2200; Tatua Tatizo Gumu…
Hii ni makala ya 2200 kwenye mfululizo wa makala ninazoandika kila siku na kuweka kwenye KISIMA CHA MAARIFA, kama ungependa kupata mafunzo haya ambayo ni ya kina kabisa kwenye mafanikio, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA.
Juzi tarehe 07/01/2021 dunia iliamka na habari moja kubwa, ya Elon Musk kuwa tajiri namba moja duniani kwa kumpiku aliyeshika nafasi hiyo kwa muda mrefu ambaye ni Jeff Bezos.
Wengi wameshangilia ushindi huo wa Musk kuweza kufikia nafasi hiyo kubwa. Lakini wengi hawajui jinsi alivyofika hapo.
Miaka zaidi ya 20 iliyopita, Musk alikaa chini na kutafakari matatizo makubwa na magumu kabisa yanayoikabili dunia. Aliweza kuja na matatizo matano ambapo baadhi ya hayo ni; malipo kwa njia ya mtandao, usafiri wa anga za juu, nishati mbadala ya uhakika na kurefusha umri wa watu kuishi.
Mara moja alijiunga na wengine na kuanzisha mfumo wa kwanza wa kufanya malipo kupitia mtandao wa intaneti, kipindi hicho (miaka ya 1990 mwishoni na 2000 mwanzoni) hakukuwa na mifumo ya aina hiyo. Kampuni waliyoanzisha ilikuwa kuwa paypal, ambayo ilikua kwa kasi a hatimaye wakaweza kuiuza kwa bei kubwa.
Fedha alizopata kwenye kuuza paypal angeweza kustaafu kabisa, asifanye chochote na maisha yake yaweze kuendelea bila ya shaka yoyote. Lakini alichukua zote na kuwekeza kwenye makampuni mapya matatu, kampuni ya safari za anga la juu (Space X), kampuni ya magari ya umeme (Tesla) na kampuni ya nishati ya umeme (Solar City).
Haya yalikuwa matatizo magumu mno kwa kipindi hicho. Mfano kwa usafiri wa anga za juu, hakuna mtu binafsi amewahi kufanya au kufikiri hivyo. Lakini yeye alianza na lengo lake lilikuwa moja, kwenda sayari ya Mars na kuhakikisha inakuwa sehemu inayoweza kukalika na binadamu. Kabla hajaingia kwenye hili, vyombo vya kwenda angani (rockets) zilikuwa zinarushwa mara moja tu na haziwezi kurudiwa tena. Alijua hiyo ndiyo inafanya gharama kuwa kubwa na kufikiria namna rocket inaweza kurushwa angani na kurudi ikiwa nzima ili iweze kutumiwa tena, kitu ambacho amekifanikisha.
Kadhalika kwenye kampuni ya magari ya umeme, makampuni mengi makubwa ya magari yamewahi kujaribu kutengeneza magari ya umeme, lakini yaliishia kushindwa vibaya. Ni tatizo gumu kweli kweli, kwa sababu hata kampuni yake yenyewe, pamoja na kufanikiwa kuzalisha magari ya umeme laki tano kwa mwaka, bado haijaweza kutengeneza faida.
Watu wanapopokea taarifa hizi za utajiri wa Elon Musk, wanajifunza mengi, lakini moja la msingi kabisa hawajifunzi. Ambalo ni kutatua matatizo magumu na kujipa muda.
Elon hakujidanganya, alikaa chini na kuiangalia dunia, akaangalia changamoto zilizopo na kuweza kuainisha matatizo magumu kabisa ambayo yanaikumba dunia.
Lakini pia hakutafuta njia ya mkato, alijipa muda, kwa karibu miaka 25 amekuwa akipambana na matatizo hayo, kuna wakati amepoteza sana, kuna wakati kila mtu alimkatia tamaa na kuona anakwenda kufilisika kabisa.
Lakini ameweza kuvuka yote hayo, na leo ni mtu tajiri kuliko wote duniani. Nafasi hii ya mtu tajiri siyo ya kudumu, maana kesho anaweza kuichukua mtu mwingine au akashuka iwapo thamani ya hisa za kampuni zake zitashuka. Lakini nafasi hii ni kiashiria kwamba dunia inathamini yale anayofanya.
Kwa kila unachofanya, angalia tatizo ambalo ni gumu kabisa na kisha pambana kutatua hilo. Tatizo gumu na ambalo wengi wanalikwepa ila ni kikwazo kwa watu ndipo mafanikio na utajiri mkubwa umelala.
Na ndivyo dunia imekuwa inakwenda, ukiangalia matajiri wote waliowahi kupita duniani, walitatua matatizo magumu kwa kipindi chao. Kuna kipindi chuma ilikuwa tatizo gumu, Andrew Carnegie akalitatua na kuwa tajiri namba moja. Kuna wakati mafuta yakawa tatizo kubwa, Rockerfeller akalitatua na kuwa tajiri namba moja. Kadhalika kwa Hendry Ford na magari.
Je wewe ni tatizo lipi gumu ambalo unalitatua? Jiulize na kujipa majibu ya swali hili kila siku ili uweze kuacha alama kubwa hapa duniani. Hata kama hutakuwa tajiri namba moja, kwa kutatua tatizo kubwa utagusa maisha ya wengi na kuacha alama duniani.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,