2923; Haina maana.

Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye upo kwenye biashara lakini bado hujajitoa kafara kweli kweli ili kufanikiwa kwenye biashara.

Leo nakwenda kukuambia kitu ambacho kinaweza kukukatisha kabisa tamaa au kukupa nguvu ya kupambana sana.

Kitu chenyewe ni hiki; KAMA LENGO LAKO SIYO KUWA BILIONEA, USIFANYE BIASHARA.

Ndiyo, najua hiyo ni kauli kali, kauli tata na inayoweza kupingwa na kila mtu kwa sababu na ushahidi mwingi.
Lakini kadiri ninavyofanya biashara na kushirikiana kwa karibu na wafanya biashara, ndivyo ninavyozidi kushawishika kwamba haina maana kwa mtu asiye na matamanio makubwa kuingia kwenye biashara.

Na matamanio makubwa yanaweza kupimwa kwa njia mbalimbali, lakini moja ya uhakika ni kutaka kufikia ubilionea.

Sioni sababu ya mtu yeyote kuchagua kuyaharibu maisha yake kwa kujihusisha na biashara kama hana matamanio makubwa sana na ambayo hayajazoeleka.

Naposema kuharibu maisha, namaanisha kweli, hasa yale maisha yaliyozoeleka kwenye jamii.

Huwezi kujenga biashara kubwa na wakati huo huo ukawa na maisha ya kawaida kwenye jamii.
Maisha ya kawaida ndiyo kitu cha kwanza kabisa utakachopaswa kutoa kafara kwenye safari ya kujenga biashara.

Kuna vitu vingi ambavyo watu wa kawaida kwenye jamii wanavifanya na wanategemea na wewe uvifanye, ila hutaweza kuvifanya.
Hilo litafanya uonekane ni wa ajabu na usiyejali, utapewa lawama na shutuma za kila aina.
Lazima uwe na ngozi ngumu ya kuweza kuyapokea na kuyavuka hayo bila ya kuyumbishwa kwa namna yoyote ile.

Kwa kifupi kama unataka umridhishe kila mtu, kama unataka ukubalike na kila mtu, tayari hayo yanapingana na kujenga biashara kubwa.

Na ubaya mkubwa ni kitu kisicho na mwisho. Maana unaweza kusema unajenga biashara na ikishakufikisha kwenye uhuru wa kifedha basi unastaafu na kuyafurahia maisha.
Unachokuja kugundua ni kwamba uhuru wa kifedha wenyewe ni kazi iliyokamilika.
Kitendo tu cha kuwa bilionea tayari ni kazi kubwa ya kufanya, maana kuna mambo mengi sana yatakayokuwa yanakutegemea.

Hayo ni mateso bila chuki, hivyo kama hujadhamiria na kujitoa kweli, haina haja ya kuingia kwenye mateso hayo.

Kama lengo lako ni kupata fedha ya kuendesha maisha yako, fedha ya kula na kuendesha gharama nyingine za maisha, kuna njia nyingine za kukamilisha hayo bila ya kuingia kwenye mateso ya biashara.

Njia mojawapo ni ya ajira, kuajiriwa na mtu na kupewa majukumu ya kufanya. Njia hii ina ukomo wa kipato, lakini pia ina mipaka ya kazi na maisha. Ukiwa kazini unafanya kazi, muda wa kazi ukiisha unafanya mengine.
Hiyo ni anasa ambayo huipati ukiwa unajenga biashara, maisha yako binafsi na biashara havina mipaka. Muda wote ni muda wa kufanya kazi kwenye biashara yako.

Njia nyingine unayoweza kutumia ni mauzo. Kwa kuwa nafasi za ajira ni chache na hazipatikani, unaweza kufanya kazi ya mauzo na ukaingiza kipato cha kuyaendesha maisha yako.
Hapa unachofanya ni kuangalia bidhaa au huduma unayoikubali sana na unayoweza kuiuza vizuri. Kisha kuongea na mfanyabiashara anayeiuza na kumpa mpango wa kufanya mauzo kisha akulipe kwa kamisheni. Kama ukiweza kuwa muuzaji mzuri, hakuna atakayekataa mpango huo.

Kazi ya mauzo ni rahisi kuliko kujenga biashara kwa sababu umakini wako unaweka kwenye mauzo pekee.
Huhitaji kuhangaika na mengine ya kujenga biashara kama kuajiri, kupata mtaji na kukamilisha matakwa mbalimbali ya kisheria ya kuendesha biashara.
Lakini pia mauzo, hasa ya kulipwa kwa kamisheni hayana ukomo wa kipato, unaweza kuingiza kipato kikubwa uwezavyo kama utakuwa tayari kuuza kwa wingi zaidi.

Kwa ujumbe huu, nataka ukate shauri kabisa.
Kama umeamua kujenga biashara, basi jitoe hasa na jiandae kwa kila litakalokukabili.
Usiwe mlalamikaji au mtu wa kulaumu kutokana na yale yanayokukabili.
Na kama unaona huwezi hilo, basi fuata njia nyingine, hasa ya mauzo ambayo haina ugumu kama wa biashara.

Kama umeamua kujenga biashara, jenga biashara kweli.
Usiwe kama wengi ambao wanacheza kwenye biashara.
Ambao miaka nenda rudi wako pale pale na hakuna hatua wanazopiga.
Wewe unataka makubwa na upo tayari kujitoa kwa kila namna kuyapata.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe