2349; Nini Unajaribu Kuficha…

Huwa ipo kauli kwamba ukimuona mtu anajisifia sana kwa kitu fulani, jua hicho kitu hana au anatumia sifa hizo kuficha kitu kingine ambacho hataki kionekane.

Mfano mtu anayesema mimi siyo muoga hata kidogo, huwa ndiye muoga zaidi. Anatumia kauli hiyo kuficha uoga wake.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye maeneo mengi ya maisha, kwa kila unachopenda sana kufanya, kuna kitu unajaribu kuficha kwa njia hiyo.

Kama una ulevi au uraibu wa kitu fulani, kuna ukweli wa maisha hako ambao hujataka kukubaliana nao.
Kama una chuki dhidi ya wengine, unaficha chuki uliyonayo kwako mwenyewe.

Chochote unachojikuta unafanya kwa kupitiliza, ni njia ya kuficha kitu kingine ambacho unacho.
Hivyo kama unataka kubadili maisha yako, usihangaike na kile unachofanya kupitiliza, bali jua kwanza nini umekuwa unaficha.

Huenda huipendi kazi yako ndiyo maana umekuwa mlevi. Au mahusiano yako mabovu na mwenza wako ndiyo yanafanya uwe na chuki kwa wengine.

Kuhangaika na kile unachofanya sana hutaweza kubadilika na kudumu kwenye mabadiliko hayo. Unaweza kufanikiwa kwa muda ila utateleza na kurudi tena.

Kwa kutambua kile unachojaribu kuficha na kukitatua, moja kwa moja unakuwa umetatua kile unachofanya sana.

Jua tobo liko wapi na ulizibe kabla hujakazana kujaza chombo.

Na kama Lao Tzu alivyoandika kwenye Tao Te Ching, wanaoongea sana hawajui na wanaojua hawaongei sana.
Chochote unachofanya sana na kuficha kitu fulani ambacho hutaki kukikubali au hutaki kionekane na wengine.

Kocha.