2957; Utatu wa umasikini.

Rafiki yangu mpendwa,
Umasikini ni mbaya sana.
Kuna vitu vingi sana tunavyokutana navyo ambavyo vinadhihirisha umasikini na madhara yake kwetu.

Aliyekuwa raisi wa kwanza wa Tanzania, Mwl. J. K. Nyerere alichagua maadui wakubwa watatu ambao alishawishi kila mwananchi kupambana nao.
Maadui hao walikuwa ni Ujinga, Maradhi na Umasikini.
Pamoja na miaka mingi kupita tangu Nyerere kuainisha maadui hao, bado wameendelea kuwa mzigo kwa watu wengi.

Ukiwaangalia vizuri maadui hao watatu ambao Nyerere aliwaainisha, utaona kuna adui mkuu mmoja ambaye ni umasikini.
Ukiwa masikini, ujinga na maradhi vinakuwa na nguvu kubwa zaidi ya kukutikisa.
Ujinga na maradhi vinachangia sana kwenye umasikini, lakini pia ni zao la umasikini ambao watu wanakuwa nao.

Umasikini, ambaye tunaweza kumwita adui mkuu, unasababishwa na vitu vingi.
Lakini kuna vitu vikuu vitatu ambavyo huwa vinaambatana sana na umasikini.
Yaani popote penye umasikini, vitu hivyo vitatu huwa vinajidhihirisha wazi.

Kitu cha kwanza ni uvivu.
Tunaweza kusema uvivu na umasikini ni mapacha wa kufanana ambao wanaambatana pamoja kwenye kila jambo.
Masikini wana uvivu mkubwa sana ndani yao.
Wengine kwa nje wanaweza kuonekana kama ni wachapa kazi, lakini ni maonyesho tu.
Ndani yao hawapendi kile wanachofanya na wanatafuta kila sababu ya kutokufanya kazi.

Kitu cha pili ni kutokujiweza au kwa maneno rahisi uzembe.
Hapa watu wanakuwa hawana uwezo wowote wanaoweza kuuonyesha kwa wengine na wakaaminika.
Watu wanaweza kuonekana wanachapa kazi sana, lakini mambo wanayofanyia kazi ni ya kawaida sana, hakuna kinachowatofautisha na wengine.
Kwa kifupi masikini huwa wana uwezo mdogo sana wa kufanya mambo makubwa na ya tofauti.
Hawapendi kujaribu vitu vipya na vya tofauti.
Hivyo kwa kukosa uwezo wa kujitofautisha na wengine, masikini wanajikuta katikati ya kundi kubwa lenye ushindani mkali sana.

Kitu cha tatu ni ujinga.
Na huu ni tofauti na ule ujinga ambao Nyerere aliutaja. Nyerere alitaja ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika, na ndiyo maana elimu ya watu wazima ilishamiri zama hizo.
Lakini kwa zama hizi, karibu kila mtu anajua kusoma na kuandika.
Ujinga wa zama hizi ni watu kukosa maarifa ya nini wafanye na wafanye kwa kiwango gani ili waweze kutoka kwenye umasikini.
Ukiangalia kwa umakini, unaona masikini wakiwa ndiyo wanajiona wajuaji wakubwa.
Waambie wajifunze kwa kusoma vitabu na hatua nyingine muhimu na watakujibu hawana muda, au fedha. Kwa vyovyote wataashiria kujitunza siyo kipaumbele kwao.
Lakini wale wanaopiga hatua kubwa kwenye maisha yao na kuushinda umasikini huwa ni wanyenyekevu na wenye utayari wa kujifunza.
Wanapojifunza wanachukua hatua mara moja kwenye yale waliyojifunza, kitu kinachowapa matokeo ya tofauti.

Rafiki yangu mpendwa, mambo hayo matatu; Uvivu (Laziness), Uzembe (Incompetence) na Ujinga (Ignorance) ndiyo utatu mkuu wa umasikini, ambayo ukiwa nayo, hakuna namna unaweza kutoboa kutoka kwenye umasikini.
Utahangaika sana, lakini kama hutayavunja hayo matatu, utaishia pale ulipoanzia.
Ni mpaka uvunje utatu huo na kuusambaratisha ndiyo utaweza kupiga hatua kubwa unazotaka kupiga.

Kataa uvivu kwa kuwa mchapa kazi, jijengee nidhamu kali ya kazi na isimamie mara zote.
Ondokana na uzembe kwa kujijengea uwezo wa kipekee unaokutofautisha na wengine.
Na muige Socrates, mtu mwenye hekima sana kuwahi kupita hapa duniani, ambaye aliwahi kusema, kitu kipekee ninachojua ni kwamba sijui, hivyo kuwa tayari kujifunza. Ondokana na ujuaji, jifunze na chukua hatua ili kuyaboresha maisha yako.

Watu huusema sana umasikini, kwamba ni laana na mengine mengi.
Lakini utatu huu uliojifunza hapa ndiyo mzizi mkuu wa umasikini.
Yeyote anayeweza kuyavunja, hakuna namna anaweza kubaki kwenye umasikini.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe