3209; Ngumu kutunza kuliko kutengeneza.

Rafiki yangu mpendwa,
Unapokuwa unaanzia chini kabisa, kiu yako kubwa inakuwa ni kufanikiwa na kufika juu.
Unakuwa tayari kufanya kila kinachopaswa kufanyika ili upate matokeo unayoyataka.
Safari inaweza kuwa ngumu, lakini kwa sababu ya kujitoa kweli kweli, unafika ulikokuwa unataka kufika.

Hapo sasa ndipo penye hatari kubwa sana kwenye maisha ya mafanikio.
Kwani baada ya kupata mafanikio fulani ndipo wengi wanajisahau, wanaacha kufanya yale yaliyowafikisha walikotaka kufika.
Matokeo yake ni watu kupata anguko kubwa kila baada ya mafanikio wanayokuwa wameyapata.

Kwa maneno mengine kutunza mafanikio ni kugumu kuliko kuyatengeneza mafanikio hayo.
Kuyatengeneza mafanikio kunahitaji mambo machache ambayo yanapaswa kufanyika kwa uhakika na msimamo.
Unapaswa kujua kwa hakika kile hasa unachotaka, kuamua kwamba utakipata na kisha kufanyia kazi mpaka kukipata.

Ukishakipata sasa, unakuwa hujamaliza matatizo yako, bali unakuwa umefungua matatizo mengine mapya kabisa.
Ambayo ni matatizo ya kutunza kile ambacho mtu ameweza kukitengeneza.

Wengi kwa kukosa mafunzo ya aina hii mapema, huwa wanajikuta kwenye mlolongo wa kutafuta na kupoteza.

Njia bora ya kuondokana na yote hayo ni kujifunza kuyatunza mafanikio kama unavyokazana kuyatengeneza.
Kwanza kwa kuhakikisha wale wanaotaka kunufaika nayo umewazuia wasiweze kujipenyeza.

Mafanikio kwa wengi imekuwa ni kitu kigeni kiasi kwamba wanapoyapata wanakuwa na mahangaiko makubwa.
Ni mahangaiko hayo ndiyo yanayowapelekea kupoteza mafanikio yanayokuwa yamepatikana.

Huwa kuna kauli inasema, Mungu akitaka kukuadhibu anakupa kile hasa unachotaka.
Inaweza kukushangaza hiyo imekaaje, lakini huhitaji hata kufikiria sana.
Wewe angalia tu mifano ya watu waliopata fedha nyingi kwa pamoja.
Labda ni mtu kashinda bahati nasibu, kapata urithi au mafao.
Tunajua kwa mifano halisia kwamba fedha hizo huwa hazidumu kwa muda mrefu.
Na zaidi, zinamwacha mtu akiwa kwenye hali mbaya kuliko alivyokuwa awali.

Kadiri unavyokazana kuyajenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako, ndivyo pia unavyopaswa kukazana kujifunza jinsi ya kuyatunza mafanikio hayo.
Weka mipango ambayo utaitekeleza hata kama utakuwa umeshapiga hatua kubwa.

Na muhimu zaidi, chagua mchakato ambao utauishi kwa maisha yako yote, iwe una mafanikio au huna.
Yafanye maisha yako yote kuongozwa na mchakato uliochagua na kamwe usiache kutekeleza mchakato huo bila kujali matokeo unayokuwa umeshapata.

Kinachowafanya wengi kushindwa baada kupata mafanikio kidogo ni kuuacha mchakato na kuishi maisha ya tofauti.
Hapo ndipo wanapojikuta wakirudi nyuma.

Wewe unajua vyema, wajibu wako namba moja ni kuendelea kukaa kwenye mchakato mara zote na kwa msimamo bila kuyumba.

Usikubali kupoteza kirahisi kile ambacho umehangaika sana kukipata.
Jifunze kutunza kama unavyokazana kutengeneza.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe