Rafiki yangu mpendwa,
Watu wamekuwa wanakimbizana sana na fursa,
Lakini kwa bahati mbaya zimekuwa zinageuka na kuwa fursana.

Yaani zinakuwa fursa za kitapeli ambazo zinaishia kuwapotezea watu muda wao, fedha na hata wakati mwingine kuharibu sifa zao.

Kwa nafasi niliyofikia na kwa watu kuona nina mtandao mkubwa, huwa haipiti wiki mtu hajaja na fursa fulani kwangu.
Huwa wanakuja na ushawishi mkubwa kwamba ni fursa nzuri na ambayo sipaswi kuikosa kwani ina manufaa makubwa.

Kipindi cha nyuma ambapo nilikuwa na muda niliweza kutafiti kila fursa kwa undani wake na kupata majibu sahihi kama ni fursa kweli au utapeli.
Lakini kwa sasa sina muda wa kuwekeza kutafiti kila fursa kwa undani wake.

Hivyo nimejitengenezea kanuni rahisi ambazo nimekuwa nazitumia kupima fursa kwa haraka na kuona kama ni sahihi au ni utapeli.
Ni kanuni ambazo kila mtu anaweza kufanyia kazi na akajiepusha kuingizwa kwenye fursa za kitapeli zinazomgharimu.

Leo nakushirikisha kanuni hizo na namna unavyoweza kuzitumia kwa manufaa yako.

1. Kama unalazimishwa sana, wewe ndiyo fursa.

Kama watu wanakulazimisha sana uingie kwenye fursa fulani, basi jua hapo hakuna fursa, ila wewe ndiyo fursa
Kwa wewe kuingia kwenye fursa hiyo wao ndiyo wananufaika.
Swali moja rahisi sana la kujiuliza, ni lini kwenye maisha yako mtu amewahi kukulazimisha kukupa fedha?
Kama hujui basi jua pia na fursa zipo hivyo, fursa sahihi hazihitaji ulazimishwe.

2. Kama inakimbiliwa na walio wengi.

Watu wengi ni wavivu, wasiotaka kuumia na kazi na wanaotaka njia za mkato za kufanikiwa.
Ukiona kitu ambacho kinakubalika na walio wengi, jua kabisa kwamba hakihusishi kazi kubwa na wala siyo kigumu.
Sasa kama unaambiwa kuna fursa na haihusishi kazi au ugumu, hakuna fursa hapo.

3. Kama haielezi manufaa nje ya fedha.

Ukiona fursa inaeleza manufaa ya kifedha tu na hakuna kingine nje ya hapo, jua hakuna fursa.
Watu wanajua fedha zinawanasa watu haraka na hivyo kutumia kama mtego.
Kwenye kila fursa unapaswa kuangalia ni manufaa gani nje ya fedha ambayo wewe na wengine wanayapata.
Kwa maneno mengine lazima kuwe na thamani inayozalishwa na fursa hiyo, la sivyo hakuna fursa hapo.

4. Sifa binafsi za watu walioibeba fursa hiyo.

Angalia sifa binafsi za wale wanaoileta fursa kwako.
Kama ni watu ambao kila mara wanakuwa na fursa mpya wanayokimbizana nayo jua hao ni wasaka fursa zaidi na hakuna thamani wanayotoa.
Pia angalia ni vitu gani vikubwa wameweza kukamilisha kwenye maisha yao.
Kwa kifupi kama mtu siyo makini, basi hata fursa anayoleta kwako siyo makini.

5. Unaisikia fursa kwa kila mtu.

Fursa huwa ni fursa yenye manufaa pale ambapo wengi bado hawajaijua.
Katika kipindi hicho inakuwa na hatari kubwa na wengi hawapo tayari kuingia.
Kwa uchache wa waliotayari kuingia kwenye fursa husika, kunaifanya iwe na thamani zaidi.
Lakini pale fura inapokuwa imeshajulikana na kila mtu, inakuwa siyo fursa tena, inakuwa ni kitu ambacho kila mtu anafanya.

Rafiki, kanuni hizi zitakuondolea kabisa utapeli wa kifursa, lakini pia zinaweza kukunyima fursa chache nzuri.
Lakini hilo halitakuwa na madhara kwako, maana kama wewe ni mtu sahihi basi fursa sahihi zitakuja kwako.

Na kama ambavyo Richard Branson amewahi kusema, fursa ni kama daladala, ukikosa moja jua kuna nyingine inakuja.
Muhimu ni wewe uondokane na papara ya fursa, uchague kwa umakini aina ya fursa unazojihusisha nazo ili iwe na manufaa kwako na kwa wengine pia.

Pata na usome kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO ili uweze kuwa mtu sahihi ambaye fursa sahihi zinakuja kwako.
Kupata kitabu hiki wasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa kitabu ulipo.

Pia watu wengi wamekuwa wanadanganywa na fursa za uongo zilizojificha nyuma ya biashara ya mtandao (network marketing).
Nimeandika kitabu kinachoelezea kwa kina mfumo huo wa biashara na jinsi ya kujua iliyo halali na utapeli.
Kitabu ni softcopy na kinatumwa kwa email.
Kukipata tuma elfu 5 kwenda namba 0717 396 253 na kisha tuma email yako na jina la kitabu IJUE BIASHARA YA MTANDAO na utatumiwa kitabu hicho.

Usikubali wewe kugeuzwa fursa na matapeli waliojaa kila kona.
Kuwa mjanja na kuwa makini, fursa sahihi zitakuja kwako.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.somavitabu.co.tz