Kwa kuwa mafanikio ni magumu kupatikana na kwa kuwa kwenye mambo mengi ambayo mtu anaanza kufanya atashindwa, wengi wamekuwa wanatengeneza mazingira ambayo yatawapa sababu za kushindwa.

Mfano mzuri ni kipindi ukiwa shule, japokuwa unajua una mtihani, unaweza usisome au usome kwa kujificha ili matokeo yanapotoka na ukawa hujafanya vizuri basi uwe na sababu kwamba kama ungeweka juhudi na kusoma, ungefanya vizuri zaidi.

Kwenye maisha ya kawaida tunaendeleza hilo, unajifanya huweki juhudi kubwa kwenye kazi au biashara yako na pale unaposhindwa kufanikiwa unajiambia ni kwa sababu hujaweka juhudi zaidi, kwamba kama ungeweka juhudi zaidi basi na wewe ungefanikiwa kama wengine.

Kingine ambacho wengi wamekuwa wanajifariji nacho ni kuangalia kile ambacho waliofanikiwa hawana au wanasumbuka nacho na kujiambia hiyo ndiyo sababu wao hawataki kufanikiwa. Mfano mtu anajiambia matajiri hawana amani kwa sababu muda wote wanafikiria kupoteza utajiri wao, hivyo yeye masikini ana amani kuliko aliye tajiri. Au kuona waliofanikiwa hawana muda kwa sababu wana mengi ya kufanya lakini yeye ambaye hajafanikiwa ana muda wa mambo yake.

Kote huko ni kujidanganya na kujipa vitu rahisi vya kujifariji ambavyo haviyafanyi maisha yako kuwa bora kwa namna yoyote ile. Kama kuna kitu unataka kwenye maisha yako, basi weka kila juhudi unazopaswa kuweka ili kukipata. Usitafute sababu za kujitetea pale utakaposhindwa. Iwapo umeweka kila juhudi na bado ukashindwa, hujapoteza chochote, jifunze na weka juhudi bora zaidi.

Na kamwe usijilinganishe na maisha ya wengine kwa kuangalia nje, usijione wewe ni bora au mwema zaidi ya wengine kwa yale unayoyaona kwa nje. Hujui kilicho ndani ya mtu hivyo usiusemee moyo wa yeyote yule. Wewe pambana na maisha yako, jua nini unataka na weka juhudi kukipata na siyo kuwakosoa wale waliopata kile ambacho wewe umekosa.

Usiwe mtu wa kutafuta sababu za kushindwa, badala yake weka nia na jitoe kweli kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha