3018; Ushindi wa kiongozi.

Rafiki yangu mpendwa.
Ushindi wa kiongozi yeyote yule huwa unapimwa kwa matokeo anayozalisha.
Viongozi wote bora huwa wanazalisha matokeo makubwa.

Unaweza kuwa kiongozi mwenye huruma, anayejali na maarufu kwa wengi, lakini kama biashara yako itashindwa, hayo yote hayatakuwa na maana.

Kama biashara yako itashindwa, hakuna atakayejali wala kusikiliza sababu na visingizio unavyokuwa navyo.
Hakuna atakayejali kuhusu bahati mbaya ulizokutana nazo.
Kwa kifupi, matokeo yanapokuwa mabaya unakuwa huna popote pa kujificha.

Hayo yote yanaweza yasiwe sawa kwako kama kiongozi, lakini huna namna, utaendelea kuhukumiwa kwa matokeo unayozalisha, bila kujali ni mambo gani unayopitia katika kuzalisha matokeo hayo.
Hivyo ndivyo asili ilivyo, hivyo tunapaswa kwenda nayo hivyo.

Habari njema ni kwamba, kama utakuwa na unga’ng’anizi kwa muda mrefu, kama utaweka mkazo kwenye kutoa huduma bora sana kwa wateja na kama utajenga utamaduni wa nidhamu kali kwa wafanyakazi wako, italipa sana kwa muda mrefu.

Huwezi kuyaathiri matokeo moja kwa moja, lakini unaweza kuathiri moja kwa moja mambo hayo makubwa matatu yenye athari kwenye matokeo.

Unapaswa kuwa kwenye mchakato sahihi wa kukufikisha kwenye matokeo unayotaka kuyapata, kisha kukaa kwenye mchakato huo kwa unga’ng’anizi wa hali ya juu.
Kama mchakato ni sahihi, ni swala la muda tu kuhusu uzalisha matokeo unayoyataka. Anayeng’ang’ana zaidi ndiye anayepata ushindi mwishoni.

Unapaswa pia kuwapa wateja wako thamani kubwa sana na kuwawezesha kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao.
Kwa kujali na kuweka mbele maslahi ya wateja wako, unawafanya waendelee kuiamini biashara yako na kuendelea kuwepo pamoja na kuleta wateja wengine wengi zaidi.

Kujenga utamaduni wa nidhamu kali kwa wafanyakazi wako ni jukumu muhimu na ambalo ni gumu sana kwako kama kiongozi.
Watu huwa wanapenda kukaa na kufanya vile wanavyotaka wao wenyewe.
Lakini wanapokuwa kwenye biashara yako, kuna namna wanapaswa kuwa na kufanya.
Hilo linasaidia timu ya biashara kufanya kitu kwa ushirikiano na umoja ambao unakuwa na nguvu ya kuzalisha matokeo bora.

Ni vigumu sana kumshinda kiongozi anayejua kwa hakika nini hasa anachotaka, anayejua mchakato wa kupata anachotaka na kukaa kwenye mchakato huo kwa unga’ng’anizi bila kukata tamaa na anayejenga timu bora na yenye umoja na ushirikiano mkubwa.

KWA NINI, NINI na NANI ni maeneo makubwa matatu ya kila kiongozi wa biashara kujijenga kwa uimara.
KWA NINI ni kile unachotaka, maono ambayo biashara inayo, lazima yawepo na yawe na msukumo kwa kiongozi kuchukua hatua.
NINI ni mchakato wa kufika kule ambapo mtu anataka kufika. Kujua mchakato kamili na kuufuata ni hitaji muhimu sana.
NANI ni watu unaoambatana nao kwenye safari ya kufikia maono ya biashara. Unapaswa kuambatana na timu ambayo ni sahihi kwenye kutekeleza mchakato uliopo.

Kwa kuyakuza maeneo hayo matatu utaweza kuzalisha matokeo bora kabisa kama kiongozi.
Ni wajibu wako kuzalisha matokeo bora na siyo sababu au visingizio vyovyote.
Visingizio vinaweza kuwa rahisi kutamka, lakini mwisho wa siku kinachohesabiwa ni matokeo yaliyozalishwa.
Wewe kama kiongozi bora zalisha matokeo na siyo visingizio.
Uwe na safari njema ya uongozi kwenye biashara yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe