2507; Siyo wa tofauti kama unavyodhani.

Kuna vitu ambavyo huwa vinawatokea watu wengi kwenye maisha yao kutokana na yale wanayofanya au vile walivyo.
Yaani wanachopata ni matokeo ya hatua walizochukua au namna walivyo.
Inakuwa imezoeleka hivyo kiasi kwamba ukimwona tu mtu anafanya kitu fulani au yulo kwa namna fulani, unajua kabisa ni matokeo gani anakwenda kupata.

Ukimwona mtu ambaye siyo mlevi, ila marafiki zake wote ni walevi unajua kabisa ataenda kuishia kwenye ulevi.
Ukimwona mtu ambaye hapendi kazi au biashara anayofanya na hajitumi unajua kabisa hawezi kufanikiwa kwenye hilo.
Ukimwona mtu ambaye matumizi yake ni makubwa kuliko mapato unajua kabisa ataishia kwenye madeni mabaya.
Na ukimwona mtu ambaye ana tamaa ya mafanikio ya haraka na asiye tayari kuweka kazi unajua kabisa ataishia kutapeliwa.

Kwa wengine ni rahisi kuona hayo na kujua kabisa watu wanaenda kuishia wapi.
Lakini inapokuja kwako binafsi, huwa unakuwa mbishi sana.
Huwa unadhani wewe ni tofauti, huwa unaona matokeo kwako yatakuwa tofauti, siyo sawa na wengine.

Unajiambia japo marafiki zako ni walevi na wewe siyo, utashirikiana nao kwenye mambo mengine lakini siyo ulevi.
Unajiambia japo hupendi kazi au biashara unayofanya sasa, utakwenda kupata iliyo nzuri na kuipenda sana.
Unajiambia japo matumizi yako ni makubwa kuliko kipato, utakwenda kutatua hilo kipato kikiongezeka.

Hayo na mengine mengi unayojiambia wewe uko tofauti jua tu unajidanganya wewe mwenyewe.
Huna tofauti kubwa sana na wengine inapokuja kwenye matokeo utakayopata kulingana na unachofanya au ulivyo.
Ni bora usijidanganye, ukabili ukweli ulivyo na uchukue hatua sahihi ili kupata matokeo sahihi.

Hatua ya kuchukua;
Kumbuka ni mara ngapi umewahi kujiambia kwako itakuwa tofauti ila ikaishia kuwa kama wengine?
Kuanzia sasa, kila unapojiambia matokeo kwako yatakuwa tofauti na wanayopata wengine, jikamate na ujiulize kipi unafanya tofauti na wao?
Kama hakuna unachofanya tofauti, jua tu unajidanganya.

Tafakari;
Ukifanya kile wanachofanya wengine, kwa namna ile ile wanavyofanya wao, usishangae pale unapopata majibu kama ya kwao.
Kupata majibu tofauti na wanayopata wengine, lazima ufanye vitu tofauti na wanavyofanya wengine.

Kocha.