3108; Kuepuka ushindani.

Rafiki yangu mpendwa,
Ushindani ni moja ya vikwazo vinavyowazuia watu wengi kupiga hatua kwenye maisha yao.
Ushindani mkali unawazuia watu wasipige hatua kubwa.

Pamoja na changamoto kubwa ya ushindani, bado ni kitu cha mtu kujitakia.
Yaani kama mtu anakabiliwa na ushindani, anakuwa amechagua yeye mwenyewe.

Huwa wanasema hakuna foleni kwenye njia iendayo kasi.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye ushindani, ni vigumu kuukuta kwenye njia iendayo kasi.

Hiyo ina maana kwamba ushindani ni kitu cha kujitakia, kwa kwenda kwenye njia iliyo na wengi, njia ambayo siyo ya kasi.

Kufanya kitu ambacho watu wengi wanakifanya na ukakifanya kwa namna ambavyo wengi hao wanakifanya ni kujipeleka wewe mwenyewe kwenye ushindani mkali.

Na pale unapojipeleka wewe mwenyewe kwenye ushindani, nafasi ya kushindwa ni kubwa, kwa sababu umeenda kwenye eneo ambalo watu wengine wako vizuri kuliko wewe.

Eneo lolote ambalo lina watu wengi huwa linakuwa na sifa kuu tatu; uvivu, ujinga na uzembe.
Hizo ndizo sifa ambazo kundi kubwa la watu huwa wanazo na ndiyo zinafanya ushindani kuwa mkali sana.

Uvivu ni kutokuwa tayari kujisukuma zaidi ya mazoea, ujinga ni kutokujua kilicho sahihi kufanya na uzembe ni kujua kinachopaswa kufanyika lakini kutokufanya.

Ukiamua tu kuachana na hayo matatu, yaani ukaacha uvivu, ujinga na uzembe, unakuwa umeachana na ushindani mkali.
Unakuwa umejitofautisha kabisa na kundi kubwa la walio wengi.

Amua kuchukua hatua kubwa na za kipekee kwenye kila unachofanya. Kamwe usitafute njia za mkato za kupata kitu chochote kile.
Jua hakuna mbadala wa kuweka kazi kwa juhudi ili kufanikiwa.
Ukiachana tu na uvivu, unakuwa umejitofautisha na kundi kubwa sana la watu.
Kwa kuamua kufanya kazi kwa juhudi kuliko wengine wote, kwa kukataa yeyote asikushinde kwenye kazi, unakuwa umewaepuka wengi wanaokimbizana na njia za mkato.

Kujifunza endelevu ni kitu unachopaswa kukisimamia bila kuyumba.
Haijalishi unajua nini, jua usiyojua ni mengi.
Haijalishi umepiga hatua kiasi gani, jua kuna hatua nyingine kubwa zaidi unazoweza kuzipiga.
Na hayo yote yatawezekana kwa kuendelea kujifunza vitu vipya na kuvijaribu.
Kwa kuacha kufanya kwa mazoea unakuwa umetengana na kundi kubwa linaloendesha mambo yake kwa mazoea.

Unapopanga kufanya kitu chochote kile, kifanye kama ambavyo umepanga kufanya, bila ya kujali umekutana na nini.
Tatizo la wengi kushindwa kufakiwa siyo kushindwa kupanga, kila mtu tayari anapanga sana.
Kinachowakwamisha wengi ni utekelezaji wa mipango ambayo tayari wameshajiwekea.
Wengi wana tabia ya kuweka mipango, lakini inapofika wakati wa utekelezaji wanaahirisha na kujiambia watafanya wakati mwingine.
Wewe kataa hilo kabisa, kataa kuahirisha mambo uliyoyapanga wewe mwenyewe.
Ukishapanga kitu, tekeleza kama ulivyopanga, bila kuruhusu chochote kukukwamisha.
Kuwa na msimamo wa hali ya juu sana kwenye kuamua na kufanya na utaepuka ushindani mkubwa wa wengi.

Watu wengi ni wavivu, wajinga na wazembe, hivyo wanajikuta kwenye ushindani mkali.
Ukiwa mchapa kazi, unayejifunza na kuchukua hatua na uliye na msimamo kwenye kutekeleza yote unayopanga, unakuwa wa tofauti na wa kipekee mno, unakosa kabisa ushindani kwenye yale unayofanya.

Uzuri kuepuka uvivu, ujinga na uzembe ni vitu ambavyo vipo ndani ya uwezo wako, vifanye kwa uhakika.
Kuepuka ushindani ni ushindi mkubwa na wa uhakika kwenye zama tunazoishi sasa, zama ambazo walio wengi wanajipeleka penye wengi tayari.

Kuwa mvivu, mzembe na mjinga ni kuchagua wewe mwenyewe kuwa na maisha ya hovyo.
Na hakuna kitakachoweza kukusaidia kwenye maisha kama umeingia kwenye hayo matatu.
Yaepuke kama ukoma kama unataka mafanikio makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe