2939; Mnatofautiana sana.

Rafiki yangu mpendwa,
Wewe na wafanyakazi uliowaajiri kwenye biashara yako mnatofautiana sana.

Mnatofautiana kimtazamo, wakati wewe unaangalia kujenga biashara ambayo itakuwa kubwa na yenye mafanikio, wao wanachoangalia ni kufanya kazi ya siku husika tu.

Mnatofautiana kiajenda, wakati ajenda yako ni kuhakikisha wanafanya kazi kubwa kwa malipo unayoweza kuwapa, wao ajenda yao ni kufanya kazi ndogo iwezekanavyo kwa malipo unayowapa.

Wakati wewe unaona unawalipa kuliko kazi wanayofanya, wao wanaona wanafanya kazi kubwa kuliko malipo unayowapa.

Mnatofautiana vipaumbele, wakati kipaumbele chako kikubwa kikiwa mauzo na faida kwenye biashara, wao vipaumbele vyao ni tofauti kabisa na mauzo na faida siyo vitu vinavyowanyima usingizi.

Kwa mfano kama huwa mnafunga biashara saa 12 jioni, saa 12 kasoro dakika 5 anakuja mteja. Ni siku ambayo hamjauza sana, wewe unafurahia mteja huyo kuja na upo tayari mzidishe muda wa kufunga ili mteja ahudumiwe vizuri. Lakini wafanyakazi wako watachukia kitendo cha mteja kuja muda wa kufunga na kuhakikisha wanaharakisha kumhudumia ili asiwacheleweshe kutoka.

Wewe ndiye ngozi yako imeingia kwenye mchezo, biashara yako ikifa leo, wewe ndiye unayebeba hasara yote, wao wataenda kutafuta kazi mahali mengine, bila mzigo wa hasara.

Hakuna ubaya wowote kwenye tofauti hizi, ni kitu ambacho kipo na hatuwezi kukikwepa.
Ubaya ni pale watu wanapojisahaulisha na kudhani wao na wafanyakazi wao ni kitu kimoja.

Unaweza kutamani sana wewe na wafanyakazi wako muwe kitu kimoja, lakini kiasili hilo haliwezekani.
Ni vyema kuukabili uhalisia ulivyo kuliko kutaka uwe vile unavyotaka wewe.

Ijue nafasi yako kwenye biashara na usimame hapo, ukihakikisha wafanyakazi wako wanasimama sehemu wanazopaswa kusimama.
Wakati mwingi inahitaji uwalazimishe wafanye kile ulichowaajiri kufanya.
Unaweza kushangaa kwa nini iwe hivyo, kazi waliomba wenyewe na sasa umewapa ila hawataki kuifanya.
Ni tofauti zilizopo kati yenu.

Weka viwango vyako vya kibiashara na hakikisha kila aliye kwenye biashara yako anavifikia.
Anza wewe mwenyewe kwa kuvifikia kisha usiwe na huruma kwa asiyevifikia.
Wafanyakazi watasukumwa kuvifikia viwango hivyo au watashindwa na kukimbia hivyo kuacha nafasi kwa wanaoweza.

Wafanyakazi wako kwenda kinyume na wewe, kukupinga, kukuibia, kukwepa majukumu na hata kukukwamisha kusikuumize. Hawana ubaya wowote na wewe, ni vile tu ajenda zenu zinatofautiana.
Wajibu wako ni kuhakikisha kuna ajenda moja tu inayofanyiwa kazi kwenye biashara yako, ajenda yako.

Wafanyakazi wako hawatafurahia kitendo cha ajenda yako kutawala na ajenda yao kukosa nafasi.
Lakini wewe unachowapa ni kazi, furaha wanapaswa kuitengeneza wenyewe.
Kama pia unataka kumfurahisha kila mtu kwenye biashara, hutakuwa na biashara na hutakuwa na furaha.

Kama ambavyo huwezi kuwabadili mwewe wasile kuku, ndivyo pia huwezi kuziondoa tofauti zilizopo kati yako na wafanyakazi wako kwenye biashara yako.
Ujue uhalisia huo na kuuishi, itakupunguzia sana msongo wa mawazo.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe