2558; Miaka 7 ya kuandika kila siku.
Kama umekuwa huelewi, namba zinazotangulia kwenye hizi nakala za kurasa, ni idadi ya siku nilizoandika kwa mfululizo bila kuacha hata siku moja.
Huwa sijikumbushi hili mara kwa mara kama vile ndiyo mafanikio yenyewe, ila huwa naangalia kama namba zinaenda sawa. Maana ni rahisi kupoteza mtiririko wa namba, kwa kuruka namba fulani au kurudia namba fulani.
Hivyo kila baada ya muda, huwa naingia google na kuuliza ni siku ngapi zimepita tangu tarehe 01/01/2015 mpaka sasa?
Namba ninayopata nalinganisha na ukurasa wa siku husika.
Nilifanya zoezi hilo jana na kushtuka kumbe ni miaka 7 tangu nilipoanza zoezi hili la kuandika kila siku bila kuacha.
Ilikuwa ni tarehe 01/01/2015, siku ya mwaka mpya wa kalenda ambapo nilipokea jumbe ambazo watu hutumiana kwenye siku za mwaka mpya.
Ujumbe huo ulisema leo ni ukurasa mpya wa kitabu kipya cha mwaka 2015, je utajaza nini kwenye ukurasa huo?
Na hapo hapo nikapata wazo, kwa nini nisiichukulie kila siku kama ukurasa na kuandika makala ya ukurasa mmoja kila siku?
Hivyo ndivyo makala hizi fupi za kurasa zilivyozaliwa na katika kipindi hicho cha miaka saba zimepitia mageuzi mbalimbali.
Kama ningeanza kwa kuangalia ni miaka mingapi ijayo nitaandika kila siku, kwa hakika ningekata tamaa na kuacha.
Lakini hilo siyo ninaloangalia, hata sasa.
Ninachoangalia ni hiki, leo nimeamka, wacha niandike kwanza makala ya ukurasa wa leo kabla siku haijaanza.
Na sijawahi kukosa hata siku moja kwa sababu ndiyo kitu cha kwanza kufanya kwenye siku husika.
Na sasa nimeboresha zaidi, naandika kwa simu hivyo sina sababu wala kisingizio cha kutokuandika.
Hatua ya kuchukua;
Ni kitu gani kimoja ambacho umekuwa unafanya kila siku bila kuacha?
Kama huna ni kitu gani unachochagua kufanya kila siku bila kuacha?
Jiambie tu kwamba kila ninapoamka, nitafanya hiki, na hapo ndiyo mwisho wa mjadala. Hujiambii vipi ikiwa hivi au vile, wewe unafanya kama ulivyopanga.
Tafakari;
Ni kile unachofanya kila siku, hata kama ni kwa hatua ndogo kiasi gani ndiyo kinachoyajenga maisha yako. Kuwa makini sana na mazoea yako ya kila siku, ndiyo adui yako mkubwa kwenye kupiga hatua.
Kocha.