Rafiki yangu mpendwa,
Maisha ni mfululizo wenye machaguo ya kupata na kukosa (trade off).

Hata uchague kiasi gani na uwe na mamlaka makubwa kiasi gani, huwezi kupata kila unachokitaka, kwa wakati unaokitaka na kwa namna unavyotaka.

Hilo halipo kabisa, lakini ukaidi wetu wa kutaka kupingana na hilo umekuwa ndiyo chanzo cha msongo kwenye maisha, kwa kudhani kuna namna ambayo bado hatujaijua ya kupata kila tunachotaka.

Ukomo huo hauishii tu kwenye maisha, bali unaenda kwenye kila eneo la maisha kama kazi, biashara, fedha, mahusiano na kadhalika.

Mfano chanzo cha changamoto nyingi za mahusiano ni mtu kutaka apate mwenza ambaye ana kila anachotaka yeye, kitu ambacho hakijawahi kutokea duniani.

Leo tunakwenda kuangalia ukomo huu tulionao kwenye eneo la biashara na kwa pande zote mbili zinazohusika kwenye bishara, yaani wauzaji na wanunuaji.

Kuna sifa kuu tatu ambazo zinaweza kuitofautisha biashara yoyote ile na biashara nyingine. Lakini sifa hizo zina ukomo, hakuna biashara inayoweza kuwa na sifa zote tatu. Chache zinazojitahidi sana zinaweza kuwa na sifa mbili, ila kwa nyingi zinakuwa na sifa moja kuu.

Zifuatazo ni sifa kuu tatu za kuitofautisha biashara na jinsi zinavyoweza kutumika.

Sifa ya kwanza; Urahisi.

Hapa biashara inauza bidhaa au huduma zake kwa bei rahisi ambayo wateja wengi wanaweza kuimudu.
Bei hiyo inakuwa inaendana na ile iliyo sokoni au kuwa chini ya hapo.

Kwa kuwa na bei rahisi, watu wengi wanavutiwa kwenda kununua.

Sifa hii inaweza kutumiwa na biashara zinazouza vitu vya kawaida ambavyo haviwezi kujitofautisha sokoni.
Kwa biashara zinazonunua jumla na kuuza rejareja, bei ni sifa kuu ya kujitofautisha.

Sifa ya pili; Ubora.

Hapa biashara inakuwa na bidhaa au huduma ambazo ni bora kuliko zile ambazo zinapatikana sokoni.

Ubora huo unaweza kuwa kwenye uimara, matumizi na kudumu kwa kile ambacho mteja anauziwa.

Sifa hii ya ubora inampa mteja uhakika kwamba akinunua hakuna anachopoteza, kwani anapata kitu kilicho bora kweli.

Sifa hii inaweza kutumiwa na biashara ambazo zinazalisha bidhaa na huduma zake yenyewe na hivyo kuweza kudhibiti ubora wake.

Sifa ya tatu; Huduma.

Hapa biashara inatoa huduma bora kabisa kwa wateja wake kiasi cha wateja kujisikia ufahari wanapokuwa kwenye biashara.

Kwa sifa hii, wateja wanajaliwa, wanasikilizwa vizuri, wanahudumiwa kwa haraka na hata kusaidiwa pale wanapopata changamoto mbalimbali kwenye kile wanachonunua.

Sifa hii inawavutia wateja kwa sababu wanapata kujisikia vizuri kwa namna wanavyochukuliwa na kuhudumiwa.

Sifa hii inaweza kutumiwa na biashara zinazolenga wateja wanaotaka ufahari zaidi, ambao bei kwao siyo changamoto sana, kwa sababu wana uwezo mzuri.

Ukomo wa kutumia sifa zote tatu kwa pamoja.

Kama tulivyojifunza hapo juu, hakuna biashara inayoweza kujijengea sifa zote tatu kwa pamoja.
Ni chache sana zinazoweza kujenga sifa mbili, ila biashara nyingi zinajenga sifa moja.

Urahisi.
Biashara inapokuwa na sifa ya kuuza kwa bei rahisi, inakuwa na vikwazo viwili;
Moja ni haiwezi kuuza bidhaa ambazo ni bora, kwa sababu bei yake inakuwa juu.
Mbili ni haiwezi kutoa huduma bora kwa wateja kwa sababu haiwezi kumudu kuwa na wahudumu wengi.
Hivyo urahisi unaweza kuwa sifa kuu, kisha moja kati ya ubora na huduma ikawa sifa nyingine, lakini siyo zote kwa pamoja.

Ubora.
Biashara inapokuwa na sifa ya ubora, inakuwa vigumu sana kuuza kwa bei ya chini.
Na kama itakuwa na ubora na kuuza kwa bei ya chini, haiwezi kuwa na huduma bora kwa sababu haitaweza kumudu kulipa wahudumu wengi.

Huduma.
Biashara inapokuwa na sifa ya huduma bora, haiwezi kuuza kwa bei rahisi kwa sababu kuwalipa wahudumu wengi kunaongeza gharama za biashara. Na kama itakuwa na huduma bora na kuuza kwa bei rahisi, hasi ubora wa bidhaa au huduma inayouzwa hauwezi kuwa mzuri.

Kama ulivyojionea hapo rafiki, hakuna namna unaweza kutimiza hivyo vitatu kwa wateja wako, hata ujaribu kwa namna gani.
Hivyo kwenye biashara unayofanya, chagua sifa kuu itakayokutofautisha na ya pili itakayoambatana  nayo, kisha ya tatu usihangaike nayo kabisa.

Na hilo unaweza kuliona wazi kwenye biashara mbalimbali tunazojihusisha nazo kila siku.
Chukua mfano wa simu janja (smartphone). Iphone na Tecno zote ni simu janja, unazoweza kutumia kufanya vitu vinavyofanana.
Lakini sifa kuu ya iPhone ni ubora, kisha huduma na bei iko juu kabisa.
Sifa kuu ya Tecno ni urahisi, kisha huduma lakini ubora haupo juu.

Je wewe ni sifa ipi kuu inayoitofautisha biashara yako?
Ipi sifa ya pili unayoijenga?
Na ipi sifa ya tatu unayochagua kuipuuza kabisa?
Haya ni maamuzi muhimu unayopaswa kuyafanya kwenye biashara yako ili ujue unaposimama na usiyumbishwe yumbishwe.

Karibu uendelee kupata maarifa bora ya kukuwezesha kuiendesha biashara yako kwa kupata kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA. Wasiliana sasa na 0752 977 170 kujipatia nakala yako ya kitabu uache kuendesha biashara kwa mazoea.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.