2538; Nafasi ya kukosea.
Ukikuta daraja limeandikwa tani 10, yaani mwisho wa uzito wa kupita hapo ni tani 10, haimaanishi ukipitisha tani 11 litavunjika.
Hata kwa dawa nyingi, unapoambiwa dozi ni vidonge viwili, haimaanishi ukinywa vitatu utakufa hapo hapo.
Mifumo mingi imewekewa nafasi kubwa ya kukosea bila ya kuleta madhara makubwa.
Hata miili yetu, inatenga nafasi kubwa ya kukosea kwenye mambo mbalimbali ili uweze kuwa hai.
Ndiyo maana ukiwa na msongo presha na mapigo ya moyo yanaweza kwenda juu sana, lakini baadaye yakarudi sawa.
Tatizo linakuja kwenye mipango yetu binafsi, huwa hatuweki nafasi kubwa ya kukosea na pale makosa yanapotokea yanakuwa na madhara makubwa.
Sehemu kubwa ya msongo tunaopata kwenye maisha unatokana na kukosa nafasi ya kukosea kwenye yale tunayofanya.
Ni pale unapojua jukumu linachukua siku mbili kukamilisha halafu unawaahidi watu utakamilisha kwa siku hizo mbili.
Kama kila kitu kitaenda sawa, utakamilisha kweli.
Lakini ni nadra sana kila kitu kikaenda sawa, maana kuna mengi hayapo ndani ya uwezo wako yanaweza kukukwamisha.
Kinachotokea ni unashindwa kukamilisha ndani ya muda ulioahidi na hapo ndipo matatizo yanapoanzia.
Kama ungejipa muda wa ziada, kama tahadhari iwapo mambo hayataenda kama ulivyopanga, unakuwa na nafasi ya kukosea bila kuathiri matokeo ya mwisho.
Hatua ya kuchukua;
Kwa kila unachopanga kufanya, weka nafasi ya kukosea. Jiulize ni namna gani mambo yanaweza kwenda tofauti na ulivyopanga kisha jipange kwa namna ambayo hata yakitokea hayatakuwa kikwazo kikubwa.
Yaani zijue njia zote unazoweza kukosea na jipange kwa namna ambayo kama makosa yatatokea hayatakwamisha mpango mzima.
Tafakari;
Mipango siyo matumizi, kwa kila unachopanga, kuna mengi yanaweza kukikwamisha. Jiwekee nafasi ya kukosea kwenye kila mpango ili uweze kukamilisha vizuri.
Kocha.