MAARIFA Arusha, Mwl Deo Kessy kwa namba 0717101505 ili kupata maelezo zaidi.

Rafiki, usipoteze tena nafasi hii, kama hukuweza kuanza mapema siyo tatizo sana, ila kama utashindwa kuanza tena sasa, umechagua mwenyewe.

UTT ni njia ambayo nashauri kila mtu aitumie kuwekeza, kwani ni rahisi, unaanza na kiwango kidogo na huhitaji kuwa na elimu yoyote kuhusu uwekezaji.

Ambacho nimekuwa nashauri na nimekieleza kwa kina kwenye kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA ni anza mapema na fanya kidogo kidogo. Usitishwe na kiasi kikubwa nilichoweka kwenye mfano, unaweza kuanza na kiasi kidogo cha shilingi elfu kumi tu na uzuri ni unaweza kufanya uwekezaji huo kupitia simu yako ya mkononi.

Karibu sana kwenye mafunzo ya uwekezaji kupitia UTT kwenye klabu ya KISIMA CHA MAARIFA Arusha, kama utashiriki, wasiliana na Mwl Deo Kessy kwa namba 0717101505, siku ya mafunzo ni kesho, hivyo chukua hatua mara moja sasa.

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania