2470; Zima, Washa.

Jana dunia ilikubwa na taharuku baada ya mitandao mikubwa ya kijamii ambayo imeshakuwa tegemeo kwa wengi kutokupatikana hewani.

Nimekuwa siyo mtumiaji wa mitandao ya kijamii, ila natumia mtandao wa WhatsApp kwa mawasiliano na huduma mbalimbali ninazotoa.

Na hali ya jana ilinikuta nikiwa katikati ya mawasiliano na mtu, yakakatika ghafla.
Nikaangalia labda ni salio la intaneti limeisha, ila likawa lipo.
Nikaona labda ni simu imepata shida fulani na hivyo kuizima na kuiwasha, lakini hiyo nayo haikusaidia.

Basi nikajiambia nitaacha mpaka baadaye labda kuna tatizo la kimtandao.
Ni mpaka baadaye sana mtu mwingine niliyekuwa nawasiliana naye kwa wasap alinitafuta kwa njia ya kawaida na kuniambia mitandao hiyo mikubwa ya kijamii imepata shida.

Kilichonishangaza ni kwa namna gani niliamini mtandao huo na kutokushuku unaweza kuwa shida.
Nimeiona hatari niliyoandika kwenye kitabu cha EPUKA UTUMWA WA KIDIJITALI ambapo tumekuwa na utegemezi mkubwa sana kwenye mitandao hii.

Lakini hili pia limetupa funzo kubwa la tamu na chungu za biashara ya uhodhi (monopoly).
Mitandao mikubwa iliyopata shida, yaani wasap, instagram na facebook, yote inamilikiwa na kampuni moja.
Mitandao mingine haikupata shida hiyo.

Kwa kampuni moja kuhodhi mitandao yote mikubwa, kuna hatari kubwa ya kuathiri wengi pale tatizo kama la jana linapotokea.

Na funzo kubwa kabisa tunaloondoka nalo kwenye hilo ni kutoruhusu teknolojia kutawala kila eneo la maisha yetu.
Kwa jana wengi walitaharuki kama vile ndiyo mwisho wa dunia, kwa sababu tayari wanategemea sana teknolojia hizo.

Kama nilivyoeleza kwenye kitabu cha EPUKA UTUMWA WA KIDIJITALI, hatuwezi kuepuka teknolojia hizi moja kwa moja, kwa sababu zina manufaa. Ila tunaweza kuzizuia tusiwe tegemezi kwazo. Tunaweza kuhakikisha maisha yetu hayaathiriki sana hata kama teknolojia hizo zitaondoka.

Binadamu tumekuwa tunajenga mahusiano na ushirikiano kwa miaka mingi kabla ya kuja kwa teknolojia hizi. Hatupaswi kuruhusu teknolojia mpya kuvunja kile ambacho tulishakijenga kwa miaka mingi.

Jenga mahusiano na ushirikiano bora na wengine ambao hautegemei kwenye teknolojia pekee. Lolote linaweza kutokea kwenye teknolojia hizi.

Hatua ya kuchukua;
Ni maeneo gani ya maisha yako ambayo yanategemea sana teknolojia mpya kiasi kwamba teknolojia hizo zikiondoka leo utaathirika sana? Anza kujenga njia mbadala isiyotegemea teknolojia hizo mpya.
Mfano kama biashara yako inategemea teknolojia hasa za mitandao ya kijamii, hakikisha pia unakuwa na njia ya moja kwa moja ambayo haitegemei teknolojia hizo.
Ili lolote linapotokea kwa teknolojia hizo, huathiriki kabisa.

Tafakari;
Usiruhusu maisha yako na maeneo muhimu ya maisha yako kutegemea moja kwa moja kwenye kitu chochote kilicho nje ya udhibiti wako. Jua chochote usichodhibiti huna nguvu nacho.
Kuwa na mbadala kwa kila ambacho huna udhibiti nacho.

Kocha.