2971; Uongozi, usimamizi na ufuatiliaji.
Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu ambaye anaajiri watu wa kumsaidia majukumu ya kibiashara, anajua changamoto nyingi ambazo anakutana nazo.
Imekuwa ni changamoto kubwa sana kupata wafanyakazi sahihi na kuweza kukaa nao kwenye biashara kwa muda mrefu.
Kumekuwa na maumivu, malalamiko, kukatishwa tamaa na kuvurugwa kwa wengi ambao wanaingia kwenye zoezi la kuajiri.
Wapo ambao wanaona ni bora waachane kabisa na zoezi la kuajiri na warudi kufanya kila kitu peke yao.
Lakini hilo siyo suluhisho, huwezi kukua bila watu. Pamoja na changamoto zao nyingi, bado unawahitaji sana watu.
Kwa muda mrefu tumekuwa tunaliangalia tatizo la wafanyakazi kama tatizo lao na siyo letu.
Tumekuwa tunalalamika wafanyakazi hawajiwezi, hawajui nini wanataka na hawataki kujifunza wala kujituma.
Mwishowe wanashindwa kazi na kukimbia.
Lakini kwenye maisha, kila jambo lina pande mbili. Na hili la changamoto ya wafanyakazi, pamoja na mapungufu waliyonayo, bado pia upande wa waajiri unachangia sana kwenye hilo tatizo.
Ndiyo, wewe unayeajiri pia una changamoto zako ambazo zinachangia wafanyakazi wanakuwa siyo wazuri na hatimaye kukimbia.
Kuna changamoto ya matarajio yasiyo sahihi. Unamwajiri mtu, ambaye haijui biashara yako kama wewe unavyoijua na hana maono makubwa uliyonayo halafu unategemea mara moja aanze kufanya kwa viwango vya juu unavyotaka wewe. Kwa kifupi ni kitu kisichowezekana, wanahitaji muda na mafunzo mpaka waweze kufanya kwa ubora unaotaka.
Pia kuna changamoto ya kushindwa kuelewa mahusiano ya msingi yaliyopo kati ya mwajiri na mwajiriwa. Kwa ndani kabisa haya ni mahusiano ya upinzani. Ajenda zako wewe mwajiri na ajenda za mwajiriwa ni tofauti kabisa.
Wewe unataka unaowaajiri wafanye kazi zaidi kwa malipo kidogo.
Waajiriwa wanataka wafanye kazi kidogo kwa malipo makubwa.
Kwa kushindwa kuelewa mahusiano haya ya msingi na kudhani mko upande mmoja inachangia sana kwenye changamoto zinazojitokeza.
Halafu kubwa kuliko yote ni kushindwa kutekeleza mahitaji makubwa matatu ya kuajiri, ambayo ni uongozi, usimamizi na ufuatiliaji.
Kwenye kuajiri kunahitajika uongozi. Uongozi unahusisha maono, mfano na hamasa. Kama kiongozi unapaswa kuwa na maono makubwa ambayo wafanyakazi wanavutiwa kuwa sehemu ya maono hayo. Unapaswa kuwa mfano kwa kila unachowaambia wafanye, usiwaelekeze tu kufanya, bali waonyeshe jinsi ya kufanya. Na zaidi, unapaswa kuweka morali yao juu kwa kuwapa hamasa endelevu, kuna wakati mambo yatakuwa magumu na wao kuelekea kukata tamaa, wape hamasa, hakikisha morali wao unakuwa juu. Kama wewe kiongozi utaonekana kukata tamaa, unaowaongoza wataona giza mbele yao.
Usimamizi ni muhimu sana kwenye kuajiri. Huwa tunadhani watu wanajua wanachopaswa kufanya, lakini ukweli ni hawajui. Ukiwaacha watu wafanye kile wanachotaka, unajua unachoishia kupata, ambacho ni hakuna, kwa sababu watu wakiachwa kwa utashi wao wenyewe, wanavurugwa na usumbufu na hakuna wanachofanya.
Unapaswa kuwapangia wafanyakazi kile wanachopaswa kufanya na kuwaelekeza namna ya kukifanya. Unapaswa kuwasimamia kwa karibu kuhakikisha kweli wanafanya na hawapotezwi na usumbufu mwingi unaowazunguka. Na pia unapaswa kuwasaidia kuendelea kuwa bora kwenye kile wanachofanya ili wawe na ufanisi mkubwa zaidi.
Ufuatiliaji ni kitu cha tatu muhimu kwenye kuajiri ambacho wengi sana huwa hawakizingatii.
Wengi hudhani kwa kuwa na usimamizi mzuri inatosha kuwafanya wanaowaajiri walete matokeo wanayopata. Na wanakuja kushangaa pamoja na kuwa na usimamizi mzuri, bado matokeo wanayopata siyo mazuri.
Ili kujihakikishia matokeo mazuri kwenye kuajiri, lazima uwe na ufuatiliaji mzuri na wa karibu sana kwenye yale yanayofanywa na wafanyakazi walioajiriwa.
Unaweza kuwaeleza vizuri wanachopaswa kufanya na kuwafundisha jinsi ya kufanya.
Kwa nje wanaweza kuonekana kama wanafanya, lakini matokeo wanayozalisha yakawa tofauti.
Hapo jua kwa ndani hawafanyi kama unavyoona kwa nje.
Ili ujue kile wanachofanya kwa ndani, lazima uwe na ufuatiliaji wa karibu. Lazima uweze kuona kila wanachofanya kwa undani na kujua usahihi wake.
Iko hivi, watu huwa wanaheshimu kile kinachokaguliwa, hivyo haitoshi tu kuwaambia watu cha kufanya, unapaswa pia kukagua ufanyaji wao. Ni kupitia ukaguzi wako ndiyo utaona wapi wanapaswa kuboresha.
Pia pale watu wanapojua wanakaguliwa, wanafanya kwa umakini mkubwa.
Leo kuwa mkweli kwako ili uweze kuvuka changamoto hiyo ya kuajiri inayokuandama.
Ni wapi umekuwa unakosea kama mwajiri?
Je umekuwa na matarajio ambayo siyo sahihi? Unabadilije hilo?
Je umekuwa unashindwa kuelewa mahusiano ya msingi kati ya mwajiri na mwajiriwa? Unakwenda kubadilije hilo?
Na je umekuwa unakosa uongozi, usimamizi na ufuatiliaji? Unakwenda kuchukua hatua gani hapo?
Weka maoni yako hapo chini ya hatua za tofauti unazokwenda kuchukua kwa upande wako ili kupunguza changamoto unazokutana nazo kwenye kuajiri.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Nimejifunza katika kuajiri, samaki huwa anaanza kuozea kichwani, tunataka mtu awe kama tulivyo sisi kwa mara moja na hakuna kanuni ya uongozi, usimamizi na ufuatiliaji. Kama ikifuatwa kama ulivyoshauri tutapunguza tatizo.
LikeLike
Kabisa,
Tunaweza kuwalaumu tunaowajiri, lakini tukiangalia tunayofanya sisi wenyewe, yanasikitisha.
LikeLike
Ni muhimu sana kufuata Kanuni ulizofundisha yaani uongozi, usimamizi na ufuatiliaji. Haya mambo 3 nimeendelea kuyaona hasa kwenye ajira ninayoifanya. Huwezi kupata mafanikio makubwa bila kutumia Kanuni hizi. Naendelea kujifunza Ili kuchukua hatua kwenye biashara yangu.
LikeLike
Asante sana kwa kushirikisha uzoefu wako kwenye hili.
Kwa hakika tujikumbushe kanuni hizi tatu mara zote,
Tuhakikishe tumesimama palipo sahihi, ili tuweze kujenga timu bora.
LikeLike
Nimejifunza jambo moja kubwa kama kiongozi ni muhimu sana kuhakikisha nakuwa mfano kwenye kila ninachokwenda kuwaelekeza wale ninaowasimamia wafanye hivyo mimi ndie niwe mfano nje ya hapo itskuwa changamoto kubwa katika kuongoza.
LikeLike
Kabisa, watu hawasikilizi unachowaambia, bali wanaangalia na kuiga unachofanya.
Tuzingatie sana hapo.
LikeLike
Mara nyingi wale tunaowaajiri hufanya Kwa kupokea maelekezo kutoka kwetu. Hivyo kama walikosea ni sisi tumeshindwa kusimamiwa.
LikeLike
Kabisa, lakini tunasahau hilo na kupeleka lawama kwao.
LikeLike
Kiongzi bora ni yule mwenye maono na kuyaeleza kwa anaowangoza, kusimamia utekelezaji, ukaguzi na ufuatiliaji.
LikeLike
Ndiyo.
LikeLike
Nimejifunza kwenye Uongozi tatizo linaanzia kwa Mwajiri lazima aonyeshe mfano wakuigwa kwa waaajiriwa wake ili mambo kwenda kwa usawa
LikeLike
Kabla hatujakimbilia kulaumu watu kushindwa kufanya, tujiulize kama tumekuwa mfano sahihi kwao.
LikeLike
Mtazamo na mategemeo kati ya mwajiri na mwajiriwa ni tofauti sana.
Nafikiri hili la mwajiriwa kutegemea zaidi kamisheni ni sehemu ya suluhisho.
LikeLike
Hata kamisheni bado haitatui tatizo lote kabisa.
Bado hayo matatu lazima yafanyike vizuri sana, la sivyo watashindwa, hata kama ni kwa kamisheni.
LikeLike
Nakwenda kuwa mfano bora kwao, kuwaonyesha maono makubwa na kuwapa hamasa kila mara
LikeLike
Safi, ongoza kwa mfano, utapunguza changamoto nyingi.
LikeLike
Nimejifunza na nimeelewa sababu ya wafanyakazi wengi niliochana nao chanzo ilikuwa ni Mimi kwa kuwa na matarajio ambayo sio sahihi. Pia kutokujua kwamba ajenda zangu na zao ni tofauti kabisa.
HATUA NITAKAZOCHUKUWA
Wote niliowaajili na nitaowaajiri nitawaogoza na nitakuwa mfano kwao pia kuwapa hamasa. Vile vile sintachoka kuwapa maelekezo na ufuatiliaji endelevu . Asante Sana kocha.
LikeLike
Vizuri, ongoza kwa mfano, kuwa na usimamizi mzuri na fuatilia kwa karibu.
LikeLike
Hakika katika hili nitajitahidi kuongoza kusimamia na kufatilia maono yangu na kuwafundisha wafanyakazi huku nikiwapa hamasa
LikeLike
Vizuri.
LikeLike
Nimekuwa nakosea katika kuajiri ,kwa kufanya maamuzi kwa hisia
Nitabadili kwa kujipa muda na kutoa mafunzo endelevu
Kuhusu mahusiano nitakuwa na mkakati sahihi
Nitaweka mfumo ili kuwa na uongozi,usimammizi na ufuatiliaji.
LikeLike
Vizuri, fanyia kazi hayo.
LikeLike
Kiongozi bora Lazima aonyeshe mfano na awe na maono,ni vzr kupitia somo hili nimejifunza juu ya uongozi,usimamizi na ufuatiliaji nahitaji kuyapitia mara kwa mara masomo haya.
LikeLike
Vizuri, fanya hivyo.
LikeLike
Nitazingatia mambo 3 katika Kuajiri wafanya kazi bora
LikeLike
Vizuri.
LikeLike
Asante sana kocha Kwa makala hii, mi Kwa upande wangu nilikuwa na udhaifu kwenye ufuatliaji hilo nimeliona na nalifanyia kazi pamoja na mambo mengine ya msingi yalioshirikishwa hapa
Asante
LikeLike
Sawa, fuatilia kwa karibu sana.
Unawaepusha kujijengea uzembe unaokuwa changamoto kwao.
LikeLike
Kosa kubwa kwangu ni kuwa na matarajio makubwa kutoka kwa mfanyakazi kuwa atakuwa anaweka kazi kwenye kila eneo kamaninavyoweka mimi kumbe yeye hana hiyo morali ya kuweka kazi hili limekuwa linapelekea kufukuza wafanyakazi,
Na kingine ni kutaka mabadiliko ya haraka kutoka kwa mfanyakazi kwamba nikimuelezabasi nione anabadilika kwa haraka kumbe nahitaji muda ili abadilike,
Jambo la mwisho ni la kujifunza kwa wafanyakazi hapa naona kuna ugumu sana kwani wafanyakazi wapya kwenye eneo la kazi wanakuwa mambo mengi hawajui, wanahitaji kujituma sana ili wayajui na kujifunza ila kumekuwa na ugumu sana kwenye kipengele cha kujifunza na huwezi kumlazimisha mtu ajifunze hili kwangu naona ni shida ya mtu na mtu anachagua mwenyewe kwenye kuiondoa au kubaki nayo. Hasa hasa kwa wafanyakazi wapya.
LikeLike
Vizuri Helanane,
Cha kuzingatia ni tabia tu, zilishakuwa sawa, mengine yanapaswa kuvumiliwa, kwa kuwapa uongozi mzuri, usimamizi na ufuatiliaji wa karibu.
LikeLike
Asante Sana kocha, hapa kitu kikubwa ni kuwafuatilia kwa ukaribu wafanyakazi baada ya kuwaajiri.
Kuwa na maono makubwa.
Kuwasimamia pia.
LikeLike
Ndiyo, tukishindwa kwenye hayo matatu, tutahangaika sana na wengi.
LikeLike
Mimi kama mmiliki na msimaizi wa biashara napaswa kufanya kwa mfano halisi yale ninayotaka wasaidizi wangu wayatekeleze kupitia kuona mimi nayatekeleza itawasukuma wao zaidi kutekeleza majukumu yao,
Pia nahakikisha nafuatilia kila kwa ukaribu kwenye utekelezJi wa majukumu yao ili niweze kuwarekebisha pale ambapo hawafanyi kwa usahihi
Pia napaswa kuwa na morali mkubwa mimi kama kiongozi hasa pale biashara inapokua katika changamoto ili kuwatia moyo hawa ninaowaongoza na kuwafanya wawe na morali pia mana watakua na imani kuwa changamoto itapita mana wananiona mimi nikiwa na morali wa juu.
Asante kocha
LikeLike
Hakika, watu hawasikilizi unachowaambia, bali wanaangalia na kuiga unachofanya.
LikeLike
Kwa upande wangu nitakua karibu na wafanyakazi kuwaonyesha njia kuwaelekeza na pia kuyakagua yale wanayofanya na mwisho kuona ni wapi warekebishe ili kupata matokeo bora zaidi nitaanza kukagua kila kitu ndani ya kazi yangu nashukuru sana kocha
LikeLike
Vizuri sana, zingatia haya, yataleta mabadiliko makubwa sana.
LikeLike
Nitafanya maamuzi ya biashara kwa kuzingatia kwamba hatari yote ya biashara kuanguka nimeibeba mimi.
LikeLike
Haya maoni umechanganya.
LikeLike
Nimetambua ulegevu wangu katika Uongozi,usimamizi na ufuatiliaji umekuwa kikwazo katika kujenga timu, changamoto ya wafanyakazi kuondoka nimeichangia Kwa kiasi kikubwa sana, nimekuwa nikijidanganya Kwa kuhisi nipo upande mmoja na wafanyakazi Kumbe siyo kweli,nimekuwa nikikosa msimamo katika ufuatiliaji na hapa nimekuwa nikikosa matokeo ninayoyataka.
Kuanzia Sasa nakwenda kuwa kiongozi Bora,msimamizi na mfuatiliaji katika majukumu yote ya wasaidizi wangu.
Asante Kocha.
LikeLike
Kuwa kiongozi bora, kuwa msimamizi mzuri na fuatilia kwa karibu.
Ukishindwa kwenye hayo matatu, hata ukapewa malaika kama wafanyakazi, bado utawapoteza.
LikeLike
Nimetambua ulegevu wangu katika Uongozi,usimamizi na ufuatiliaji umekuwa kikwazo katika kujenga timu, changamoto ya wafanyakazi kuondoka nimeichangia Kwa kiasi kikubwa sana, nimekuwa nikijidanganya Kwa kuhisi nipo upande mmoja na wafanyakazi Kumbe siyo kweli,nimekuwa nikikosa msimamo katika ufuatiliaji na hapa nimekuwa nikikosa matokeo ninayoyataka.
Kuanzia Sasa nakwenda kuwa kiongozi Bora,msimamizi na mfuatiliaji katika majukumu yote ya wasaidizi wangu.
LikeLike
Huwa tunadhani watu wanajua wanachopaswa kufanya, lakini ukweli ni hawajui.
Ukiwaacha watu wafanye kile wanachotaka, unajua unachoishia kupata, ambacho ni hakuna, kwa sababu watu wakiachwa kwa utashi wao wenyewe, wanavurugwa na usumbufu na hakuna wanachofanya.
Ahsante
LikeLike
Tuhakikishe tunawaelewesha watu kile wanapaswa kufanya.
LikeLike
Huwa tunadhani watu wanajua wanachopaswa kufanya, lakini ukweli ni hawajui.
Ukiwaacha watu wafanye kile wanachotaka, unajua unachoishia kupata, ambacho ni hakuna, kwa sababu watu wakiachwa kwa utashi wao wenyewe, wanavurugwa na usumbufu na hakuna wanachofanya.
Ahsante sana Kocha Dr. Makirita Amani.
LikeLike
Napaswa kuwa mstari wa mbele kwenye kutekeleza na kuwaelekeza ninaowaajiri ili wao waige ninachokifanya kama kiongozi wao,pia napaswa kuwaelekeza namna ya kutekeleza majukumu yao na kuwafuatilia kwa ukaribu ili kujua kama wanafanya kwa usahihi au wanaenda tofauti ili kuwarekebisha na kufanya kwa usahihi.
Sipasw kuwaacha wafanya kazi kwa namna wanavyofikiria wao,kwani wao hawana maono niliyo nayo mimi juu ya biashara yanu.
Asante sana kocha
LikeLike
Ukiajiri:
1. Hakikisha anajua majukumu yake.
2. MSIMAMIE.
3. Pima matokeo.
LikeLike