Mpendwa mstoa mwenzangu,

Sina uhakika kama itakufaa lakini wewe ni mtu mwenye bahati sana na ujasiri mkubwa mpaka hapa ulipofikia. Kwa sababu kuishi ni ujasiri mkubwa mno, mpaka hapa ulipo umeshavuka vikwazo vingi na umevipita.

Pata picha changamoto mbalimbali ulizoweza kukabiliana nazo. Ni wangapi walioshindwa kufikia hapo wewe ulipo? Unaona ni jinsi gani ulivyokuwa na bahati? Unaona ni jinsi gani ulivyokuwa na ujasiri?

Kila unachopitia kwenye maisha yako kinakuandaa kwa ajili ya kitu fulani. Maisha unayoishi yanakuandaa kuwa mtu fulani.

Mwanafalsa Seneca aliwahi kunukuliwa akisema, wakati mwingine hata kuishi ni kitendo cha ujasiri.

Kitendo cha wewe tu kuwa hai na kuendelea na maisha yako ni ujasiri mkubwa mno. Kwa sababu watu wengi wanaishia kufa au kuishi maisha wasiyoyataka kwa sababu ya kukosa ujasiri wa kuishi na kusikiliza sauti zao za ndani.

Hivi maisha yangekuwaje kama ungekosa ujasiri wa kujaribu vitu? Vitu vingi ulivyofanya kwenye maisha yako ni kwa sababu ya ujasiri uliokuwa nao. Kuwa na biashara tu ni ujasiri, ni wangapi mpaka wanakufa wanaogopa kufungua biashara? Ni wangapi wanaogopa kusimama mbele ya watu na kuongea? Ni wangapi ambao wanaweza kuwashawishi watu na kuuza kile alichonacho?
Kitendo tu cha kuweza kuwashawishi watu na kuwauzia ni ujasiri.

Mwanafalsa falsafa Aristotle anasema, kamwe huwezi kufanya kitu chochote kwenye hii dunia kama huna ujasiri.

Ujasiri una nguvu kubwa kwenye maisha yako. Bila ujasiri usingekuwa na hivyo ulivyo navyo leo. Bila ujasiri, huna utakachoweza kufanya.

Aliyekuwa waziri wa uingereza Winston Churchill aliwahi kusema, ujasiri ndiyo kitu ambacho kinatufanya sisi tusimame na kuongea juu ya jambo fulani. Na ujasiri ndiyo kitu ambacho kinatusukuma sisi kukaa chini na kusikiliza.

Kwa yeyote ambaye hana ujasiri, hawezi kukamilisha kitu chochote kwenye maisha yake. Unashindwa kukamilisha kile unachotaka kwa sababu bado hujaweza kuwa na ujasiri wa kukipambania kile unachotaka.

Hatua ya kuchukua leo; Kuwa na ujasiri. Bila ujasiri huna utakachoweza kufanya hapa duniani. Maisha yanahitajika ujasiri wako ili uweze kufanikiwa.

Maisha ni ujasiri, pambania kile unachotaka mpaka ukipate.
Kuwa jasiri, kumbuka kuishi tu ni kitendo cha ujasiri mkubwa.
Kitendo tu cha wewe kuzaliwa ni cha kijasiri na ili upate kile unachotaka kwenye maisha unatakiwa kuwa jasiri.

Kitu kimoja zaidi, ujasiri ndiyo fadhila yenye nguvu na mafanikio kuliko fadhila zote. Fadhila ya ujasiri ndiyo inaweza kukupa wewe chochote kile unachotaka.
BILA UJASIRI HUWEZI KUTOBOA WALA KUONEKANA SEHEMU YOYOTE ILE.
Ujasiri ndiyo ufunguo wa wewe kwenda kule unakotaka.

Rafiki na mstoa mwenzako,
Mwl. Deogratius Kessy