3149; Miaka 100.

Rafiki yangu mpendwa,
Nikiwa mkubwa, nataka kuwa kama Charlie Munger 🤗🤗

Sababu ni 5;
1. Ni bilionea.
Mimi; Nitakuwa bilionea.

2. Ana miaka 99 na anaendelea kufanya kazi.
Mimi; Nitaishi zaidi ya miaka 100 na nitafanya kazi maisha yangu yote.

3. Muda mwingi wa siku yake (asilimia 80) anautumia kusoma.
Mimi; Nasoma angalau kitabu kimoja kila siku.

4. Ni mwekezaji wa kununua na kushikilia badala ya kucheza na soko la hisa.
Mimi; Naendelea kuwa mwekezaji bora bila kuhangaika na soko.

5. Amekuwa rafiki wa karibu wa Warren Buffet tangu mwaka 1959 (miaka 64 sasa) na wamekuwa washirika wa kibiashara na uwekezaji tangu mwaka 1978 (miaka 45 sasa). Katika kipindi chote hicho wamepata mafanikio makubwa (kuwa mabilionea) na hawajawahi kugombana.
Mimi; nitaendelea kuwa rafiki yako na mshirika wako wa karibu kwenye hii safari ya ubilionea, lazima tutoboe pamoja.

Siri ya kuishi maisha marefu na yenye furaha.

Charlie Munger alikuwa anahojiwa na mwandishi wa habari ambaye alimwambia watu wengi wamekuwa wanatafuta siri ya kuishi maisha marefu na yenye furaha.
Kabla hata mwandishi huyo hajamaliza kuuliza swali, Munger alimkatisha akisema hiyo ni rahisi.
Alieleza kwamba amekuwa akifuata sheria hizi sita;
1. Usiwe na wivu.
2. Usiwe na chuki.
3. Usitumie zaidi ya kipato chako.
4. Kuwa mchangamfu (mwenye shauku) hata kama una matatizo.
5. Jihusishe na watu wa kuaminika.
6. Fanya yale unayopaswa kufanya.

Munger anasisitiza kwamba ni vitu vya kawaida kabisa, ila vyenye nguvu kubwa sana.

Ahadi yangu kwenye kutekeleza sheria hizo za kuishi maisha marefu na yenye furaha na mafanikio makubwa;
1. Sitakuwa na wivu kwa mtu yeyote yule. Ninapoona wengine waliopata mafanikio makubwa nitawafurahia na kujifunza kutoka kwao ili na mimi nizidi kufanikiwa.

2. Sitakuwa na chuki kwa mtu yeyote yule. Kama naona mtu hana manufaa kwangu nitamwondoa kwenye maisha yangu. Sitakuwa na muda wa kujenga chuki naye. Na yeyote anayeamua kunichukia kwa sababu yoyote ile, hayo ni matatizo yake binafsi.

3. Sitatumia zaidi ya kipato changu. Hii ndiyo sheria ya kwanza ya mafanikio niliyojifunza, jilipe wewe mwenyewe kwanza. Na sijawahi kuivunja tangu nimejifunza. Imekuwa na manufaa makubwa sana kwangu. Nitaendelea kuizingatia daima.

4. Mara zote nitakuwa mchangamfu (mwenye shauku) hata kama kuna matatizo ninayoyapitia. Sitaruhusu mtu yeyote aone nimevurugwa na kitu chochote kile. Nitavaa uso wa tabasamu mara zote na kuwa na shauku kubwa ya kuyakabili maisha.

5. Nitajihusisha na watu wa kuaminika tu. Nitashirikiana na wale wanaothamini ninachofanya na wanaotekeleza kila wanachoahidi. Wale wanaofanya kile wanachosema watafanya. Na wanakifanya kwa viwango vya juu na kwa msimamo mara zote.
Mtu yeyote anayenipa sababu ya kutokumwamini, nitamwondoa kabisa kwenye maisha yangu.

6. Nitafanya yale ninayopaswa kufanya. Nitatimiza kila ninachoahidi, kwa viwango vikubwa na kwa msimamo. Nitaweka kipaumbele na juhudi kubwa kwenye yale niliyochagua kufanya. Nitayapenda sana na mara zote kwenda hatua ya ziada ili kutoa thamani kubwa zaidi. Nitahakikisha nawapa watu vitu ambavyo hawawezi kuvipata kwa mwingine yeyote ila mimi tu. Nitawafanya watu wanitegemee kwa uhakika kwenye maeneo niliyochagua kufanyia kazi, ambayo ni kusoma, kuandika na kufundisha.

Rafiki, hayo ndiyo mambo sita nitakayohakikisha kwa asilimia 100 nayaishi kila siku bila kuruhusu sababu yoyote kunikwamisha.
Na nina uhakika, bila ya shaka yoyote nitafikia sifa tano ambazo Charlie Munger ameweza kuzifikia kama nilivyoshirikisha hapo juu.

Na Munger hatuachi hivi hivi, bali anatupa ahadi hii;
“Hakikisha kila siku unayoimaliza unakuwa na hekima zaidi ya ulivyokuwa wakati unaamka. Kama utafanya hivyo kila siku bila kuacha na ukaishi maisha marefu, utapata kile unachostahili.” – Charlie Munger.

Kwa nukuu hiyo kuna vitu vitatu vya kuzingatia ili kupata kile unachotaka kwenye maisha;
1. Jifunze kila siku.
2. Weka kwenye matendo yale unayojifunza. (Ndiyo tofauti ya maarifa na hekima.)
3. Usife mapema, yaani hakikisha unaishi maisha marefu zaidi.
Hayo yote yapo ndani ya uwezo wetu, tuyatekeleze.

Rafiki yangu mpendwa, kwenye maoni hapo chini weka ahadi yako ya kuziishi sheria sita za Charlie Munger na jinsi unavyokwenda kuziishi kila siku.
Hilo ni zoezi muhimu kwa kila mmoja wetu kulifanya.
Lifanye sasa, shirikisha na liishi kila siku ya maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe