2956; Viwango, Fokasi na Kasi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kama unataka kujenga biashara yenye mafanikio makubwa sana, unapaswa kufanyia kazi kwa uhakika maeneo hayo matatu.

Unapaswa kuweka viwango vya juu sana kisha kuhakikisha watu wote wanafikia viwango hivyo.
Biashara nyingi hazifanikiwi kwa sababu hakuna viwango vilivyowekwa.
Biashara inakuwa haina msimamo wowote.
Kila wakati inabadilika ili kuendana na kila mtu.
Mwishowe inakuwa ni biashara isiyoeleweka inalenga watu gani na kusimamia nini.

Biashara inapaswa kuwa na fokasi, kwa umakini wote kupelekwa kwenye vitu vichache ambavyo ndiyo muhimu zaidi.
Biashara nyingi hazifanikiwi kwa sababu kila wakati zinakimbizana na vitu vipya vinavyojitokeza.
Kila wakati kuna fursa mpya inayokuwa inafanyiwa kazi.
Fursa zinaweza kuwa nzuri, lakini kama haziwekewi umakini na kufanyiwa kazi kwa muda mrefu, zinakosa maana.
Unapaswa kujua kusudi la biashara yako kisha kuweka malengo ya kufika kwenye kusudi hilo.
Baada ya hapo kuachana na mengi yanayokujia kila wakati na kuweka fokasi yako yote kwenye yale yaliyo muhimu zaidi.

Biashara inapaswa kuendeshwa kwa kasi kubwa.
Maamuzi yanapaswa kufikiwa na kufanyiwa kazi haraka.
Biashara nyingi hazifanikiwi kwa sababu ya mambo kwenda taratibu.
Mambo muhimu yanachelewa kufanyiwa maamuzi na hata baada ya kuamuliwa bado utekelezaji unakuwa wa kusua sua.
Unapaswa kuwa na kasi kubwa kwenye kuamua na kutekeleza mipango ya kibiashara.
Ushindani ni mkali, ukizubaa unaachwa nyuma.

Ni viwango gani umeweka kwenye biashara yako? Watu wanaisifia biashara hiyo kwa vitu gani vya kipekee?
Ni fokasi gani uliyonayo kibiashara? Ni mambo gani pekee unayofanya na kupuuza mengine yote?
Una kasi kiasi gani kwenye kuamua na kutekeleza? Inachukua muda mrefu kiasi gani kuamua na kufanya?
Jikague maeneo hayo matatu kibiashara na utaona kuna fursa ya kuboresha zaidi ili uweze kukuza biashara yako zaidi.

Kila biashara ina wigo wa kuboreshwa zaidi kwa kukuza viwango, kuwa na fokasi na kuongeza kasi ya kuamua na kutekeleza.
Wewe kiongozi wa biashara ndiye unayeweza kuwa kikwazo kwa ukuaji wa biashara kwa kupuuza maeneo hayo matatu muhimu ya ukuaji wa biashara.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe