3104; Ishara moja, maneno matano. LAZIMA.

Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya malengo makubwa tunayoyafanyia kazi kwenye biashara zetu ni kujenga wateja waaminifu.
Wateja waaminifu ni wale wanaorudi tena kununua, wananunua kwa wingi na wanakupa wateja wa rufaa.

Huwa inashangaza pale unapoona biashara inakazana kutafuta wateja wapya kila wakati, huku kukiwa hakuna wateja wanaorudi tena kununua baada ya kununua mara moja.

Ili kuepuka hilo la wateja kutokurudi tena kununua, inahitajika kazi ya ziada ya kutoa huduma bora sana kwa wateja wote wanaonunua kwenye biashara.

Kuna nambo mengi ya kufanya kwenye utoaji wa huduma bora kwa wateja, lakini hapa tunakwenda kujifunza ishara moja na maneno matano ya LAZIMA kufanyia kazi kwa kila aliyepo kwenye biashara, kwa kila mteja na mara zote.
Mambo haya hayahitaji gharama yoyote ile kwenye kuyafanya, ila yana manufaa makubwa sana.

Mambo hayo ni ya LAZIMA kufanya na ni wajibu wako kuhakikisha kila aliyepo kwenye biashara yako anayafanyia kazi kwa uhakika mara zote anapokuwa anajihusisha na wateja.
Ni mambo yenye nguvu kubwa, hakikisha yanafanyika kwa uhakika kwenye biashara yako.

Ishara; TABASAMU
Kila aliyepo kwenye biashara yako, anawajibika kuvaa uso wa tabasamu muda wote anaokuwa anajihusisha na mteja.
Hii ni lazima, iwe mtu anajisikia au hajisikii, ni lazima akiwa na mteja awe na uso wa tabasamu.
Tabasamu ni ishara yenye nguvu kubwa ya kuwashawishi watu wakubaliane na wewe.
Huhitaji kulipa gharama yoyote ili uweze kutabasamu, lakini ni kitu ambacho kitakupa matokeo mazuri sana.

Neno la kwanza; SALAMU (HABARI/SHIKAMOO)
Salamu ni neno muhimu sana ambalo kila mtu aliyepo kwenye biashara anapaswa kulitumia kwa kila mteja mara zote.
Salamu ni kuonyesha kujali, hivyo kila mteja anapaswa kupewa salamu.
Hata kama mteja anaonekana kuwa na haraka, hakikisha huendelei na mengine kama bado hujamsalimia.
Salamu zinatumia neno HABARI kwa wale mnaoendana umri au umewazidi, wakati SHIKAMOO inaenda kwa wale waliokuzidi umri kwa kiasi kikubwa.
Salamu inafungua ukurasa mzuri wa mazungumzo.

Neno la pili; TAFADHALI
Kwa kitu chochote kile unachotaka kupendekeza kwa mteja, anza na nano TAFADHALI.
Tafadhali ni neno la kistaarabu linalomwonyesha mtu kwamba unamjali na kumthamini.
Unapotumia neno Tafadhali, unaondoa hali ya kuonekana unamlazimisha mtu kufanya vitu vya aina fulani.
Neno tafadhali linamfanya mtu aweke umakini kwenye kile anachokuwa anaelezwa.

Neno la tatu; ASANTE
Ni muhimu sana kumshukuru mteja kwa chochote anachokuwa amefanya kwako, hata kama hajajunua.
Mshukuru mteja kwa kutembelea biashara au kukupa nafasi ya kuongea naye kwenye simu au unapomtembelea.
Neno ASANTE lina nguvu kubwa sana ya kumfanya mtu aone kuna mchango mkubwa anaokuwa ameutoa.
Kila mtu kwenye biashara anatakiwa kutumia neno ASANTE kila anapozungumza na mteja.

Neno la nne; KARIBU
KARIBU ni neno la kwanza na la mwisho ambalo kila mteja anapaswa kuambiwa kila mara kwenye biashara yako.
Kila mteja anatakiwa kukaribishwa pale anapofika kwenye biashara au anapotafutwa kwa kutembelewa au kwa mazungumzo ya simu.
Pia kila mteja anatakiwa kukaribishwa tena kurudi pale mnapokuwa mmemalizana kwa wakati huo.
Pale mteja anaposhukuru kwa jambo lolote lile, anapaswa kuambiwa KARIBU.

Neno la tano; SAMAHANI
Pale inapotokea hali yoyote ya kutokuelewana vizuri na mteja, neno SAMAHANI ni lazima litumike, hata kama mteja ndiye mwenye makosa.
Ni wajibu wa yule anayemhudumia mteja kumwomba samahani kwa hali hiyo ya kutokuelewana na kuahidi jinsi anavyokwenda kusahihisha lile lililotokea.
Neno SAMAHANI pia linapaswa kutumika pale unapompa mteja mapendekezo ya tofauti na kile alichotaka yeye.
Mtu anaposikia neno samahani, anashusha chini silaha zake za mashindano na kuonyesha ushirikiano mkubwa.
Kila aliyepo kwenye biashara anapaswa kuwa mwepesi kuwaomba wateja SAMAHANI pale kunapotokea hali yoyote ya mteja kuonyesha kutokuridhishwa.

Ishara hiyo moja na maneno hayo maneno hayo matano ni lazima vitumike na kila aliyepo kwenye biashara kwa kila mteja.
Kama upo kwenye biashara peke yao jijengee tabia ya kuyatumia hayo kuwahudumia vizuri wateja wako.
Na kama kwenye biashara yako una wasaidizi, unapaswa kuhakikisha wote wanayatumia hayo kwa kila mteja wa biashara, mara zote.
Wafundishe waelewe jinsi ya kuyatumia na wakague kila mara kuhakikisha kweli hayo yote yanafanyiwa kazi.

Hayo mambo yanafanya kazi vizuri sana, kama yatafanyiwa kazi kwa uhakika.
Hivyo ni jukumu lako namba moja kuhakikisha kila mtu kwenye biashara yako anayafanyia kazi.
Yaelezeke vizuri na maanisha hasa kwamba kila mtu analazimika kuyafanyia kazi muda wote.
Siyo pale anapochagua yeye, wala pale anapojisikia, bali ni LAZIMA kuyafanyia kazi mara zote na kwa msimamo mkubwa.

Ni lazima wewe mwenyewe uwe na njia ya kumkagua kila mmoja ili kuona kama kweli anayafanyia hayo kazi kwa uhakika.
Hupaswi kubahatisha kwenye hilo, lazima uwe na uhakika mkubwa.

Mambo hayo ni ya kawaida kabisa na yanaweza hata kudharaulika, lakini nguvu yake ni kubwa sana.
Hakikisha yanafanyiwa kazi muda wote kwenye biashara na kila mtu kwa kila mteja mara zote kwa msimamo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe