Rafiki yangu mpendwa,
Kilio kikubwa cha watu kwa sasa ni pengo kati ya matajiri na masikini kuzidi kuwa kubwa.
Matajiri wanazidi kuwa matajiri huku masikini wakizidi kuwa masikini.

Ni hali ambayo imezua taharuki kubwa hata kwenye nchi zilizoendelea na zenye utajiri mkubwa kama Marekani.

Tukichukulia kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita ambapo kwa sehemu kubwa uchumi wa dunia ulifungwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa korona, hilo limeongeza zaidi penguin kati ya matajiri na masikini.

Wakati mataifa mengi yaliwafungia wananchi ndani na wasifanye shughuli zozote, matajiri walizidi kuwa matajiri huku masikini wakizidi kudidimia kwenye umasikini.

Ukichukua mfano wa mtu tajiri zaidi duniani ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Amazon, Jeff Bezzos, wakati dunia imefungwa na biashara hazifanyiki, kampuni yake ndiyo iliingiza faida kubwa zaidi na yeye kuzidi kukuza utajiri wake.

Ukiangalia pia wamiliki wa mitandao mikubwa ya kijamii, kadiri watu walivyokaa nyumbani ndivyo walivyozidi kutajirika maana watu hawakubali na cha kufanya bali kuperuzi mitandao ya kijamii.

Serikali za mataifa hayo yaliyoendelea kwa kuona hali hiyo ya pengo kuwa kubwa, zimeamua kuchapa fedha zaidi na kuzigawa kwa masikini ambao kipato chako kiliathiriwa sana na kufungwa kwa uchumi.

Lakini hata kwa kufanya hivyo, bado pesa zote zinarudi kwa wale wachache ambao wana utajiri mkubwa.

Huwa natumia mfano kwamba kama serikali itakusanya fedha zote za nchi na kuzigawa sawa kwa kila mwananchi, baada ya muda mfupi zitakuwa zimerudi kwa wachache wale wale wenye utajiri mkubwa.

Ukiangalia mfano huo kwa hapa Tanzania, kama wote tutagaiwa kiasi sawa cha fedha, baada ya muda mfupi fedha zitakuwa zimerudi kwa akina Bakhresa, Dewji na wengineo.

Kinachosababisha hilo ni kwa sababu watu hao wametengeneza miundombinu ya kuzivuta fedha kuja kwao mara zote.

Katika historia ya fedha na utajiri kwenye dunia, fedha zimekuwa zinaenda kwenye uzalishaji.
Hata ukipewa kiasi sawa cha fedha na Bakhresa, bado utampelekea fedha zako Bakhresa kwa sababu anazalisha vitu ambavyo una uhitaji navyo.

Na hiyo ndiyo sababu kuu ya pengo kati ya masikini na matajiri kuzidi kuwa kubwa. Matajiri wana nyenzo za uzalishaji zinazovuta fedha kwao wakati masikini hawana nyenzo hizo.

Serikali nyingi kwa kuwa zinapenda matokeo ya haraka na kuwaridhisha masikini ambao ndiyo wapiga kura wengi, huwa hazihangaiki kutatua tatizo hilo la msingi, bali huhangaika kulifunika tu.
Serikali inapochapa na kugawa fedha kwa wananchi masikini, haitatui tatizo la msingi, bali inalifunika tu.

Kikubwa tunachojifunza hapa, kama kweli unataka kutoka kwenye umasikini na kwenda kwenye utajiri, hutaweza kufanya hivyo kwa kusubiri fedha ya kupewa, iwe ni kwa ruzuku au mshahara.

Njia pekee unayopaswa kutumia ni kuwa na nyenzo za uzalishaji ambazo zinazalisha kitu chenye uhitaji mkubwa.
Mlipuko wa ugonjwa wa korona unapaswa kuwa na funzo hilo kubwa kwetu kwa sababu umetikisha uchumi wa kila nchi duniani.
Hata kwa nchi ambazo hazikufunga uchumi wake, bado ziliathirika kwa sababu uchumi wa dunia unaingiliana sana.
Utalii, usafiri wa anga na biashara za kimataifa vinategemea sana uchumi wa nchi nyingine.

Kumiliki nyenzo za uzalishaji ni hitaji muhimu kabisa la kutoka kwenye umasikini. Lakini siyo wote wanaoweza kufanya hivyo, siyo wote wanaweza kupata mitaji mikubwa ya kuwa na viwanda au kuwa wasambazaji wakubwa wa bidhaa muhimu.
Lakini bado hilo siyo kikwazo, kwani uchumi unatoa fursa ya kushiriki moja kwa moja kwenye kumiliki nyenzo za uzalishaji kupitia soko la hisa.

Kama huwezi kumiliki nyenzo kubwa za uzalishaji wewe mwenyewe, basi hakikisha unanunua hisa za makampuni makubwa na kuzimiliki. Kwa njia hiyo, makampuni hayo yanapopata faida na wewe pia unanufaika.

Usikubali kuachwa nje ya uchumi kwa kuridhika na kile kipato unachopewa na wengine kwa njia mbalimbali. Kazana uwe na ushiriki wa moja kwa moja kwenye uchumi kwa kumiliki nyenzo za uzalishaji au kumiliki hisa za makampuni makubwa.

Kwa hapa kwetu Tanzania, soko la hisa la Dar (DSE) bado ni changa na lina fursa mbalimbali za kila mmoja kuweza kushiriki moja kwa moja. Jielimishe kwenye hilo na chukua hatua.

Lakini pia tuna mifumo ya pamoja ya uwekezaji (UTT) ambayo haihitaji wewe kuwa na utaalamu mkubwa kwenye mambo ya uwekezaji ndiyo ushiriki. Badala yake unaweza kuanza mara moja na kukuza uwekezaji wako.

Kama uko makini na hali yako ya kiuchumi unapaswa kuwa unajua kuhusu DSE na UTT, kama unadhani hivyo ni vitu vya wale ambao tayari ni matajiri basi jua umeruhusu wao waendelee kutajirika huku wewe ukiendelea kubaki kwenye umasikini.

Kwa kuwa umeamua hilo mwenyewe, huna wa kumlaumu. Na hata ukichagua kumlaumu yeyote utakuwa unajifurahisha tu maana haitakuwa na msaada kwako.
Hakuna tajiri atasusa kukusanya utajiri kwa sababu wewe masikini unalaumu mfumo hauna usawa.
Hakuna mfumo umewahi kuwa na usawa, wewe angalia wapi unaweza kunufaika na mfumo huu wa uchumi na patumie hapo.

Kama bado hujaanza kunufaika na mfumo huu wa uchumi siyo kwa sababu huna fedha au mtaji, bali kwa sababu huna elimu sahihi.
Na kwa zama hizi, siyo mpaka urudi shule ndiyo upate elimu sahihi, bali ziko njia nyingi unazoweza kutumia kujielimisha.

Kwenye kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA unapata nafasi ya kujifunza msingi muhimu kabisa wa fedha na uchumi, kuanzia kuongeza kipato, kuweka akiba, kufanya biashara na kuwekeza zaidi.
Kama bado hujapata kitabu hiki wasiliana na 0752 977 170 ukipate.

Kwenye kitabu cha TABIA ZA KITAJIRI unapata nafasi ya kujifunza namna sahihi ya kufikiri na kuchukua hatua ili uweze kutoka kwenye umasikini na kwenda kwenye utajiri. Maana kinachowatofautisha masikini na matajiri siyo juhudi kwenye kazi, masikini wanaweka juhudi kubwa kuliko hata matajiri. Ila matajiri wanaishia kupata faida kubwa kuliko masikini.
Usiseme mfumo hauna usawa, bali jua kinachowanufaisha masikini na uhakikishe kinakunufaisha na wewe pia.
Kama bado hujasoma kitabu hiki kipate sasa kwa kufungua; www.bit.ly/somavitabuapp

Rafiki yangu mpendwa, umejionea hapa ni sababu ipi kuu inawafanya matajiri kuzidi kutajirika huku masikini wakiendelea kuzama kwenye umasikini.
Chukua hatua sahihi ili uondoke kwenye umasikini na kwenda kwenye utajiri.
Anza na maarifa sahihi kisha chukua hatua.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.